Saturday 24 May 2014

Adhabu dhidi ya Germain ni ujumbe kwa masalia ya FRPI: MONUSCO



Mwakilishi maalum wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC,  Martin Kobler amesema adhabu ya kifungo cha miaka 12 dhidi ya kiongozi wa kundi la waasi la FRPI nchini humo Germain Katanga ni ujumbe thabiti kwa masalia wake.
Kobler ambaye pia ni Mkuu wa ujumbe wa Umoja wa Mataifa nchini DRC, MONUSCO amesema kundi hilo la FRPI bado linaletekeleza vitendo vyake kwenye wilaya ya Ituri na kutishia usalama wa raia.

Martin Kobler (katikati) mkuu wa MONUSCO akiwa na baadhi ya maafisa na askari kutoka jeshi la serikali FARDC na lile la kuingilia kati mashambulizi, (FIB) walipofanya ziara karibu na eneo la Tongo, Mashariki mwa DRC

Hivyo amesema adhabu dhidi yake iliyotolewa na ICC inatuma ujumbe sahihi kwa wafuasi waliosalia na hivyo wasitishe mara moja vitendo vyao na wasalimishe silaha.
Kobler amesema kuchukua hatua dhidi ya vitendo vya ukwepaji sheria ni jambo muhimu katika kuleta utulivu DRC na kwamba MONUSCO inaendelea kusaidia ICC na mfumo wa sheria nchini humo ili kudhibiti ukwepaji sheria dhidi ya uhalifu wa aina hiyo.
Mahakama ya ICC ilimhukumu kifungo cha miaka 12 jela Germain Katanga baada ya kupatikana na hatia ya makosa matano kati ya Kumi.

No comments: