Monday, 26 May 2014

Wamisri waanza kupiga kura kuchagua rais wao mpya

Aliyekuwa mkuu wa majeshi wa Misri, Abdel Fatah al-Sisi ambaye anapewa nafasi kubwa ya kushinda uchaguzi wa mwaka huu.
Aliyekuwa mkuu wa majeshi wa Misri, Abdel Fatah al-Sisi ambaye anapewa nafasi kubwa ya kushinda uchaguzi wa mwaka huu

Wananchi wa Misri, leo Jumatatu na kesho Jumanne wanapiga kura kuchagua rais mpya, kwenye uchaguzi ambao aliyekuwa mkuu wa majeshi wa nchi hiyo, Jenerali Abdel Fatah al-Sisi anatarajiwa kushinda.

Al-Sisi anapewa nafasi kubwa ya kushinda kwenye uchaguzi wa mwaka huu kutokana na kuwa na uungwaji mkono karibu nchi nzima kufuatia mapinduzi aliyoyaongoza ya kumuondoa madarakani Mohamed Morsi wa chama cha Muslim Brotherhood.

Abdel Fatah al-Sisi aliyekuwa mkuu wa majeshi wa Misri na anawania kiti cha urais

 
 Jenerali Sisi anatarajiwa kumsinda mpinzani wake wa karibu anayepewa nafasi ya kutoa upinzani kwa kiongozi huyo, Hamdeen Sabbahi ambaye kwenye uchaguzi uliopita alikuwa mshindi wa tatu.
Mamia ya wananchi wa Misri wameonekana wakiwa kwenye misururu mirefu ya watu wakisubiri kufunguliwa na kisha kuanza kupiga kura kwenye vituo mbalimbali vilivyoko nchi nzima.
Al-Sisi mwenyewe amepiga kura kwenye kituo cha Heliopolis ambako alikutana na mamia ya wafuasi wake wanaomuunga mkono na kuanza kumzonga wakati akipiga kura yake.
Mji wa Cairo kwa mara ya kwanza ukilinganisha na uchaguzi uliopita umeshuhudia maelfu ya wananchi wakijitokeza kwenye vituo vya kupigia kura mapema zaidi licha ya hofu ya kiusalama ambayo imekuwepo katika mji huo hivi karibuni.
Sisi mwenyewe wakati wa kampeni zake aliahidi kuwa iwapo ataingia madarakani atahakikishakuwa analeta mabadiliko makubwa ya kiuchumi kwenye taifa hilo ambalo katika kipindi cha miaka mitatu iliyopita imekuwa vigumu kusimama kiuchumi.

Hamdeen Sabbahi kiongozi wa chama cha upinzani anayepewa nafasi ya kutoa upinzani kwa Jenerali, Al-Sisi
Kwaupande wake, Hamdeen Sabbahi ambaye amekuwa mshirika wa karibu wa Serikali ya Syria, amesema kuwa atahakikisha kunakuwa na usawa nchini humo pamoja na kumaliza utawala wa kijeshi ambao yeye mwenyewe aliunga mkono wakati rais Morsi akiondolewa madarakani.
Kwenye uchaguzi wa mwaka huu kilichokuwa chama kikuu cha upinzani chenye nguvu cha Muslim Brotherhood kimepigwa marufuku kushiriki kwenye uchaguzi wa mwaka huu baada ya kudaiwa kuhusika na makundi ya kigaidi nchini humo.
Uchaguzi huu unatarajiwa kumaliza miaka mitatu ya mzozo wa kisiasa nchini humo toka rais Morsi alipoangushwa madarakani ambapo kumekuwa na hali ya sintofahamu kuhusu suala la demokrasia nchini humo.

Aliyekuwa mkuu wa majeshi wa Misri, al-Sisi akisalimiana na rais wa Urusi Vladmir Putin alipofanya ziara nchini humo
Wananchi wa taifa hili wanashiriki uchaguzi huu huku kukiwa na kumbukumbu ya kuuawa kwa wafuasi zaidi ya 1400 wa aliyekuwa rais wa taifa hilo Mohamed Morsi ambaye anakabiliwa na kesi ya uhaini na kuchochea machafuko nchini humo.
Hata hivyo mashirika ya kutetea haki za binadamu nchini humo yanasema kuwa licha ya mapinduzi yaliyofanyika bado nchi hiyo itasimama kidemokrasia na kwamba hivi sasa maisha ni mazuri zaidi ukilinganisha na hali ilivyokuwa wakati wa utawala wa Hosni Mubarack.

No comments: