Sunday, 25 May 2014

UKAWA yainyima CCM usingizi

Waziri  Sophia Simba na Naibu Waziri Janet MbeneUMOJA wa Katiba ya Wananchi (UKAWA), ulioanzishwa wakati wa Bunge la Katiba, umekuwa mwiba kwa Chama Cha Mapinduzi (CCM) ndani na nje ya Bunge,

Tayari umoja huo unaoundwa na vyama vya CHADEMA, CUF na NCCR-Mageuzi, umeshaweka wazi dhamira yake ya kusimamisha mgombea mmoja katika ngazi tofauti kwenye uchaguzi mkuu unaotarajia kufanyika mwakani.
Kauli hiyo inaonekana kuzidisha hofu kwa CCM, ambayo kwa miaka mingi imekuwa ikifurahia msambaratiko wa upinzani ili ipate nafasi ya kutawala.
Kuimarika kwa UKAWA, kumetishia chama hicho tawala ambacho kinadaiwa kupanga mikakati ya kuwadhoofisha, ikiwemo kuwatumia makada wanaotoka kwenye vyama vinavyounda umoja huo.
Mabadiliko yaliyofanywa na kiongozi wa kambi rasmi ya upinzani bungeni, Freeman Mbowe, katika baraza lake la mawaziri vivuli kwa kuwaingiza wajumbe kutoka NCCR-Mageuzi na CUF, yamezidisha hofu kwa CCM.
Awali baraza kivuli liliundwa na wabunge wa CHADEMA, lakini baada ya UKAWA kuanzishwa, viongozi wa vyama husika waliamua kuimarisha umoja wao.
Uimara wa UKAWA umeanza kutishia mijadala ya Bunge la  Bajeti linaloendelea Dodoma, ambako wabunge wake wamekuwa mwiba kwa mawaziri wanaowasilisha hotuba za bajeti zao.
Uchunguzi uliofanywa na gazeti hili umebaini kuwa UKAWA wamekuwa na ushirikiano mkubwa kuanzia wakati wa kuandaa hotuba za bajeti zao kivuli wakati wa mijadala na hata kuuliza maswali.
Kama sio wingi wa wabunge wa CCM kupitisha hoja zao kishabiki, baadhi ya bajeti za wizara zilizokwishasomwa na kupitishwa, zingekwama.
Baadhi ya mawaziri waliowasilisha bajeti zao, wamekiri walipomaliza hotuba zao kwamba wamepata wakati mgumu kwa UKAWA kuliko wakati mwingine wowote.
Mmoja wa mawaziri hao, Sophia Simba ambaye ni Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto, alisema nje ya ukumbi wa Bunge mara baada ya kupitishwa kwa bajeti yake kwamba hajawahi kupata wakati mgumu kama mwaka huu alivyopata kutoka kwa UKAWA.
“Bajeti yangu imepita, lakini wale wabunge wa UKAWA walinibana sana, waliniweka pabaya sana, nashukuru Mungu imepita,” alisema Waziri Simba wakati akipongezwa na baadhi ya mawaziri, wabunge na maofisa wa wizara yake.
Hata baadhi ya mawaziri ambao hawajawasilisha bajeti zao, hofu yao imekuwa kwa wabunge wa UKAWA ambao hutumia muda mwingi kusoma na kuibuka na hoja nzito ambazo mara nyingi zimekuwa mwiba.
Spika wa Bunge, Anne Makinda, ni miongoni mwa makada walioonekana kutishwa na mabadiliko ya baraza kivuli ambapo alisema jambo hilo limefanyika kwa kuchelewa.
Makinda, alimnanga Mbowe kuwa amefanya mabadiliko hayo kwa kuchelewa kwa kuwa alishawahi kumshauri aunde baraza lenye muungano wa wabunge wa upinzani, lakini alipuuza na kuteua wa CHADEMA pekee.
Spika huyo aliifananisha hatua hiyo ya Mbowe, sawa na kukumbuka kujifunika shuka wakati kumeshakucha.
Baadhi ya wachambuzi wa masuala ya kisiasa walibainisha kauli hiyo ilionyesha kiongozi huyo ameanza kujawa na hofu juu ya mustakbali wa chama chake.
Makinda pia amekuwa akiwakataza wabunge kutoka umoja huo kujitambulisha wanatoka UKAWA bali wajitambulishe kutoka kambi rasmi ya upinzani.
Kiongozi huyo amekuwa akiwaambia wabunge wa UKAWA kuwa umoja wao uishie kwenye Bunge Maalumu la Katiba na wasiuingize kwenye Bunge la Bajeti.
Hofu kwa CCM
UKAWA wamekuwa gumzo kiasi cha kuwafanya vigogo wa CCM, wanaofanya ziara zao mikoani kutumia muda mrefu kuwazungumzia huku wakiulaani umoja huo.
Katika ziara hizo zinazoongozwa na Katibu Mkuu wa CCM, Abdulrahman Kinana na Katibu wa Itikadi na Uenezi, Nape Nnauye, UKAWA wameteka mijadala ya wanachama, viongozi na mashabiki wanaohudhuria mikutano ya chama tawala.
Katika mikutano hiyo, Nape amekuwa akipinga kufanywa kwa mazungumzo yenye lengo la kuwashawishi wajumbe wa umoja huo warejee kwenye Bunge la Katiba walilosusia vikao vyake mwezi uliopita.
Wataka viongozi kuelekea uchaguzi mkuu mwakani
Viongozi wa vyama vinavyounda umoja huo, wako kwenye ziara mikoani wakifanya mikutano ya hadhara kuelimisha umma namna mchakato wa katiba mpya unavyohujumiwa na CCM.
Viongozi wa UKAWA wamegawanyika katika makundi, moja likishambulia kwa mikutano ya hadhara katika mikoa ya Nyanda za Juu Kusini likiongozwa na Mwenyekiti wa CUF taifa, Profesa Ibrahim Lipumba.
Kundi jingine liko mikoa ya Kanda ya Kaskazini wakitoa elimu kuhusu mchakato wa katiba.
Katika mikutano yao ya hadhara, UKAWA walipata maelfu ya watu na kuna wakati polisi wamekuwa wakitumika kuidhibiti.
Duru za siasa zinasema kuwa hofu ya CCM kwa sasa ni kama ushirikiano huo utaendelea hadi 2015 ambapo UKAWA wamepanga kusimamisha mgombea mmoja kuanzia ngazi ya urais, ubunge na udiwani, kwamba chama hicho tawala kitakuwa na wakati mgumu.
Ni kutokana na kasi hiyo, CCM imepanga kupitia kwenye maeneo yote ambayo UKAWA wamepita, kujibu mapigo.

No comments: