Monday, 26 May 2014

Ulimboka mwakingwa amshangaa Julio kugombea umakamu Rais

Jamhuri Kihwelo ‘Julio’
 MIONGONI mwa wachezaji wenye heshima kubwa na wanaokubalika miongoni mwa wanachama wa Simba katika kipindi cha miaka 10 iliyopita, yumo Ulimboka Mwakingwe.
Straika huyo wa zamani ambaye kwa sasa anaishi Morogoro na familia yake, ameibukia na kudai kushtushwa kwake na uamuzi wa kocha mahiri wa zamani wa Simba, Jamhuri Kihwelu ‘Julio’ kuwania Umakamu wa Rais wa klabu hiyo.
Mchezaji huyo amedai kwamba beki huyo wa heshima wa Simba, bado hajaiva kiasi cha kuwa kiongozi wa timu kubwa kama Simba.  Ulimboka alidai kushangazwa na uamuzi wa Julio wa kuwania nafasi hiyo bila kujipima kwani anaamini hana sifa stahili.
Ulimboka alisema: “Namuheshimu Julio kwa kuwa ni kocha wangu wa zamani na kaka yangu lakini uamuzi wake wa kuamua kugombea nafasi ya makamu wa rais ni kufurahisha nafsi yake ambayo kamwe ndoto yake haiwezi kutimia hata kidogo.”
“Nina mashaka na washauri wake ambao ndiyo waliomshawishi kuchukua fomu, najua hawezi kuambulia lolote katika uchaguzi huo. Tuache utani jamani kwenye mambo ya msingi, Julio anawezaje kuwa kiongozi wa Simba?
“Kila mtu anajua tabia ya Julio hasa sisi Simba, inawezekanaje baadaye aonekane kiongozi Simba? Nafikiri washauri wake hawakumshauri vizuri hadi akachukua fomu mbaya zaidi anagombea nafasi kubwa kama hiyo ya makamu wa rais.”
Julio ambaye anakubalika Simba kutokana na kunusuru benchi la ufundi kila makocha wanapotimuliwa, anawania nafasi hiyo katika Uchaguzi Mkuu wa Simba utakaofanyika Juni 29, mwaka huu akichuana na Swed Mkwabi, Wilbard Mayage, Geofrey Nyange ‘Kaburu’, Joseph Itang’are ‘Mzee Kinesi’ na Bundala Benedict.
Alipotafutwa Julio alisema: “Kila mtu ana maoni na mtazamo wake, mimi natumia haki yangu kugombea.”

No comments: