Thursday 22 May 2014

Safari ya Mbeya City kwenda Sudan yaingiliwa na Mdudu

Hatma ya safari ya timu ya Mbeya City kutoka jijini Mbeya kuelekea Sudan kwa ajili ya kushiriki mashindano mapya ya Kombe la Nile Basin yanayotarajiwa kuanza leo mjini Khartoum haijajulikana, imeelezwa.

Akizungumza na gazeti hili, Katibu Mkuu wa Mbeya City, Emmanuel Kimbe, alisema kuwa hadi jana mchana walikuwa hawajapokea tiketi hizo za kuelekea Sudan ili kupeperusha vyema bendera ya Tanzania Bara katika mashindano hayo.

Kimbe alisema kuwa timu yao inaendelea na mazoezi yake kwenye Uwanja wa Karume, Ilala jijini na mara safari hiyo itakapokamilika wataondoka kuelekea Sudan.

"Yaani hadi muda huu (jana mchana) bado hatujaambiwa chochote, timu inaendelea na mazoezi huku tukisubiri kupewa maelekezo na viongozi wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) ambao ndiyo wanawasiliana na viongozi wa Shirikisho la Soka Afrika Mashariki na Kati (CECAFA).

Gazeti hili lilipomtafuta Katibu Mkuu wa CECAFA, Nicholas Musonye, kutaka kufahamu hatma ya safari ya Mbeya City, kiongozi huyo ambaye ni Mkenya, hakupatikana katika simu yake ya mkononi.

Hata hivyo, inaelezwa kuwa Chama cha Soka cha Sudan (SFA) ndiyo wanaotakiwa kushughulikia tiketi za timu na viongozi wanaoelekea nchini humo kwa kushirikiana na serikali yao iliyodhamini michuano hiyo.

Mechi za ufunguzi za mashindano hayo leo zitakuwa ni kati ya Victoria University dhidi ya Malakia na baadaye usiku wenyeji El Mereikh itawakaribisha Polisi kutoka Uganda timu hizo zote ziko kundi A.

Timu nyingine zinazoshiriki mashindano hayo zilizoko kundi C ni pamoja na Al Ahly Shandy, Al Masry ya Misri, Defence na Dhikil huku kundi D likiwa na Hey Al Arab, Arab Contractors, Flam beaude L'EsT ya Burundi na Etincelles ya jijini Kigali, Rwanda.

Mbeya City ambayo iko kundi B inatakiwa kuanza kampeni za kuwania ubingwa huo kesho Alhamisi kwa kuwavaa El Mereikh Al Fashery na baadaye kucheza dhidi ya AFC Leopald ya Kenya Mei 25 na kumaliza mechi zake za hatua ya makundi kwa kukutana na Elman ya Somaliza Mei 27.

No comments: