Thursday, 15 May 2014

Nimeteseka miaka 17, Watanzania naombeni Msaada wenu

Kijana Amos Ng’arare Sasi (21) mkazi wa kijiji cha Kizaru wilayani Musoma Vijijni
Kijana Amos Ng’arare Sasi (21) mkazi wa kijiji cha Kizaru wilayani Musoma Vijijni amepoteza mwelekeo wa maisha baada ya ndoto yake ya kusoma hadi chuo kikuu kuishia njiani kutokana na matatizo ya ugomjwa wa ajabu ambao umemtesa kwa kipindi cha miaka 17.
Kwa kipindi hiki kijana Amos, ambaye anatoka Kata ya Mryaza, amelazwa Hospitali ya Taifa Muhimbili kwa ajili ya matibabu, lakini matarajio ya kupona kwa tiba za hapa nchini hayapo hivyo njia pekee iliyobaki ni kwenda nchini India kwa matibabu zaidi.
Katika mahojiano na Ukombozi wiki iliyopita akiwa Wodi Namba 21, Sewahaji, Amos alionekana mwenye mawazo kupita kiasi.
“Ndoto yangu ya elimu itakuwa imeishia hapa. Sitegemei kurudi tena. Wenzangu niliokuwa nikisoma nao darasa moja, kwa sasa wapo kidato cha nne. Nilizaliwa nikiwa sina tatizo la aina yoyote kiafya na nililelewa na wazazi wote wawili. Kwa kweli kwa malezi niliyoyapata, sikuwahi kujiona tofauti,” anasema.
“Nikiwa na miaka minne baba alifariki dunia, nikabaki na mama ambaye alitulea mimi na kaka yangu kwa furaha akijishughulisha na kilimo cha jembe la mkono,” anasema Sasi.
“Baadaye tulibaki wawili tu, yaani mimi na mama baada ya kaka kuondoka kwa madai kuwa anakwenda kutafuta maisha. Ilikuwa mwaka 1998 na mpaka leo hatujawahi kumuona wala kusikia taarifa zake,” anasimulia Sasi.
Anasimulia kuwa alipofikisha umri wa miaka minne, usoni kwake kuliota kitu kama kipele ambacho alisema kilikuwa kinamuwasha sana.
Anaongeza kuwa mama yake alimpeleka hospitali ambako alipewa dawa za kupunguza maumivu tu.
“Nilipofikisha umri wa miaka tisa hali ilizidi kwa mbaya, maumivu na uvimbe ukazidi,” anasema.
“Mama alinionea huruma akawa halali pale anapoona nalia kutokana na maumivu makali. Aliamua kunipeleka hospitali ya Musoma lakini hakukuwa na mabadiliko. Mwaka 2010 alinipeleka Hospitali ya Bugando mkoani Mwanza, huko nilifanyiwa uchunguzi, lakini ugonjwa haukujulikana.”
Anasema wakati huo matokeo ya shule ya msingi yalikuwa yametoka naye alifaulu kwenda kidato cha kwanza, lakini alishindwa kutokana na kuzidiwa na maumivu.
“Nilirudishwa nyumbani, nikawa sipati huduma ya aina yoyote. Watu walioniona walinionea huruma, wengine wakawa hawataki kuniona mitaani. Walinitishia kuwa nikionekana, nitakamatwa na wachimba madini wanichinje wachukue viungo wakafanye manbo ya kishirikina wapate madini kwa wingi,”
“Baadhi ya wananchi walinionea huruma. Walinichangia fedha ili nije Muhimbili nipate matibabu.”
Anasema alifika Muhimbili Septemba, 2011 na madaktari walichukua vipimo na kumwambia arudi mwezi mmoja baadaye.
“Hata hivyo sikuweza kurudi kipindi hicho kutokana na kukosa nauli. Namshukuru mbunge wetu Nimrod Mkono na diwani wetu walinisaidia nauli ya kuja. Nikaja mwezi wa pili mwaka huu. Walinipima kwa mara ya pili na kunieleza kuwa kuna mshipa wa fahamu unapitisha damu nyingi hivyo natakiwa kufanyiwa upasuaji nchini India.
“Wakati fulani ninapata maumivu hadi napoteza fahamu. Nasikitika hali hii huwa inanikuta nikiwa peke yangu na mama anapenda sana kuja kuniona, lakini anashindwa kwa sababu ya kukosa nauli.
“Nawashukuru sana madaktari kwa kuwa karibu nami na kunipa dawa za kupunguza maumivu. Pia wauguzi wamekua nami kwa kunisaidia na kuniliwaza. Ninawapongeza ila kinachoniuma ni pale ninapowaona wagonjwa wanatembelewa na ndugu zao, lakini kwa upande wangu hakuna hata mtu mmoja,” anasema kijana huyo.
“Nawaomba Watanzania wanisaidie kwa msaada wowote hata kwa kuniombea, ili Mungu anisimamie nipelekwe India nitibiwe.
“Mimi ni kijana mdogo ninayetamani kurudi shule na kufanya shughuli nyingine za maendeleo.”
Kwa atakayeguswa na tatizo la mtoto huyu anaweza kuwasiliana na ofisi za Mwananchi au kupiga simu namba 0688551355.
Chanzo Cha Habari Ni Mwananchi Communication News

No comments: