Sunday 25 May 2014

Hakimu Kortin kwa kupokea rushwa

TAASISI ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) wilayani Bunda, Mara imemfikisha mahakamani Ofisa Mtendaji wa Kijiji cha Kibara A, Witness Lameck (38) kwa tuhuma ya kuomba na kupokea rushwa kutoka kwa wavuvi.
Ofisa mtendaji huyo ameunganishwa kwenye kesi hiyo inayomkabili pia Hakimu wa Mahakama ya Mwanzo Kewnkombyo, Emmanuel Mng’wale (37), aliyefikishwa mahakamani hapo Mei 19 mwaka huu, kwa tuhuma hiyo.
Akiwasomea mashitaka yao mbele ya Hakimu wa Mahakama ya Wilaya ya Bunda, Hamad Kasonso, Mwanasheria wa Takukuru, Eric Kiwia alisema washitakiwa wote walitenda kosa hilo kati ya Aprili 22 na 23 mwaka huu.
Kiwia alidai hakimu huyo aliandika hati bandia na kugonga mhuri wa mahakama na sahihi yake na kisha kumpatia ofisa mtendaji huyo, ili azipeleke kwa wavuvi kwamba wanashitakiwa kwa makosa ya uvuvi haramu.
Alidai kuwa hati hizo zililenga kuwabambikizia kesi wavuvi hao na kuwatisha ili watoe rushwa kati ya sh 60,000 hadi 150,000.
Ilidaiwa mahakamani hapo na wakili huyo kwamba ofisa mtendaji huyo alizisambaza hati hizo kwa wavuvi hao huku akiwaomba watoe kiasi hicho cha fedha, ili kesi zao zifutwe, vinginevyo wangehukumiwa kifungo ch miezi sita jela.
Kwa mujibu wa wakili huyo, baadhi ya wavuvi walitoa kiasi hicho cha fedha huku wengine wakitoa taarifa Takukuru, ambako uchunguzi ulibaini kuwa hati hizo ni bandia kwa vile watuhumiwa hawakuwa na kesi zinazowahusu.
Washitakiwa wote walikana mashitaka yao na kupewa dhamana hadi Juni 16 mwaka huu kesi hiyo itakapotajwa tena mahakamani hapo.
Kwa mujibu wa Takukuru wilayani hapa, wavuvi waliotoa rushwa hiyo inasadikika ni wengi na kuongeza kuwa taasisi hiyo imeamua kushirikisha wavuvi watano kwa ajili ya ushahidi katika kesi hiyo.

No comments: