Wednesday 28 May 2014

UDA yawavua wabunge nguo

 Waziri wa Uchukuzi, Dk. Harrison Mwakyembe SAKATA la umiliki wa Shirika la Usafiri jijini Dar es Salaam (UDA), limeiingiza serikali katika aibu ya mwaka, huku mawaziri na wabunge ‘wakivuana nguo’ bungeni.
Hali hiyo iliyosababisha baadhi ya wabunge kuishambulia serikali, ilitokea juzi wakati wa mjadala wa hotuba ya Bajeti ya Wizara ya Uchukuzi kwa mwaka wa fedha 2014/2015.
Waliohitimisha mnyukano huo kwa kauli za kuumbuana ni Waziri wa Uchukuzi, Dk. Harrison Mwakyembe na Naibu Spika Job Ndugai.
Dk. Mwakyembe, akihitimisha mjadala huo, alisema suala la umiliki wa UDA halina uhusiano na wizara yake, hivyo alimlaumu Naibu Spika Ndugai, kuruhusu mjadala huo kwenye wizara yake, huku Naibu Spika huyo akifoka na kusisitiza wizara hiyo inahusika.
Awali kabla ya mzozo wa UDA haujaanza juzi, Waziri Mwakyembe, wakati akijibu hoja za Waziri Kivuli na Msemaji Rasmi wa Kambi ya Upinzani wa wizara hiyo, Moses Machali (NCCR-Mageuzi), aliyehoji sakata la UDA, aliweka bayana kwamba suala la umiliki wa shirika hilo halihusu wizara yake.
Hata hivyo, pamoja na kuweka angalizo hilo mapema na wakati Bunge likiendelea, Mbunge wa Nzega, Dk. Khamis Kingwangala (CCM), aliliibua sakata hilo na kusema kuwa mmiliki wa UDA, Robert Kisena, alinunua kihalali.
Dk. Kingwangala, alitoa kauli hiyo akijua fika kwamba siku chache zilizopita, Spika wa Bunge, Anne Makinda, alilipeleka suala la UDA mbele ya Kamati ya Haki, Kinga na Madaraka ya Bunge kumhoji Kisena kwa kauli yake kwamba wabunge waliopinga umiliki wa UDA, wamehongwa na mwekezaji wa nje anayetaka kuinunua.
Sambamba na hilo, Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), Frederick Werema, amepata kuliambia Bunge wiki iliyopita kuwa sakata la umiliki wa UDA limepelekwa tena mbele ya Taasisi ya Kudhibiti na Kuzuia Rushwa (Takukuru) na Mkurugenzi wa Mashitaka (DPP) kwa hatua zaidi za kisheria.
Mbali na viongozi hao, Naibu Waziri wa Fedha na Uchumi, Adam Malima, wiki iliyopita wakati akijibu swali la Mbunge wa Kawe, Halima Mdee (CHADEMA), alisema UDA inamilikiwa na serikali kwa asilimia 49 ya hisa na Jiji la Dar es Salaam asilimia 51, na kwamba mmiliki wa sasa, Kampuni ya Simon Group chini ya Kisena hana umiliki wa hisa.
Akijenga hoja yake juzi bungeni, Dk. Kingwangala, alisema mmiliki wa UDA, Kisena amekuwa akinyanyaswa kutokana na kauli tata za serikali.
Huku akisoma nyaraka za kuhalalisha umiliki wa UDA kwa Kisena, mbunge huyo alitaka serikali itoe kauli juu ya sakata hilo na kama asingepata majibu ya kuridhisha, angekwamisha Bajeti ya Wizara ya Uchukuzi.
Hoja hiyo iliungwa mkono na wabunge wengi, akiwemo Mbunge wa Mwibara, Kange Lugola (CCM), aliyemshangaa Waziri Mwakyembe kwamba suala la UDA halihusiani na wizara yake.
Lugola, alisoma moja ya barua ya Wizara ya Uchukuzi wakati huo ikiitwa Wizara ya Miundombinu, ikitoa maelekezo kuhusu suala la UDA, hivyo alisisitiza kuwa wizara hiyo inahusika na kumtaka waziri atoe kauli juu ya mzozo huo.
Huku akishangiliwa na baadhi ya wabunge, Lugola alisema mwekezaji huyo amekuwa akizungushwa kama mchezo wa ‘Joyce Wowowo’ huku wizara husika zikitupiana mpira.
Alisema wenye hisa, yaani Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam wameamua kuuza hisa zao kwa Kisena, lakini aliishangaa serikali imekuwa ikitoa maelezo aliyoyaita ya kukengeuka.
Wakati mzozo ukiendelea, Waziri Malima alisimama kutoa ufafanuzi wa kauli yake ya awali ya umiliki wa hisa za UDA ambapo alisisitiza kuwa serikali haimtambui Kisena kwani alilinunua shirika hilo kiujanja.
Mpira wa hoja hiyo ulimrukia Mbunge wa Kilwa Kaskazini, Multazar Magungu (CCM), aliyesema kama mnunuzi alikosea, serikali imlipe fidia na kulirudisha shirika hilo mikononi mwake na kisha kuliuza upya.
Alisema kwa sasa wanaomtetea Kisena, wana maslahi yao na wanaopinga pia wana maslahi yao, hivyo serikali ikae chini kupata ufumbuzi wa tatizo hili.
Mbunge wa Kasulu Mjini, Moses Machali (NCCR-Mageuzi), alisema kama Kisena alinunua UDA kwa bei ya kutupwa, wa kulaumiwa ni serikali na sio mmiliki wake.
Kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani, Freeman Mbowe, alisema kama kuna jambo limeivua nguo serikali, hili la umiliki wa UDA ni aibu ya mwaka.
Mbowe, alisisitiza kuwa jambo hili limeivua nguo serikali kwani kauli za viongozi wake zinagongana na kamati tano za Bunge zilizoshughulika na suala hilo, kila moja inasema lake.
“Mheshimiwa Mwenyekiti, sijawahi kuona serikali imenywea kama leo kwenye hoja hii. Mheshimiwa Mwenyekiti, mwekezaji wa UDA ameingiza magari 300, serikali inamwona, kauli za viongozi wa serikali zinagongana, kamati tano kila moja inasema lake, leo mnakuja kuvuana nguo hadharani, hii ni aibu kwa serikali hii sikivu ya CCM.
“Ushauri wangu, kaeni chini mmalize utata huu badala ya kuvuana nguo bila sababu maana wananchi wa Dar es Salaam wanahitaji usafiri,” alisema Mbowe.
Kuona mzozo unazidi kuwa mkubwa, Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais (Sera, Uratibu na Bunge), William Lukuvi, alisema serikali haijajivua nguo katika suala hilo kwani maelezo yake yako wazi.
Alisema Ripoti ya Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Serikali (CAG), ipo na imesema wazi kwamba kuna utata wa umiliki wa UDA.
“Lakini pia si mnajua suala hili lipo Takukuru na kwa DPP. Pili Mnyika alilitolea mwongozo na jambo hili lipo mbele ya Kamati ya Haki, Kinga na Maadili ya Bunge kwa hatua zaidi,” alisema Lukuvi.
Mbunge wa Kigoma Mjini, Peter Serukamba (CCM), hakuridhika na majibu ya serikali ambaye katika mchango wake aliishangaa kusema haimjui mwekezaji Kisena wakati imetoa msamaha wa magari 300 aliyoyaingiza nchini bure bila kodi.
“Mheshimiwa Spika, naunga mkono hoja ya Kingwangala kuhusu mmiliki wa UDA. Mwekezaji huyo ameingiza magari 300, yakatolewa bure bila kodi, leo serikali hii hii inasema haimjui. Mmeenda mahakamani, ameshinda kesi, mahakama imewaachia huru. Hili suala liangaliwe upya, huyo mwekezaji ni mwenzetu, ngozi nyeusi (Mzawa), tumwache,” alisema Serukamba.
Sakata la UDA lilihitimishwa kwa malumbano makali kati ya Naibu Spika Ndugai na Waziri Mwakyembe.
Ndugai, alipompa nafasi Mwakyembe kujibu hoja za wabunge kuhusu UDA, waziri huyo aling’aka huku akikunja sura kwamba wizara yake haihusiki na UDA.
“Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nieleze masikitiko yangu kwa kuruhusu mjadala wa UDA ambao hauhusiani kabisa na hoja yangu. Mimi sijawahi kuliona faili la UDA likija mezani pangu, unataka nijibu nini hapa? Hatuhusiki ndio maana tangu awali nilisema hili halituhusu.”
Kuona hivyo, Ndugai alisimama kwenye kiti chake na kufoka: “Suala hili linahusu Wizara ya Uchukuzi na mada iliyopo inahusu uchukuzi ndiyo maana leo wamekuja madereva wa malori, kwa hiyo linawahusu. Lakini jambo hili linatuhusu sote, kwa hiyo serikali ikae ije na majibu kumaliza utata huu,” alisema Ndugai na kufunga mjadala wa UDA.
Mjadala nje ya Bunge
Baada ya mjadala wa UDA kumalizwa bungeni kwa kufuata ushauri wa Mbowe aliyeitaka serikali ikae chini kumaliza utata huo, nje ya ukumbi wa Bunge kulikuwa na vituko vyake.
Baadhi ya wabunge na mawaziri walisimama kwenye vikundi kujadili kilichojiri bungeni kuhusu suala la UDA.
Mshangao wa kwanza ulielekezwa kwa Naibu Spika kuruhusu mjadala huo huku akijua fika kwamba Spika Makinda, alishalitolea maamuzi na serikali kupitia kwa AG Werema ilieleza kwamba jambo hili lipo Takukuru.

No comments: