Sunday, 18 May 2014

Kambi ya upinzani ya Mlipua Mama salma Kikwete


 
 Waziri Kivuli wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto, Salum Barwany akiwasilisha Bungeni maoni ya kambi ya upinzani kuhusu bajeti ya Wizara hiyo kwa mwaka wa fedha 2014/15, mjini Dodoma jana


Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni jana imemlipua Mke wa Rais Jakaya Kikwete na Mwenyekiti wa Taasisi ya Wanawake na Maendeleo (Wama), Mama Salma Kikwete kuwa mwaka 2010 aliitumia taasisi hiyo kumpigia kampeni mumewe.

Kutokana na hali hiyo, kambi hiyo imeitaka Serikali kueleza hatua ilizochukua dhidi ya shirika hilo lisilo la kiserikali linaloonekana wazi kukipigia debe Chama Cha Mapinduzi (CCM).
Akizungumza wakati akiwasilisha hotuba ya Kambi ya Upinzani bungeni jana, msemaji wa kambi hiyo wa Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto, Salum Khalfan Barwany alisema Serikali imekuwa ikiyafumbia macho mashirika yasiyo ya kiserikali yanayotumika kisiasa kwa manufaa ya CCM.
“Serikali inayoongozwa na CCM imekuwa ikiyafuta mashirika yasiyo ya kiserikali yasiyofungamana na chama chochote pale ambapo imeona yanafanya harakati za kudai haki kwa niaba ya makundi mbalimbali,” alisema na kuongeza:
“Serikali ilifuta Baraza la Wanawake Tanzania (Bawata) na Shirika la Vijana la National Youth Forum (NYF).”
“Hali hii imeachwa muda mrefu na kuota mizizi na Taifa limeshuhudia uteuzi wa wajumbe 201 wa Bunge Maalumu la Katiba kutoka katika mashirika, taasisi za kidini, asasi za kiraia na taasisi mbalimbali, ambao wapo kwa masilahi ya CCM,” alisema Barwany.
Alisema hali hiyo imesababisha kutengenezwa kwa genge la kutetea misimamo ya CCM kinyume na Rasimu ya Katiba iliyowasilishwa na Tume ya Mabadiliko ya Katiba.
Wabunge wapinga
Mbunge wa Viti Maalumu (CCM), Amina Makilagi alisema: “Mama Salma amekuwa mstari wa mbele kutetea haki za wanawake. Pia kama alimpigia kampeni Rais Kikwete hilo siyo ajabu.” Kwa upande wake Mbunge wa Mbinga Magharibi (CCM), John Komba alisema hakuna ubaya kusisitiza bora kupigiwa kampeni na mke kuliko mchumba.
“Wapo wengine wanatembea katika kampeni na wachumba zao,” alisema Komba huku akitaja jina la Josephine, akimaanisha mke wa Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Dk Wilbroad Slaa.
Akizungumzia bajeti ya wizara hiyo mwaka 2014.15, Barwany alisema ni aibu kwa Serikali kutoa asilimia 25 tu ya bajeti ya maendeleo na asilimia 36 ya bajeti ya matumizi mengineyo kwa wizara hiyo katika mwaka 2013/14.

No comments: