Mkazi wa Kyela mkoani Mbeya, Mboka Mwakikagile (20) akiwa na mtoto wake Godluck Mwangosi katika Hospitali ya Rufaa Meta ya jijini Mbeya baada ya polisi kumkamata mtu anayedaiwa kumwiba mtoto huyo.
Kwa muda mrefu kumekuwapo na taarifa za watoto kupotea katika mazingira tofauti, huku baadhi yao wakipatikana na kuunganishwa tena na wazazi wao, lakini wengine hawajaonekana hadi leo.
Wakati wazazi na walezi wa watoto hao wakiwa
katika kiza kinene wasijue nini cha kufanya, serikali na wadau
wanaoshughulikia masuala ya watoto bado hawajapata jibu la swali; watoto
hao wapo wapi? Badala yake wameweka wazi sababu za watoto kupotea au
kuibwa.
Uchunguzi uliofanywa na blog hii katika mikoa
mbalimbali nchini kubaini sababu za watoto hao kupotea, umebaini kuwa
baadhi ya watoto huondoka nyumbani baada ya kutokea ugomvi kati ya
wazazi au walezi wao.
Sababu nyingine ni kuibuka kwa biashara ya watoto
wanaouzwa kwa watu ambao hawana watoto, nchini na nje ya nchi na imani
za kishirikina zinazochochewa na waganga wa jadi.
Taarifa kutoka polisi zinasema kuwa baadhi ya
watoto walioripotiwa kwenye vituo vya polisi kupotea au kuibwa,
walibainika kuchukuliwa na mmoja wa wazazi wa mtoto kutokana na migogoro
kwenye familia.
Zaidi ya watoto 61 waliripotiwa kuibwa Dar es Salaam katika ya mwaka 2012 na 2013, kati yao wa kiume 28 na wa kike 32.
Taarifa kutoka Polisi Kanda Maalumu ya Dar es
Salaam inaeleza kuwa mwaka 2012 kulikuwa na kesi 29 za wizi wa watoto,
ambapo kati yake watoto wanne wa kiume waliibwa hospitalini na watano wa
kike walichukuliwa wakiwa nyumbani. Watoto saba pekee kati ya wote
walioibwa ndiyo walipatikana.
Mwaka jana kulikuwa na kesi za wizi wa watoto 31,
kati yao wa kiume wawili walichukuliwa na watu wasiofahamika wakiwa
hospitalini na 17 wakiwa nyumbani. Pia watoto wa kike 12 walipotea mwaka
huo. Hadi kufikia Desemba 2013, watoto 21 walikuwa wamepatikana, ambapo
kati yao wa kiume 11 na wa kike 10.
Kamanda wa Polisi wa Kinondoni, Camillius Wambura
anasema watoto wachanga ndio wanaoibwa huku wenye umri mkubwa kidogo
hupotea kutokana na sababu mbalimbali zikiwamo uzembe wa wazazi. Wambura
anasema baadhi ya wazazi waliiba watoto wachanga kwa sababu ya kutokuwa
na uwezo wa kuzaa, tabia iliyokomaa kutokana na wazazi wa aina hiyo
kushindwa kukubali hali waliyonayo.
Akitoa mfano anasema kuwa mama mmoja aliiba mtoto
mwenye umri wa wiki mbili Dar es Salaam, lakini alikamatwa siku chache
baadaye mkoani Rukwa.
“Huyu mama alikuwa akiishi Rukwa, alimrubuni mume
wake kuwa ana ujauzito, hivyo kwa kuwa siku za kujifungua zilikuwa
zimefika alimwambia mumewe anataka kuja Dar es Salaam kujifungua kumbe
alikuwa anakuja kuiba mtoto,” anasema.
Mama huyo alipomwiba mtoto alimpa rafiki yake
atangulie naye Morogoro ambapo alikwenda kumchukua na kwenda naye Rukwa,
hata hivyo mtoto huyo alifariki dunia baadaye. Wambura anazitaja sababu
za watoto kupotea kuwa ni pamoja na watoto kutoroka nyumbani baada ya
kukithiri kwa migogoro kwenye ndoa na wazazi kutokujali watoto wao.
“Ndoa nyingi zipo kwenye migogoro ambayo haiwahusu watoto,
lakini wanaishi kwenye mateso. Usiombe kuishi kwenye nyumba yenye
mateso,” alisema.
Anasema baadhi ya watoto wapo tayari kuishi kwenye
vituo vya kulelea watoto kuliko kukaa na wazazi wao, ambao wanagombana
kila siku.
Anaongeza kuwa baadhi ya wazazi hawawajali watoto
wao, kisha anatoa mfano huu: “Tuliwahi kukaa kituoni na mtoto wa miaka
mitatu kwa wiki mbili, hakuna mtu yeyote anayekuja kumuulizia. Tukaja
kubaini alikuwa anatoka karibu kabisa na kituo, tulipowauliza wazazi
mtoto wenu yuko wapi? Walituambia tulijua akiokotwa ataletwa.”
Kamanda huyo anasema dawa ya watoto kutokupotea ni
wazazi kuwapenda watoto wao, kusimamia michezo yao, kujua wanakula nini
na wanakwenda wapi.
“Tuwafanye watoto wetu watuone sisi ni wazazi bora kuliko wengine,” alisisitiza.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Dodoma, David Misime
anasema jumla ya matukio 24 ya kupotea kwa watoto yaliripotiwa Polisi
katika kipindi cha kuanzia Januari 2013 hadi Aprili 2014.
Misime anasema kuwa watoto wote waliopotea
walipatikana kwa nyakati tofauti ingawa hakueleza walikuwa katika hali
gani na kwamba waliohusika walichukuliwa hatua gani.
“Taarifa hizo zimekuwa zikiletwa na wazazi na
walezi wa watoto hao, na sababu za kupotea kwao tumebaini zinatokana na
watoto hao kwenda mbali na maeneo ya makazi wanayoishi,” anasema.
Alitaja maeneo yenye matukio mengi ya kupotea kwa watoto kuwa ni machungani, shuleni na katika maeneo ya uwindaji.
Taarifa kutoka Tanga zimeeleza kuwa kati ya mwaka
2012 hadi Aprili 2014 jumla ya watoto 63 waliripotiwa kupotea katika
mazingira tofauti.
Watoto waliopotea na wilaya zao kwenye mabano ni
31 (Handeni), wawili (Pangani), Saba (Korogwe), tisa (Tanga Mjini),
wanne (Muheza), watano (Lushoto), wawili (Kilindi) na mmoja (Mkinga).
Alisema watoto wote waliopotea walionekana kwa nyakati tofauti wakiwa hai na kwamba umri wao ulikuwa kati ya miaka mitano na 13.
Pia, baadhi ya watu waliohojiwa walibainisha kuwa kuna watoto
wanaoibwa na kupelekwa kwenda kutumikishwa nje ya nchi katika nchi za
Mashariki ya Kati na Ulaya kutokana na kushamiri kwa biashara ya
usafirishaji watu.
Ahmed Sheikh ambaye awewahi kufanya kazi za ndani
katika nchi za Mashariki ya Kati, anasema baadhi ya watu huwalaghai
wazazi kuwa wanakwenda kuwasomesha watoto wao Uarabuni au Ulaya, lakini
hali huwa kinyume chake kwani wakifika huko hutumikishwa kwa kufanya
kazi zilizo juu ya umri wao ikiwamo kuhusishwa na biashara na ngono.
Ushirikina watajwa
Baadhi ya watu wamewanyooshea kidole waganga wa
jadi kwa madai kuwa wameshiriki kupotea kwa watoto kwa imani za
kishirikina. Wamesema yapo matukio ambayo watu walikamatwa wakijaribu
kuwatorosha watoto na kuwapeleka kusikojulikana.
“Kama utakumbuka yule mtoto aliyekamatwa na kichwa
cha mtoto utaelewa kuwa ushirikina nao unahusika hapa. Sasa kama yule
mtoto asingekamatwa, wazazi wake hadi leo wangekuwa wanasema mtoto wao
alipotea au alichukuliwa na mtu wasiyemjua,” anasema Vero Msemwa mkazi
wa Temeke Mwisho.
Mganga wa jadi, Dk Ameir anayeishi Mkuranga, Pwani
anasema baadhi ya watu huenda kwake wakitaka awasaidie kuwatafuta
watoto wao waliopotea katika mazingira anayoyataja kuwa ya kutatanisha.
Anasema waganga wanatumia nafasi hiyo kuwaibia
wateja wao fedha, kwani siyo rahisi wakasema hawawezi kumpata mtoto
aliyepotea, badala yake hubadilisha sababu kila siku huku wakizidi
kujiingizia fedha.
“Mtu anaweza kukwambia anaweza kumvuta mtu wako
aliyepotea au kuibwa hata kama yupo mbali namna gani, lakini utamngoja
ndugu yako huyo hadi uchoke, na kama ukimsumbua anaweza kukufanyia kitu
chochote kibaya,” anasema.
Waziri aliahidi kuwalinda watoto
Akisoma hotuba ya makadirio ya matumizi ya fedha
kwa mwaka 2013/14, Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto,
Sophia Simba alisema kuwa Serikali imeanzisha timu maalumu za kusimamia
ulinzi wa watoto katika mikoa 24 Tanzania Bara.
Alisema kutokana na kuendelea kwa vitendo vya
ukatili dhidi ya watoto, imeanzisha mikutano ya kuongeza uelewa wa
ukatili dhidi ya watoto katika mikoa ya Mara, Shinyanga na Singida.
“Wizara yangu itaendelea kuwatambua na kuwapongeza
wadau wanaoshiriki kikamilifu na kutoa mchango mkubwa katika
kufanikisha upatikanaji wa haki za mtoto na kuzuia ukatili wa watoto,”
alisema.
Mwanaharakati wa haki za watoto, Usu Mallya anasema watoto wengi
wanaopotea wanatoka katika familia duni, ambazo zinashindwa kumpa mtoto
ulinzi wa kutosha. Usu anasema watoto wanaoishi uswahilini wanapotea
kwa sababu ya kukosa maeneo ya kucheza yaliyotengwa kwa ajili yao.
“Watoto watengewe maeneo maalumu yenye ulinzi,
najua ni suala la kisera na kijamii na kama mambo haya yote
yatajumlishwa kwa pamoja watoto watakuwa salama,” anasema.
Pia, anawanyooshea kidole wanaume wanaowapa mimba
wasichana kisha wanazikana, kuwa wanahitaji kulaumiwa kwa kushiriki
kuwaweka watoto kwenye mazingira hatarishi ya kupotea.
“Wanaume wanasababisha mama anakuwa na watoto
wengi baba tofauti halafu baadaye anashindwa kuwalinda wote, haya
wanaume wabanwe wawalee watoto,” anasema.
No comments:
Post a Comment