Thursday, 22 May 2014

Pinda akiri Kumwingilia waziri wa ujenzi Dr. John Magufuli

Waziri wa Ujenzi, Dk. John Magufuli
Waziri wa Ujenzi Dr.Magufuli
WAZIRI Mkuu Mizengo Pinda, amedaiwa kumhujumu Waziri wa Ujenzi, Dk. John Magufuli kwa kuruhusu malori makubwa kuzidisha uzito na hivyo kukiuka sheria ambayo waziri huyo amekuwa akiisimamia ili kulinda barabara zisiharibike mapema.
Madai hayo mazito dhidi ya Pinda, yalitolewa juzi bungeni na Msemaji mkuu wa Kambi Rasmi ya Upinzani wa Wizara ya Ujenzi, Felix Mkosamali (NCCR-Mageuzi).
Akichangia mjadala wa hotuba ya makadirio ya mapato na matumizi ya bajeti ya Wizara ya Ujenzi kwa mwaka wa fedha 2014/2015, Mkosamali alisema uamuzi wa Pinda kuruhusu malori makubwa ya mizigo yaendelee kuzidisha uzito wa mizigo, umetokana na maslahi binafsi.
Alisema uamuzi huo ni hatari na utaisababishia Serikali hasara ya mamilioni ya fedha za kukarabati barabara zinazoharibika ndani ya muda mfupi kutokana na uzito wa malori.
Huku akishangiliwa na wabunge wa kambi ya upinzani, Mkosamali alisema agizo la Pinda la kuruhusu malori yanayozidisha uzito wa mizigo ni kinyume na kanuni 7 (3) ya Sheria ya usalama barabarani ya 2001.
“Matakwa ya sheria  namba 30 ya 1973 na kanuni namba 30 ya 2001 iliyotangazwa kwenye Gazeti la Serikali, tangazo namba 30 la Februari 9, 2001 iliyoanza kutumika Januari 24 2001, inafafanua uzito wa magari unaotakiwa.
Kipengele cha saba cha sheria hiyo kinaeleza magari yote yenye uzito kuanzia tani 3.5 na kuendelea na aina ya makosa ya uzidishaji uzito, ambapo kifungu cha 2, 3 na 4 vinafafanua matumizi ya uzito uliozidi asilimia tano,”alisema.
Alisema kuwa Dk.Magufuli aliwahi kunukuliwa akisema ataendelea kusimamia sheria ya barabara namba 30 ya mwaka 1973, hadi anaingia kaburini kwa kuhakikisha hakuna magari yanazidisha uzito na kuharibu barabara.
Namnukuu Mh. John Pombe Maghufuli,“Nchini Ujerumani, uzito wa magari yote ni tani 40, Uingereza tani 40, Ufaransa tani 40, Urusi tani 38 lakini Tanzania tani 56, wakati mwingine tunakamata hadi tani 96,”alisema.
Mkosamali alisema kuwa ujasiri wa Dk. Magufuli kusimamia sheria hiyo, ulizimwa na amri ya Waziri Mkuu aliyetengua agizo lake na kuamua kuruhusu magari yenye uzito uliopitiliza kuendelea kuharibu barabara.
Alisema ujenzi wa barabara unatumia gharama kubwa na hata ukarabati wake umekuwa ukitengewa mabilioni ya fedha za walipakodi kutokana na uharibifu unaofanywa.
Alitolea mfano katika bajeti ya 2013/14, akisema serikali ilitenga sh. bilioni 314.535 kwa ajili ya mpango wa matengenezo ya barabara kuu na barabara za mikoa.
“Kiasi hicho cha fedha ambacho ni zaidi ya robo ya bajeti nzima ya wizara hiyo kwa mwaka, kinatosheleza kujenga barabara mpya ya lami yenye urefu wa kilometa zipatazo 315, kwa makadirio ya kilometa moja kugharimu sh. bilioni moja.
Katika mwaka huu wa fedha, bajeti nzima ya Wizara ya Ujenzi ni sh. trilioni 1.226.
“Kambi rasmi ya upinzani inapenda kuelewa hivi katika kuingilia tatizo hili la amri iliyotolewa na waziri mwenye dhamana ya barabara kulikuwa na mashauriano au ilikuwa ni wakubwa kuvuana ngua hadharani?
“Katika utendaji wa namna hii, Je, watanzania watarajie tija kutoka kwa serikali yao? Baba wa taifa aliwahi kusema serikali makini ni yenye kuwa na kauli moja na uwajibikaji wa pamoja (collective responsibility). Kwa serikali hii, wananchi watarajie nini? alihoji.
Kutokana na hali hiyo, Mkosamali alisema kambi rasmi ya upinzani, inamtaka Waziri Mkuu alithibitishie Bunge kwamba yeye na marafiki zake na viongozi wa CCM wanamiliki malori, pia wana hisa katika makampuni mbalimbali, ndio maana imekuwa rahisi kwake  kuruhusu uzidishaji wa mizigo na kuunga mkono uharibifu wa barabara  zilizojengwa kwa jasho la walalahoi.
Tuhuma kama hizo pia kwa Waziri Mkuu, zilitolewa na mbunge wa Kasulu, Moses Machali (NCCR-Mageuzi) wakati akichangia bajeti ya waziri Magufuli.
Alisema uamuzi uliofanywa na Pinda unaonesha kuwa ana maslahi kwenye biashara ya malori.
“Tunataka majibu ya serikali kuhusu hili maana uamuzi uliofanywa na Waziri Mkuu, kwa mtu mwenye akili timamu, hawezi kutoa agizo la kuharibu barabara zetu,”alisema.
Akizungumzia vifaa vya ufuatiliaji utendaji katika vituo vya mizani (CCTV), Mkosamali alisema wanataka majibu kutoka kwa serikali kuhusu ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu (CAG) wa Serikali kuhusu ukosefu wa CCTV, katika vituo vya mizani.
“Ukaguzi ulibaini kuwa CCTV kamera zilikuwa bado hazijawekwa katika baadhi ya vituo kama Namanga na Makuyuni (Arusha), Mikese, Kihonda na Mikumi (Morogoro), Uyole na Mpemba (Mbeya), Makambako (Iringa).
Mkosamali aliitaka serikali kuhakikisha inaweka vifaa hivyo katika mizani yote nchini ili kuboresha uwazi na uwajibikaji katika utendaji.

No comments: