Dhahabu hii inapatikana mtoni tu, watu wanakusanya michanga na kupata dhahabu, hakuna mtu ambaye anachimba,” alisema Sandea. |
Maelfu ya watu wamemiminika tena katika eneo la Samunge, Wilaya ya Ngorongoro Mkoa wa Arusha, safari hii siyo kunywa Kikombe cha Babu Mchungaji Ambilikile Mwasapile, bali kupata dhahabu inayodaiwa kugundulika katika eneo hilo.
Habari kutoka katika eneo hilo zinasema kuwa watu
wanazidi kumiminika katika kujipatia madini hayo yaliyobainika katika
mashamba ya watu na maeneo ya kingo za Mto katika Kijiji cha Mgongo
kilichopo jirani na Kwa Babu.
Diwani wa Samunge, Jackson Sandea alisema maelfu
ya watu kutoka maeneo mbalimbali nchini wamefurika katika kijiji ambacho
kuna mto na madini ya dhahabu yanapatikana hapo.
“Hadi sasa kuna watu zaidi ya 4,000 na bado
wanaongezeka, hii inaweza kuwa ni zaidi ya kipindi kile cha Babu wa
Kikombe. Dhahabu hii inapatikana mtoni tu, watu wanakusanya michanga na
kupata dhahabu, hakuna mtu ambaye anachimba,” alisema Sandea.
Alisema tofauti na maeneo mengine, dhahabu ya
Samunge inaonekana ni ya Watanzania wote kwani ipo eneo la mto ambao
unamilikiwa na Serikali na ndiyo sababu watu wanaingia kwa wingi.
“Kuna wengine wanapata hata mashambani lakini mtoni ndipo inapatikana kwa wingi zaidi,” alisema.
Ulinzi waimarishwa
Diwani huyo alisema ulinzi umeanza kuimarishwa
katika eneo hilo akisema hali ikiachwa kama ilivyo, kunaweza kutokea
vurugu kubwa na hata mauaji.
“Sisi kama viongozi, tumeweka utaratibu mzuri wa
kuchimba madini kiusalama na hata wale ambao wameanza kuuza mashamba
yao, tunawawekea utaratibu mzuri,” alisema.
Maofisa madini kutua Samunge
Kamishna wa Madini Kanda ya Kaskazini, Alex
Magayane alisema jana kwamba baada ya kupokea taarifa za kugundulika kwa
dhahabu katika eneo la Samunge, maofisa wake wanajiandaa kwenda
kijijini hapo.
Alisema taarifa za kitaalamu kuhusu akiba ya
madini hayo iliyopo Samunge itatolewa baada ya maofisa hao kufika katika
eneo hilo na kufanya utafiti.
Ahadi ya Babu
Kugundulika dhahabu katika eneo hilo kunahusishwa
na ahadi ya Mchungaji Mwasapila kuwa mamilioni ya watu watafika tena
Samunge baada ya kupungua ikilinganishwa na miezi ya mwanzo baada ya
kuanza kutoa tiba ya kikombe cha dawa iliyodaiwa kutibu magonjwa sugu.
Tiba yake hiyo ambayo ilizua utata kitaalamu na
ikielezwa kuwa waliotibiwa waliugua tena na wengine kupoteza maisha,
aliwahi kunukuliwa na vyombo vya habari akisema watu kutoka mataifa yote
watakwenda tena Samunge siyo kupata kikombe pekee, bali huduma
nyingine.
Licha ya wengi kuitilia shaka kauli yake hiyo,
aliendelea kuisisitiza na akikata miti na kujenga kituo kikubwa cha
kutolea huduma ya kikombe.
No comments:
Post a Comment