Saturday 17 May 2014

Marekani kuizuia Iran kutengeneza silaha za nyuklia

Waziri wa mambo ya ndani wa Marekani Chuck Hagel amewaahidi viongozi wa Israel kwamba Marekani itafanya kile inacholazimika kufanya kuzuia Iran kuwa taifa lenye kumiliki silaha za nyuklia
Waziri huyo wa ulinzi wa Marekani Chuck Hagel ametowa tamko hadharani katika taarifa wakati wa mazungumzo yake na Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu mjini Jerusalem. Hagel amekariri akisema " nataka kuwahakikishia juu ya kujitolea kwa Marekani kuona kwamba Iran haimiliki silaha za nyuklia na kwamba Marekani itafanya kile wanachopaswa kufanya kutimiza ahadi hiyo."
Wote wawili wamezungumzia juu ya mpango wa tata wa nyukilia wa Iran ambao ulikuwa mada ya mazungumzo wiki hii mjini Vienna kati ya mataifa makubwa ya magharibi na Iran. Netanyahu amesema katika taarifa akiwa amesimama pembezoni mwa Hagel kwamba wamekuwa wakisema kwa muda mrefu kuwa Iran inajaribu kuifumba macho jumuiya ya kimataifa kwa kuibabaisha.

Ameitaja repoti ya Umoja wa Mataifa kwa kile alichokiita juhudi zinazoendelea za Iran kuidanganya jumuiya ya kimataifa kuendelea kurutubisha kwa kiwango kikubwa madini ya urani kufikia uwezo wa kutengeneza silaha za nyuklia na kuendelea kukiuka ahadi zake za Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa lenye kuipiga marufuku kuendeleza sehemu fuklani za mpango wake huo wa nyuklia.
Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu
Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu
Amesema wanaendelea kufanya hivyo na anafikiri jambo hilo linahitaji kuwa na sera kwa upande wa mataifa makubwa duniani. Kiongozi huyo wa Israel amesema lazima wasikubali kuwaachia maayatollah washinde kwa hilo, lazima wasiliwachie taifa hilo kubwa kabisa la kigaidi katika enzi hii Iran kujijengea uwezo wa kutengeneza silaha za nyuklia.
Waziri wa mambo ya ulinzi wa Marekani alikuwa akikamilisha ziara yake ya siku nne Mashariki ya Kati ambayo ilianza Jumanne wiki hii mjine Jeddah Saudi Arabia ambapo alikutana na mawaziri wa ulinzi kutoka mataifa ya Ghuba ya Uajemi yenye uhusiano wa masuala ya usalama wa muda mrefu na Marekani.
Ziara ya Hagel inafanyika sambamba na mazungumzo ya kimataifa na Iran mjini Vienna Austria yenye lengo la kurasimu makubaliano ya kuuwekea vikomo mpango huo wa nyuklia wa Iran ambalo ni suala linalopewa kipau mbele na mataifa ya Kiarabu yalioko Ghuba halikadhalika na Israel.
Suala la kuboresha uhusiano na Iran limekuwa kipau mbele katika sera ya kigeni ya Rais Barack Obama wa Marekani na mazungumzo ya Vienna yameleta matumaini ya maana katika suala hilo la nyuklia. Akiwa nchini Saudi Arabia Hagel amesema kwamba katika mazingira yoyote yale Marekani haitoyatolea muhanga maslahi ya washirika wake ili kwamba ifikie makubaliano ya nyuklia na Iran.

No comments: