Akiwasilisha maoni ya Kambi Rasmi ya Upinzani
Bungeni kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Makamu wa
Rais (Muungano), msemaji wake, Tundu Lissu aliitaka Serikali kueleza
waasisi hao walifanya makosa gani.
Aliwataja waasisi hao kuwa ni Abdallah Kassim
Hanga aliyekuwa Waziri Mkuu, Abdulaziz Twala aliyekuwa Waziri wa Fedha
na Saleh Akida aliyekuwa Mjumbe wa Baraza la Mapinduzi na viongozi
waandamizi wa Serikali ya Mapinduzi, Othman Shariff, Mdungi Ussi na Jaha
Ubwa ambao alisema waliuawa na kuzikwa handaki moja eneo la Kama,
Zanzibar.
Lissu alisema hayo huku akinukuu kitabu cha
‘Kwaheri Ukoloni, Kwaheri Uhuru’ kilichoandikwa na Harith Ghassany
alichosema kilionyesha jinsi viongozi hao walivyouawa na kuzikwa katika
kaburi moja.
“Sisi wa kizazi cha Muungano tunataka kujua ukweli
juu ya makosa waliyoyafanya hawa waasisi wa Muungano hadi wakauawa na
kuzikwa katika kaburi au handaki moja,” alisema Lissu huku wabunge
wakiwa kimya kumsikiliza.
Mgawo wa Zanzibar
Lissu pia aliibua mambo mazito kuhusu mgawanyo wa
fedha za misaada na mikopo ya kibajeti kati ya Serikali ya Muungano na
Serikali ya Mapinduzi Zanzibar.
Alisema Muungano ni kielelezo cha unyonyaji na ukandamizaji ambao nchi kubwa imeifanyia nchi ndogo ya Zanzibar kwa miaka mingi.
Alikwenda mbali na kuitaka Serikali ya Mapinduzi
Zanzibar au Wazanzibari kwa umoja wao, kufungua kesi Mahakama za
kimataifa kudai fedha zote ambazo nchi yao imeibiwa kwa kivuli cha
Muungano.
Mbunge huyo ambaye pia ni Mwanasheria Mkuu wa
Chadema, alisema hadi Machi mwaka huu, Zanzibar ilikuwa imepata gawio la
Sh27.1 bilioni badala ya Sh32.6 bilioni zilizoidhinishwa na Bunge, sawa
na asilimia 83.
Hata hivyo, alisema hilo linaweza lisiwe tatizo,
kwani kwa mwelekeo wa takwimu hizo, hadi kufikia mwisho wa mwaka huu wa
fedha, gawio lililoidhinishwa linaweza kuwa limelipwa lote.
Haya hivyo, alisema tatizo kubwa na la msingi ni
kwamba, gawio lililoidhinishwa na Bunge si halali kwa Zanzibar, kwa
mujibu wa hotuba ya Waziri wa Fedha, Saada Mkuya ya Aprili 30, mwaka huu
Lissu alimnukuu Mkuya akisema mapato halisi ya Serikali ya
Muungano yanayotokana na misaada na mikopo nafuu ya nje kwa mwaka
2013/2014 yalikuwa Sh1.163 trilioni.
“Kama Zanzibar ingepatiwa asilimia 4.5 ya mapato
hayo kama inavyotakiwa kwa mujibu wa sheria, kwa mwaka jana pekee, gawio
halali la Zanzibar lingekuwa Sh52.335 bilioni,” alisema.
“Badala ya kupatiwa Sh52.335 bilioni ambazo ni
fedha zake halali, Zanzibar iliidhinishiwa Sh32.62 bilioni au asilimia
52 ya fedha zake halali. Hii ni sawa na asilimia 2.8 ya fedha zote za
misaada badala ya asilimia 4.5.”
Alisema kwa ushahidi huo wa nyaraka za Serikali,
kwa mwaka jana pekee Zanzibar iliibiwa Sh25.145 bilioni sawa na asilimia
48 ya fedha zake halali za gawio la misaada na mikopo ya kibajeti.
Kutokana na hali hiyo, kambi hiyo imeitaka
Serikali kueleza ni kwa nini fedha halali za Zanzibar kutokana na
misaada na mikopo ya kibajeti hazijalipwa kwa mwaka jana wa fedha.
Pia kambi hiyo imeitaka Serikali kupeleka mbele ya
Bunge, takwimu za fedha zote za misaada ilizopokea na mikopo ya
kibajeti kwa kipindi cha miaka 10 iliyopita.
Katika takwimu hizo, kambi hiyo imeitaka Serikali
kueleza katika fedha hizo, ni kiasi gani kililipwa kama kwa Zanzibar
kama gawio lake katika kipindi hicho kwa fedha za misaada na mikopo ya
bajeti.
Kuhusu misaada na mikopo isiyokuwa ya kibajeti,
Lissu alisema: “Ukweli ni kwamba hali ni mbaya zaidi kuhusu fedha za
misaada na mikopo isiyokuwa ya kibajeti. Hapa pia takwimu za Serikali
hii ya CCM zinatisha na kusikitisha.”
Alitolea mfano kuwa Mwaka wa Fedha 2013/2014 fedha
za nje kwa ajili ya miradi ya maendeleo zikijumuisha misaada na mikopo
zilikuwa Sh2.692 trilioni.
“Fedha hizi zote zilitumika kwa ajili ya miradi ya
maendeleo ya Tanganyika. Zanzibar haikupata kitu chochote,” alisema
Lissu ambaye pia ni Mbunge wa Singida Mashariki.
Lissu alisema kutokana na Muungano, Zanzibar
imenyang’anywa mamlaka ya kuomba mikopo au misaada kutoka nje bila
kibali cha Wizara ya Fedha ya Muungano.
“Sisi tuliozaliwa ndani ya Muungano tunataka kujua
unyonyaji na wizi huu wa fedha za Wazanzibari utakomeshwa lini?”
alihoji Lissu.
Waziri afafanua
Wakati Lissu akisema hayo, Waziri wa Nchi, Ofisi
ya Makamu wa Rais (Muungano), Samia Suluhu Hassan alisema kati ya Julai
Mosi, 2012 na Machi mwaka huu Zanzibar imepata gawio la Sh36.75 bilioni
kutokana na Kodi ya Mishahara ya Wafanyakazi (Paye).
Waziri Hassan alisema hatua hiyo ni baada ya
mawaziri wa pande mbili kukaa na kukubaliana kuwa SMZ inastahili kwa
vile kodi ya mapato inayotokana na mishahara ya wafanyakazi ni suala
linalohusu mapato ya Muungano.
Hata hivyo, alisema marekebisho ya Sheria ya Kodi
ya Mapato kuhusu kodi ya mishahara yanahitajika ili kuweka utaratibu wa
wazi zaidi.
Pia alisema kuanzia Julai, 2013 hadi Machi mwaka
huu, SMZ imepokea kodi ya mshahara ya Sh15.75 bilioni na fedha za Mfuko
wa Maendeleo ya Jimbo Sh1.24 bilioni.
Kuhusu gawio la mapato ya misaada ya kibajeti,
Waziri Hassan alisema SMZ imepata Sh27.19 bilioni kati ya Sh32.63
bilioni zilizoidhinishwa na Bunge kwa Mwaka wa Fedha 2013/14.
Alisema Serikali pia iliichangia SMZ Sh600 milioni kwa ajili ya kufanikisha maadhimisho ya miaka 50 ya Mapinduzi ya Zanzibar.
Waasisi na Picha
Lissu alisema kuna jambo linalofikirisha sana
kuhusu picha za miaka 50 ya Muungano, kwa kuwa baadhi ya watu
wanaoonekana katika picha hizo wamefutwa katika historia wanayofundishwa
watoto shuleni.
Alitolea mfano picha ya Mwalimu Julius Nyerere na
Sheikh Abeid Karume wakisaini hati za makubaliano ya Muungano wakiwapo
viongozi waliokuwa wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar.
“Kwa upande wa Tanganyika alikuwapo Oscar Kambona,
Bhoke Munanka na Job Lusinde, wakati kwa Zanzibar wanaoonekana ni
Abdallah Kassim Hanga, Abdulaziz Twala na Ali Mwinyigogo,” alisema.
Lissu alisema Ghassay katika kitabu chake
ameonyesha jinsi waasisi hao walivyotoa mchango mkubwa katika
kufanikisha Mapinduzi ya Zanzibar ya Januari 12, 1964.
“Baadaye viongozi hao walifanikisha Muungano wa Zanzibar na
Tanganyika Aprili 26 ya mwaka huo,” alisema na kuongeza kuwa hilo
lilithibitishwa pia na aliyewahi kuwa Rais wa Zanzibar, Aboud Jumbe.
Lissu alisema katika kitabu chake, Jumbe ameeleza
kuwa Kambona, Munanka na Lusinde ndio waliompelekea Karume nakala za
hati ya makubaliano na kusainiwa Aprili 22, 1964.
No comments:
Post a Comment