Sunday, 11 May 2014

Wanafunzi 212 wafukuzwa chuoni (CCP) moshi kwa kugushi Vyeti

Jeshi la Polisi limewafukuza chuo wanafunzi wa mafunzo ya uaskari 212 wa Chuo Cha Taaluma Moshi baada ya wanafunzi hao kubainika kughushi vyeti vya elimu ya sekondari.
Kamishna wa Utawala na Utumishi kutoka jeshi la polisi, Thobias Andengenye ametoa taarifa hizo jana wakati wa kikao cha  waandishi wa habari na maofisa wa polisi kilichofanyika chuoni hapo kilichopo Moshi mkoani Kilimanjaro.
CP Andengenye alisema uamuzi wa kuwafukuza chuo wanafunzi hao umekuja baada ya jeshi hilo kwa kushirikiana na baraza la mitihani la taifa kubaini vyeti vya wanafunzi 212 kati ya 3,390 kuwa vimeghushiwa.
Alisema jumla ya wanafunzi 3,415 waliripoti chuoni na kati yao 25 walishindwa kuendelea na masomo kutokana na sababu mbalimbali ikiwamo ya utovu wa nidhamu na matatizo ya kiafya.
“Baada ya hawa 25 kuondoka tulipeleka majina kwenye baraza ili kuhakiki vyeti na baraza la mitihani limetuletea majibu wiki iliyopita na kubaini vyeti vya wanafunzi wa uaskari 212 ni vya kughushi,”alisema Andengenye.
Alisema jeshi hilo linaendelea na hatua za upelelezi kwa kushirikiana na taasisi nyingine ili kujua wanaohusika kuwaghushia vyeti hivyo.
 “Itambulike kuwa kitendo cha kughushi ni kosa la jinai na pindi unapobainika polisi haitasita kuwachukulia hatua za kisheria,” alisema Andengenye.
Hata hivyo amewataka wananchi kuacha tabia za kughushi vyeti na badala yake wafuate sheria na taratibu zilizopo kwa ustawi wa taifa.
Wanafunzi hao walianza mafunzo ya uaskari Disemba mwaka jana ambapo walitarajia kumaliza mafunzo ya awali Septemba mwaka huu.
Tatizo la kughushi vyeti nchini limekuwa sugu hususani katika idara mbalimbali zikiwamo polisi, uuguzi ,ualimu na nyinginezo

No comments: