Sunday 18 May 2014

Njaa yatufanya tule nyama ya Paka

Paka akiwa amechinjwa 

Siyo rahisi kwa mtu ambaye anapata chakula kutwa mara tatu, kuamini kuwa kuna binadamu ambao wanaweza kuishi hata siku tatu bila kupata hata mlo mmoja.
Hata hivyo ni ukweli usiopingika kuwa wakati unakula na kumwaga chakula kwenye mifuko ya takataka, wapo ambao hutamani kukimbilia mifuko hiyo na kujitafutia chochote kwa ajili ya matumbo yao.
Wapo ambao hudiriki kula hata vitu ambavyo havistahili kuliwa na binadamu, lakini hawana jinsi wanafanya hivyo kutuliza matumbo yao yanayosumbuliwa na njaa.
Njaa imekuwa ni tatizo sugu linaloonekana kujitokeza katika mataifa mbalimbali yanayoendelea, huku bara la Afrika likiwa limeathirika kwa sehemu kubwa kutokana na janga hili.
Licha ya kuwa na eneo kubwa la ardhi yenye rutuba na mvua za kutosha, ukanda wa Afrika Mashariki nao umekuwa ukikumbwa na baa hili katika baadhi ya maeneo.
Hilo linatokana na maeneo hayo kuwa na ukame na kukosa mvua, hali inayopelekea kilimo kutofanyika kama inavyostahili hivyo chakula kuwa miongoni mwa vitu hadimu kupatika kwa wakazi wa eneo husika.
Kijiji cha Kakoghit kilichopo kwenye Kata ya Lokis nchini Kenya, kimekuwa miongoni mwa maeneo ambayo yapo katika hali mbaya zaidi kutokana na tatizo la njaa.
Tukio la hivi karibu la familia moja kuchinja paka na kumla kama kitoweo baada ya kuzidiwa na njaa waliyokaa nayo kwa siku kadhaa kutokana na kukosa chakula, limedhihirisha namna gani njaa ilivyokuwa tishio.
Familia hiyo yenye jumla ya watu watatu ikiwajumuisha Jepoterit Yaranyang (80), Jepteker Ng’uriawing (35) na mtoto wake wa miaka miwili ilifikia uamuzi wa kumuiba paka wa jirani na kumchinja ili kutuliza njaa iliyokuwa ikiwasumbua kwa muda mrefu.
Katika mahojiano yake na gazeti la moja nchini Kenya, Ng’uriawing anasema kuwa baada ya kukaa siku nyingi bila kula huku mama yake akiwa hoi kitandani akidhoofika kutokana na njaa, akafikiria kumkamata paka wa jirani ili wamfanye kitoweo. Wazo hilo likatawala kichwani mwake na dakika chache alipokatiza paka huyo alimpiga kichwani kabla ya kumchinja na kuchoma nyama yake kuitafuna ili kupoza njaa iliyokuwa ikiwakabili.
“Baada ya kuona hali inazidi kuwa mbaya nikaona tutaangamia kwa kuwa mama yangu tayari alishaanza kudhoofika kutoka na njaa, nikaamua kumgonga paka kisha nikamchuna ngozi na kuchoma nyama yake ambayo ilikuwa na damu nyingi”anasema Ng’uriawing na kuongeza:
“Ukweli ni kwamba hali ilikuwa mbaya sana hata kama paka asingejitokeza ingewezekana ningemchinja mtoto wangu tuile nyama yake maana nisingeweza kuvumilia hali ya njaa kali kiasi kile”.

Mmiliki wa paka huyo, Chepochegheh Todong’ira alimtafuta paka wake mpaka kufikia hatua ya kukata tamaa lakini alipozunguka kwenye nyumba ya jirani yake alikuta mabaki ya mifupa, ngozi na mkia.
Anasema alipojaribu kuhoji familia hiyo walimweleza wazi kuwa walimchinja paka huyo na kumfanya kitoweo kutokana na kukabiliwa na njaa kali.
Baada ya kupewa majibu hayo yaliyomtia simanzi Todong’ira alitoa taarifa kwa chifu wa eneo hilo na kumfahamisha namna ambavyo hali ilivyo tete mpaka kufikia hatua ya binadamu kuchinja paka.
“Nilipomuhoji Jepteker hakukanusha alikubali kuwa wamemchinja paka wangu kutokana na njaa, kiukweli hali ni mbaya sana huku kwetu na Serikali imetusahau kabisa inapaswa kuleta chakula katika eneo hili,” anaeleza.
Wakati mahojiano yakiendelea kikongwe Yaranyang alikuwa hoi kitandani huku akionekana muda wowote anaweza kukata roho kutokana na kukosa chakula.
Naibu Chifu wa Kata ya Lokis, Johnston Long’iro alifika katika nyumba hiyo na kukuta mabaki ya paka huyo na kujihakikishia kwa kiasi gani hali ni mbaya.
“Hali ya njaa ni mbaya sana hapa kwetu watu wengi wamefikia hatua ya kuhamia katika maeneo jirani kama Elgeyo-Marakwet na Pokot Magharibi ambako wamekwenda kutafuta chakula na lishe na maji kwa mifugo yao,” anasema Long’iro.
Anaongeza kuwa njaa pia imeathiri kwa kiasi kikubwa sekta ya elimu katika eneo hilo, huku shule za msingi kadhaa zikiwamo Korelech, Krezeek na Ng’aina zikiwa hazijafunguliwa kutokana na wanafunzi na wazazi wao kuhamahama wakitafuta chakula.
Anafafanua kuwa mara ya mwisho chakula cha msaada kupelekwa katika eneo hilo ni mwaka uliopita na shughuli hiyo ilioongozwa na Shirika la Chakula Duniani (WFP).
Kisa hiki kinaweza kuwa mfano mmojawapo wa maisha ya baadhi ya maeneo barani Afrika, ambayo yameathirika kwa kiasi kikubwa kutokana na njaa.
Wapo ambao hulazimika kula matunda na mizizi bila kufahamu huenda ikawa na sumu hatua inayowafanya wengine kupoteza maisha.

No comments: