Wabunge wa vyama vyote vya kisiasa nchini Ujerumani wameulaani ugaidi
nchini Nigeria. Wakati nchini Nigeria kwenyewe maandamano makubwa
yamefanyika kuonyesha mshikamano na wasichana waliotekwa nyara
Mwenyekiti wa chama cha kijani Cem Özdemir amesema lazima kundi la
itikadi kali ya kiislamu ,Boko Haram likomeshwe.Ameeleza kwamba kundi
hilo ni tishio,siyo tu nchini Nigeria bali pia kwa nchi jirani.Akihutubia bungeni,Mwenyekiti huyo Ozdmer amesema itikadi ya kundi la Boko Haram inaipotosha dini ya kiislamu inayofuata imani ya utukufu wa Mwenyezi Mungu .Mwenyekiti huyo amesema hakuna chochote katika dini ya kiislamu kinachoweza kuhalalisha kutekwa nyara mamia ya wasichana wa shule.
Mwenyekiti Özdemir amesema Boko Haram siyo suala la ndani ya Nigeria pekee. Ameeleza kwamba wote wanao wajibu wa kufanya kila linalopasa ili wasichana waliotekwa nyara wakombolewe . Amesema lazima kundi la Boko Haram likomeshwe.
Wanawake wakombolewe
Bwana Özdemir ameeleza kwamba ikiwa idadi kubwa ya nchi za kiislamu zinataka kuchukua nafasi zinazostahiki katika ustaarabu wa binadamu, zitaweza kulifikia lengo hilo ikiwa wanawake watakombolewa na ikiwa watachukua asilimia 50 ya mamlaka katika nchi hizo za kiislamu
Naye mbunge wa chama cha Social Demokratik Edelgard Bulmahn amesema yeyote anaendesha harakati, kama kundi la Boko Haram basi yeye anajitenga na maadili yote ya dini na tamaduni za dunia. Mbunge huyo amesisitza kwamba jambo la kipaumbele sasa ni kuwakomboa wasichana waliotekwa nyara.
Wabunge wa vyama vyote vya Ujerumani ukiowaondoa wale wa chama cha mrengo wa shoto wameuunga mkono mpango wa kupambana na kundi la Boko Haram uliopitishwa na viongozi wa nchi za Afrika waliokutana mjini Paris mwishoni mwa wiki iliyopita. Wajumbe wa Umoja wa Ulaya,Uingereza na Marekani pia walishiriki kwenye mkutano wa mjini Paris.
Mjadala wapendekezwa na vyama vinavyooingoza serikali
Mjadala juu ya hali ya sasa nchini Nigeria katika Bunge la Ujerumani ulipendekezwa na vyama vinavyoiongoza serikali ya mseto ,Christian Demokratik Union na Social Demokratik .Kiongozi wa wabunge wa vyama ndugu vya CDU na CSU bwana Volker Kauder amesema pana ushahidi wa kutosha unaothibitisha kwamba kundi la Boko Haram linadhamiria kuwatimua wakristo kutoka Nigeria.
Bwana Kauder amesema kinachotokea nchini Nigeria si mgogoro wa kikabila bali ni suala linalohusu uhuru wa kuabudu.Amesema ukweli wenyewe ni kwamba, watu ambao hasa wanaandamwa ni Wakristo na hasa pale ambapo Waislamu ni wengi na wenye mamlaka.
Hata hivyo kauli ya bwana Kauder imepingwa na mbunge wa chama cha Social Demokratik Frank Schwabe. Mbunge huyo ameeleza kwamba viongozi wa dini ya kiislamu na kanisa Katoliki nchini Nigeria wamesisitiza kwamba kiini cha tatizo nchini Nigeria si mgogoro wa kidiini, kwani mbunge huyo bwana Frank Schwabe amesema wanaoathirika ni Waislamu na Waksrito kadhalika. Amewataka wabunge wenzake waepuke kuyaangalia matatizo yanayoikabili Nigeria sasa kama mgogoro wa kidini.
Ustawi wa Boko Haram
Hata hivyo wabunge wote wa Ujerumani wamekubaliana kwamba pana sababu mbalimbali zinazochangia katika kulishtawisha kundi la Boko Haram. Watu wengi nchini Nigeria hawanufaiki na utajiri mkubwa wa nchi hiyo na wala hawanufaiki na ustawi wake wa uchumi. Umasikini,mabadiliko ya tabia nchi na ufisadi ni mambo yanayowafanya vijana wajiunge na kundi la Boko Haram. Mbunge wa chama cha Social Demokratik bwana Schwabe ameuunga mkono mkakati wa kijamii wa serikali ya Nigeria wenye lengo la kuzitathmini sababu za kiuchumi na kijamii zinazochangia katika uwepo wa kundi la itikadi kali ya kiislamu la Boko Haram.
Mbunge huyo amesema Nigeria inapasa kupiga hatua katika juhudi za kuwashirikisha watu wake kijamii.Haki za binadamu zinapaswa kutekelezwa na adhabu ya kifo iondolewe .Harakati za kupambana na ugaidi lazima zifuate misingi ya kisheria. Amesema ikiwa serikali ya Nigeria itapitia katika njia hiyo,basi Ujerumani itaiunga mkono.
Wakati huo huo Waziri wa Ujerumani anaeshughulikia ushirikiano wa maendeleo Gerd Müller amefahamisha kwamba atafanya ziara nchini Nigeria hivi karibuni tu. Waziri Müller atafanya mazungumzo juu ya ushirikiano baina ya nchi yake na Nigeria. Ujerumani inadhamiria kuyaimarisha mawasiliano yake na Nigeria
No comments:
Post a Comment