Thursday, 22 May 2014

Serikali kuwekeza elimu ya juu

Waziri wa Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia Profesa Makame Mbarawa (katikati) na Naibu Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Jenista Muhagama, wakimsilikiza Afisa Uhusiano wa Chuo cha Kikristo cha Uganda, Prim Tumuramye baada ya ufunguzi wa Maonyesho ya Tisa ya Elimu ya Juu, Sayansi na Teknolojia yaliyoanza jana kwenye ukumbi wa Diamond Jubilee jijini Dar es Salaam.
 
Serikali  imesema itaendelea kuwekeza katika Elimu ya Juu, Sayansi na Teknolojia ikishirikiana na sekta binafsi kwa manufaa ya watu wote, na katika kutimiza malengo ya milenia  ya Elimu kwa wote na mpango wa matokeo makubwa sasa.

Kauli hiyo ilitolewa na Waziri wa Mawasiliano Sayansi na Teknolojia, Profesa Makame Mbarawa,   wakati wa ufunguzi wa maonyesho  ya tisa ya vyuo vikuu yaliyoandaliwa na Tume ya vyuo Vikuu (TCU) jijini Dar es Salaam.

Profesa Mbarawa alisema kuwa ili kufikia mpango wa maendeleo (2011/12 hadi 2015/16) ni lazima kuwapo rasilimali watu yenye nguvu na iliyo na ujuzi na kuwa kipaumbele chake kuwa ni elimu na ujuzi.

Akitaja upungufu katika sekta hiyo na kusema kwa sasa wanahitajika walimu waajiriwa waliokidhi vigezo  900,000 na kuwa waliopo kwa sasa ni 238,000 wakati katika sekta ya Afya 110,000 huku mahitaji halisi ni 476,000.

Waziri Mbarawa alisema ongezeko la wana taaluma hao linatokana na matokeo  ya Sensa ya Taifa ya watu na makazi ya mwaka 2012 inayoonyesha kuwa idadi ya watu imeongezeka kutoka watu milioni 12 mwaka 1967 hadi watu milioni 44.9 mwaka 2012.

Naibu waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Jenista Mhagama, alisema kuwa maonyesho hayo ya siku tatu  yana malengo ya kukuza uelewa kwa jamii kuhusu elimu ya juu.

Aliongeza kuwa maonyesho hayo yanatoa fursa kwa taasisi hizo za elimu  kuonyesha shughuli zao sambamba na kuwapa fursa wadau kutumia nafasi hiyo kuona namna wanavyoweza kupata huduma kutoka kwao.

No comments: