Sunday, 11 May 2014

Hans Van Der Plujim auponda mfumo wa soka la Tanzania

Hans Van Der Plujim
Aliyekuwa kocha wa Yanga, Hans Van Der Plujim ameponda miundombinu ya viwanja nchini na kudai inachangia soka la Tanzania kutoendelea.
Akizungumza na waandishi wetu mfupi baada ya kutangaza kubwaga manyanga ndani ya klabu hiyo juzi,  Plujim alisema Watanzania kama wanataka kukuza soka lao ni lazima kwanza wawekeze katika miundombinu ya viwanja na timu za vijana.
“Uwanja wa mazoezi niliouona bora kwa kipindi chote nilichokaa ni ule wa Bunju Veteran, lakini viwanja vingine vyote ni hovyo, inashangaza viwanja vya mikoani ni vibovu, ona kama ule wa Tanga (Mkwakwani) na Morogoro (Jamhuri), halafu unatumika kucheza mechi ya Ligi Kuu.
“Kwanza kama Watanzania wanataka maendeleo kama walivyo wenzao wa Ghana na Nigeria ni lazima wawekeze kwenye viwanja, ni lazima wawekeze kwenye soka la vijana, hapo wanaweza kutoa ushindani hata kwa wachezaji wao kucheza soka Ulaya.
“Kwa sasa, wachezaji wa Tanzania kucheza Ulaya ni ndoto kwa vile hawana elimu ya kutosha ya mpira, wanachezea kipaji, mfumo uliopo hauwezi kutoa zao sahihi kwa wachezaji waliokomaa kucheza soka la kulipwa Ulaya,” alisema kocha huyo raia wa Uholanzi.
Plujim alisema, pia mfumo wa uendeshaji wa soka la Tanzania ni mbovu hususani upangaji wa ratiba za mechi ambazo hazitoi nafasi kwa timu kupumzika kwa vile haulingani na jiografia ya nchi kwani zimekuwa zikisafiri umbali mrefu.
Katika hatua nyingine, Plujim alidai  Azam ni timu pekee iliyokuwa ikimpa presha.

No comments: