Sunday, 11 May 2014

Abiria zaidi ya 2000 wa kwama Lindi

Abiria waliokuwa wakisafiri kati ya Dar es Salaam na Lindi, wakitembea kwa miguu baada ya magari yao kukwama  katika tope eneo la Somanga,  Kijiji cha Marendego, Wilaya ya Kilwa, mkoani Lindi kutokana na mvua zinazoendelea kunyesha
Zaidi ya abiria 2,000 wanaofanya safari kutoka Dar es salamu kwenda mikoani ya Lindi, Mtwara, na Ruvuma waliokuwa wamekwama njiani  kwa siku tano mfululizo katika eneo la Marendengo wilayani Kilwa baada ya barabara kuzolewa na maji wameendelea na safari.
Akizungumza na gazeti hili jana, Katibu Tawala wa Wilaya ya Kilwa, Semion Manjulugu alisema kuwa magari 500 yalikwama katika eneo la Marendego baada ya mvua kuharibu miundombinu ya barabara yakiwamo madaraja.
Manjulugu alisema hadi kufikia jana jioni magari 102 yalikuwa yamekwisha ondolewa katika eneo hilo, huku abiria wakilazimika kutembea kwa miguu kwenda ng’ambo ya pili ya barabara kupanda mabasi mengine.
“Hizi siku mbili mvua haijanyesha na kama hali itaendelea hivihivi nina uhakika magari yote yatakuwa yameondoka katika eneo lile,” alisema Manjulugu.
Alisema kuwa jitihada za kuyakwamua magari hayo ziliongozwa na Naibu Waziri wa Ujenzi, Mhandisi Gerson Lwenge, aliyesema kuwa Serikali imetenga fedha kwenye bajeti ya mwaka huu kwa ajili ya ujenzi wa kipande cha barabara hiyo chenye urefu wa kilometa 12.
Alipotafutwa kwa njia ya simu Mhandisi Lwenge ili kufafanua ni kiasi gani cha fedha kimetengwa kwa ajili ya gharama za ujenzi huo, simu yake iliita kisha ikazima.
Awali, Kaimu Mkuu wa Mkoa wa Lindi, Agnes Hokororo alisitisha mabasi  kusafirisha abiria   baada ya kutembelea eneo na  kukuta magari zaidi ya 250 yakiwamo ya abiria na mizigo.
Hokororo alisema kwa kuwa  hali ya barabara kilometa 17 siyo  nzuri ni vyema wasafirishaji  na  wasafiri  wasio na safari za haraka kusitisha, sababu eneo hilo limekuwa  ni tatizo kwa sasa mpaka utaratibu wa kutengeneza utakapokamilika.
 Alisema ofisi yake kwa kushirikiana na Wizara ya Ujenzi inalichukulia  suala hilo kwa umuhimu wa kipekee kuhakikisha  matengenezo ya eneo hilo yanakamilika na wananchi wa mikoa ya Lindi na Mtwara waweze kusafiri kwa uhakika nyakati zote.
 Alisema  anatambua ni wajibu wa Serikali  kupitia Wizara ya Ujenzi  kufanya jitihada za haraka za kuwapatia msaada wananchi wa mikoa ya Lindi na Mtwara, kwa kutengeneza kipande hicho  ambacho kimeharibika vibaya kutokana na mvua zinazoendelea kunyesha na kuleta adha kwa abiria na hata watembea kwa miguu.

No comments: