Sunday, 11 May 2014

Gari 700 mpya za polisi kununuliwa kuelekea uchaguzi 2015

Serikali inatarajia kununua magari mapya 700 kwa ajili ya Jeshi la Polisi ambayo yatatumika kwenye shughuli mbalimbali ukiwamo uchaguzi mkuu utakaofanyika mwakani.
Kauli hiyo ilitolewa jana Dar es Salaam na Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mathias Chikawe alipokuwa akifungua Baraza la Wafanyakazi la Wizara hiyo kujadili bajeti ya mwaka 2014/15.
Waziri Chikawe alisema Serikali imejipanga kudhibiti uhalifu nchini kwa kuhakikisha askari wanapata vifaa vya kisasa yakiwamo magari 700 ambayo pia yatatumika kusimamia hali ya usalama wakati wa uchaguzi mkuu.
“Kwenye bajeti hii polisi imepata ongezeko zuri tu hasa kwenye vifaa kama magari, wamepata fedha za kutosha. Tunakusudia kwa ajili ya kujipanga na chaguzi kubwa mbili zijazo kununua siyo chini ya magari 700 ,”alisema.
Waziri huyo alisema magari hayo ni kwa ajili ya matumizi ya polisi kwa shughuli zao zote zikiwamo za kupambana na biashara ya dawa za kulevya, uchaguzi na operesheni mbalimbali watakazotakiwa kuzifanya.  Alifafanua kuwa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi inatarajia kutumia Sh955.9 bilioni ambapo kati ya hizo Sh691.5 bilioni ni kwa ajili ya matumizi ya kawaida na Sh264.3 bilioni ni za maendeleo.
Alisema Idara ya Polisi ina uwezo wa kukusanya fedha nyingi na kwamba kwa mwaka 2014 imekusanya zaidi ya asilimia 120 kwa miezi mitatu iliyopita.
“Tunakusanya kitu kinaitwa maduhuli. Kwa mfano polisi hasa trafiki kwa kuwakamata watu wanaokiuka sheria za barabarani wanakusanya pesa nyingi. Idara ya Uhamiaji kwa kutoa vibali nao wanakusanya pesa nyingi,” alisema na kuongeza iwapo Idara ya Zimamoto itasimamiwa ipasavyo inaweza kuingiza fedha nyingi kuliko Sekta ya Kilimo nchini.
Alieleza hayo wakati akijibu swali la kwa nini idara hiyo ameitaja kuwa chanzo cha mapato makubwa wakati ndiyo inayolalamikiwa na wananchi kwa kuwa na vifaa chakavu. Tunaanza kuajiri watu zaidi ya 800 mategemeo yetu katika miaka miwili mitatu ijayo kitengo hiki kitafanya kazi vizuri sana.”

No comments: