Wanamuziki Nguza Viking na Papii Kocha wanaotumikia kifungo cha maisha jela, wamemuomba Rais Jakaya Kikwete awasamehe kwa makosa waliyofanya.
Nguza na mwanaye Papii walitoa ombi hilo kupitia
wimbo wakati wakitumbuiza katika maadhimisho ya Siku ya Magereza
yaliyofanyika Chuo cha Magereza Ukonga jijini Dar es Salaam.
Ombi hilo waliliwasilisha kupitia kwa Waziri wa
Mambo ya Ndani ya Nchi, Mathias Chikawe aliyekuwa mgeni rasmi kwenye
sherehe hizo ambapo Nguza maarufu Babu Seya na mwanawe, Johnson Nguza
(Papii Kocha), walitumbuiza wakiwa na Bendi ya Wafungwa. Walimwomba
Waziri Chikawe kufikisha ombi lao kwa Rais Kikwete.
Babu Seya na Papii Kocha walitoa burudani hiyo
huku wakighani mashairi yenye ujumbe wa kuomba Rais awasamehe, hali
iliowafanya mamia ya watu waliofurika kwenye hafla hiyo kutulia kimya,
wengine wakilengwa na machozi.
Akiimba huku akitabasamu, Papi Kocha alikuwa
akionyesha mikono ya kuomba msamaha na kusema: “Kosa gani sisi
tusilosamehewa; vifungo vya maisha, miaka 30 gerezani havifundishi.”
“Waziri Chikawe tunaomba umfikishie Rais Jakaya
Kikwete ombi letu, mwambie atusamehe. Hata Petro alimkana Yesu mara
tatu, lakini Yesu alimsamehe kwa nini sisi….,” alisikika akiimba Papi
Kocha na baadhi ya wananchi waliohudhuria uwanjani hapo wakiinamisha
vichwa chini na wengine kutokwa na machozi.
Akijibu ombi hilo wakati akiwahutubia wananchi
Waziri Chikawe alisema: “Nimesikia maombi yenu, yamefika na nitajitahidi
kuyafikisha kwa Rais Kikwete.”
Chikawe akijibu ombi hilo alisema “Mtu
akishatumikia kifungo kwa miaka saba au 10 gerezani nina hakika kama ana
moyo na nafasi ya kuacha, atakuwa amebadilika hivyo anaweza kupewa
msamaha.”
Baadaye Chikawe alitembelea mabanda ya maonyesho
na Bendi ya Wafungwa ikipewa tena nafasi ya kutumbuiza. Babu Seya
aliimba wimbo maarufu wa ‘Seya tucheze wote’ na umati wa watu kutoka
kwenye mabanda ya maonyesho na kumiminika jukwaani kucheza wakiwamo
askari magereza na wakishangilia jambo lililowafanya askari kuzuia bendi
hiyo kuendelea kutumbuiza.
Awali, Kamishna Jenerali wa Magereza nchini, John
Minja alitoa wito kwa wananchi kushirikiana na Magereza katika
kutekeleza majukumu ya jeshi hilo.
No comments:
Post a Comment