Friday, 20 June 2014

Wakimbizi duniani kote wafika milion 50

Wakimbizi karibu na uwanja wa Bangui,

Ikiwa leo ni Siku ya Wakimbizi Duniani, Shirika la Kuhudumia Wakimbizi katika Umoja wa Mataifa, UNHCR, imetoa ripoti inayoonyesha kuwa idadi ya wakimbizi, watafuta hifadhi salama nje ya nchi zao na wakimbizi wa ndani, imeongezeka kote duniani na kuzidi watu milioni 50 kwa mara ya kwanza tangu vita vikuu vya pili.
Ripoti hiyo ya UNHCR ya kila mwaka kuhusu mwelekeo wa wakimbizi duniani, ambayo inatokana na takwimu zinazokusanywa na serikali, mashirika yasiyo ya kiserikali, UNHCR yenyewe na wadau wengine, inaonyesha kuwa watu milioni 51.2 walilazimika kuhama makwao mwishoni mwa mwaka 2013, idadi hiyo ikiwa ni milioni sita zaidi ya idadi ya milioni 45.2 iliyoripotiwa mwishoni mwa mwaka 2012
Ongezeko hilo kubwa lilichangiwa hasa na mzozo wa Syria, ambao mwishoni mwa mwaka uliwalazimu watu milioni 2.5 kuikimbia nchi yao, na kulazimu wengine milioni 6.5 kuwa wakimbizi wa ndani. Barani Afrika, idadi kubwa ya watu wamelazimika kuhama upya nchini Jamhuri ya Afrika ya Kati na Sudan Kusini mwishoni mwa mwaka 2013. Antonio Guterres ni Kamishna Mkuu wa UNHCR
"Tuna ongezeko kubwa la matatizo mapya, na wakati huo huo, matatizo ya zamani hayaonyeshi kupungua. Na hali hiyo inazua mizozo mingi inayowalazimu watu wengi kukimbia makwao, na hilo linatoa shinikizo kubwa mno, siyo tu kwa UNHCR, bali pia kwa mashirika yote ya kibinadamu yanayojaribu kuitikia mizozo hiyo."
Bwana Guterrs amependekeza mwarubaine wa matatizo hayo
"Ni muhimu mno kwa jamii ya kimataifa kuchagiza rasilmali za fedha tunazohitaji kutekeleza majukumu yetu, na wakati huo huo, kuweka mazingira yatakayoweka kikomo kwa msururu huu wa migogoro."

No comments: