WANACHAMA wapato 250 wa Yanga wamejiorodhesha na kusaini ili
kuzuia Mwenyekiti wao, Yusuf Manji, asiendelee kuiongoza klabu, lakini
yeye wala hana habari nao, badala yake amempa kazi tatu mmoja wa watu
wake aliyeenda Brazil kumaliza kazi juu ya ujio wa kocha wao mtarajiwa,
Marcio Maximo.
Tayari Yanga walishamtumia Maximo CD tatu za mechi
za Yanga ambazo kocha huyo alizipokea na kuangalia ubora wa nyota
wanaoitumikia klabu hiyo kwa sasa, ili akija ajue mahali pa kuanzia.
Taarifa ambazo Ukombozi Mimezipata kutoka kwa
mmoja wa mabosi wa juu wa Yanga, imesema Mwenyekiti wa Kamati ya
Mashindano ya Nje ambaye ni mtu muhimu katika Kamati ya Usajili, Seif
Ahmed ‘Seif Magari’ leo Alhamisi atakuwa ndani ya Uwanja wa Itaquerao
jijini Sao Paulo, Brazil kutazama mechi ya ufunguzi ya Kombe la Dunia
kati ya wenyeji na Croatia. Seif atatazama mechi zisizopungua tano za
michuano hiyo.
Bosi huyo alisema Seif mara baada ya kushuhudia
mchezo wa ufunguzi, atakutana na Maximo kujadiliana naye mambo
mbalimbali ambayo ndiyo yatatoa picha halisi ya ujio wa kocha huyo
mwenye msimamo mkali anayesimamia nidhamu kwa kiasi kikubwa.
Alisema baadhi ya mambo ambayo bosi huyo mwenye
uzoefu mkubwa katika kusajili atazungumza na Maximo ni kuhusu ubora wa
wachezaji na aina ya wachezaji anaowataka huku ajenda nyingine zikiwekwa
siri nzito ingawa Mwanaspoti linajua kuwa hata suala la maandalizi ya
kambi ni kitu kitakachojadiliwa katika kikao hicho.
“Hao wanaompinga Manji acha waendelee, bosi huku
anaendelea na majukumu yake, Seif ameshaondoka nchini tangu jana (juzi
Jumanne) yupo Brazil na kesho (leo Alhamisi) atakwenda kuangalia mechi
ya ufunguzi ya Kombe la Dunia na kujadiliana mambo kadhaa na Maximo,”
alisema bosi huyo,” kilisema chanzo chetu.
“Mwenyekiti (Manji) hataki maneno, Seif alikuwa
anakwenda Brazil kwa safari zake, lakini hapo hapo akaunganishiwa na
kazi za kwenda kufanya na Maximo kwa ajili ya timu na hilo linaweza
kufanyika wakati wowote baada ya mchezo wa ufunguzi kwa kuwa Seif
atakuwa huko kuangalia mechi zisizozidi tano.”
Wakati huohuo, Katibu wa Baraza la Wazee la Yanga,
Ibrahim Akilimali, amesema amepokea kwa mshtuko mkubwa taarifa za
wanachama 250 kujiorodhesha kwa lengo la kumpinga Manji baada ya
kuongezewa muda wa uongozi kwa mwaka mmoja.
“Sisi tulikubaliana tukiwa wanachama 1,663 tena
kwa moyo mmoja kwamba Mwenyekiti aendelee kwa mwaka mmoja, sasa iweje
hawa waibuke na kupinga?” Alihoji Akilimali.
Akilimali aliwataka wanachama kutulia na kutazama
jinsi uongozi unavyofanya kazi kuandaa kikosi kitakachoshiriki msimu
ujao wa Ligi Kuu Bara na Kombe la Shirikisho Afrika.
Alisema Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) nalo
halina mamlaka ya kubatilisha uamuzi huo wa mkutano wao kwani haukuwa
uamuzi wa Manji binafsi bali ni wa wanachama wa klabu hiyo.
No comments:
Post a Comment