Watu sita wamefariki dunia na wengine 12 kujeruhiwa baada ya kutokea ajali iliyohusisha magari matatu, eneo la Lugalo, jijini Dar es Salaam jana.
Kamanda wa Polisi, Mkoa wa Kipolisi Kinondoni
Camillius Wambura, alithibitisha kutokea kwa ajali hiyo na kueleza kuwa
ilitokea baada ya gari la abiria aina ya DCM kupoteza mwelekeo na kuhama
njia, kisha kuligonga gari jingine la abiria lililokuwa upande wa pili,
ambalo nalo liligonga gari lililokuwa mbele yake.
“Kati ya waliofariki dunia, watatu ni wanawake na
watatu wengine ni wanaume. Majeruhuri wanane kati ya 12 ni wanaume,
wanne ni wanawake na wawili kati yao wamepelekwa Hospitali ya Taifa
Muhimbili kwa matibabu zaidi,” alisema Kamanda Wambura na kubainisha
kuwa baada ya ajali hiyo madereva wa magari yote walikimbilia
kusikofahamika.
Mkuu wa Hospitali ya Lugalo, Brigedia Jenerali Dk.
Josiah Mekere alisema kuwa amepokea maiti za watu sita na majeruhi 12
na kwamba wawili walihamishiwa katika hospitali ya Taifa Muhimbili kwa
matibabu zaidi akieleza kuwa wameumia zaidi maeneo ya kichwani.
‘’Wengi wamepata madhara kichwani, waliopelekwa
Muhimbili (wawili) ni kwa ajili ya matibabu na uchunguzi zaidi kwa kuwa
wanahitaji kufanyiwa kipimo cha CT scan,’’ alisema Dk. Mekere.
Akisimulia ajali ilivyotokea David Jailos, mkazi
wa Tegeta aliyejeruhiwa mdomo na mguu katika ajali hiyo alisema: “Nikiwa
katika daladala kutoka Ubungo kwenda Tegeta iliyokuwa katika mwendo
kasi, dereva alitaka kulipita gari lililokuwa kulia kwake, lakini
alipotokeza ili apite, akakuta kuna gari na kushindwa kurudi eneo lake
kutokana na mwendo kasi, hivyo kuligonga kwa nyuma gari la mbele yake.
Alifafanua kuwa baada ya kuligonga, gari hilo nalo
likagonga gari la mbele yake, hivyo ajali hiyo kuhusisha magari matatu,
mawili ya abiria yaliyokuwa yakienda Kunduchi na jingine Tegeta.
Majeruhi mwingine, Jamila Mohamed mkazi wa
Kigamboni aliyeumia mkono na bega alieleza kwa uchungu kuwa mtoto
(Nasseri Nassoro) ni miongoni mwa abiria sita waliofariki kwenye ajali
hiyo. Alisema kuwa alishtukia kioo kimemwangukia kikiwa kimesambaa na
mtoto wake aliyekuwa amekaa naye kiti kimoja akiwa amemwangukia na baada
ya kutolewa ndani ya gari, ndipo alipobaini kuwa amefariki dunia.
“Gari yetu ilikuwa imesimama, sikuelewa
kilichoendelea zaidi ya kusikia mtikisiko mkubwa na mwanangu
akaniangukia, baada ya hapo sikufahamu kilichoendelea hadi
nilipofikishwa hapa hospitalini na kuona mwanangu ni miongoni mwa
waliofariki katika ajali, ambayo siwezi kuielezea, “alisema Jamila.
No comments:
Post a Comment