Idara ya Uhamiaji nchini Tanzania imegundua maficho ya wasichana
waliosafirishwa kutoka nchi za India na Nepal mjini Dar es Salaam ambao
wanatumikishwa katika biashara zisizo halali katika maeneo mbalimbali
jijini humo
Katika siku tano zilizopita, idara ya uhamiaji jijini Dar es salaam
inasema imewaokoa wasichana 51 raia wa India na Nepal waliohifadhiwa
katika nyumba kadhaa na kutumikishwa katika biashara ya ngono na
nyinginezo na kuwakamata wafanyabiashara wenye asili ya kiasia
wanaotuhumiwa kusafirisha wasichana hao na kuwatumikisha hapa nchini
Mwishoni mwa mwezi uliopita wasichana wengine 17 walikutwa wamehifadhiwa
katika nyumba moja eneo la Msasani jijini Dar es salaam kwa zaidi ya
miezi mitatu huku wakidaiwa kutumika kwenye biashara ya ngono huku
wengine 34 wakikamatwa jana eneo la Mwananyamala jijini humo.
Wafanyabiashara waliotiwa nguvuni wanadai kuwa waliwaleta nchini humo
wasichana hao kushiriki kucheza ngoma za asili kutoka mataifa yao katika
club mbali mbali za usiku maarufu-Mujra na walikuwa wamehifadhiwa
katika jengo moja huku pasi zao za kusafiria zikiwa zimechukuliwa na
aliyetambuliwa kama meneja wao
Afisa Uhamiaji Mkaguzi wa mipaka Doto Selasini amesema wasichana hao
wenye umri wa chini ya miaka 26 waliingizwa nchini kwa njia halali kwa
ahadi ya meneja wao kukaa nchini kwa siku 14 kwa ajili ya kushiriki
ngoma za utamaduni wa mataifa yao, lakini wamekuwa wakitafutiwa wateja
na baadae kulazimishwa kufanya vitendo vya ngono na kwamba wamefanikiwa
kupata taarifa zao kupitia raia wema
Meneja wa wasichana hao Savio Menes ambaye naye ametiwa mbaroni na
maafisa wa uhamiaji amesema wasichana hao aliwaingiza nchini kupitia
wakala aliyeko nchini India na kudai kuwa walikuja kushiriki ngoma za
utamaduni za bara la Asia
Hata hivyo wasichana wenyewe walipohojiwa na maafisa wa uhamiaji
walikiri kuishi katika mazingira magumu na kufanya biashara isiyo halali
na kwamba wako tayari kurejeshwa makwao India na Nepal. Wamedai kuwa
wamekuwa chini ya ulinzi mkali huku wakitolewa usiku na kupelekwa katika
mahoteli na kurejeshwa alfajiri na hawakuruhusiwa kuwa na mawasiliano
na mtu yeyote.
Taarifa zilizopatikana baadaye zilieleza kwamba wasichana 17
waliokamatwa Mei 30 wamesafirishwa na kurejeshwa makwao India na Nepal
huku wafanyabiashara waliowaleta wakisubiri taratibu za kufunguliwa
mashtaka
No comments:
Post a Comment