Kama siyo kuzuiwa na mawaziri, Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), Jaji Frederick Werema jana angezua tafrani bungeni kutokana na kitendo chake cha kutaka kumpiga Mbunge wa Kigoma Kusini (NCCR-Mageuzi), David Kafulila.
Sakata hilo lilitokea jana asubuhi baada ya
Mwenyekiti wa Bunge, Mussa Azzan Zungu kuahirisha kikao cha Bunge hadi
jioni, ikiwa ni muda mfupi baada ya Werema na Kafulila kurushiana maneno
bungeni. Jaji Werema alichukia baada ya Kafulila kumwita mwizi, akijibu
mapigo baada ya mbunge huyo kuitwa tumbili na mwanasheria huyo.
Waliomzuia ni Waziri wa Ushirikiano wa Afrika
Mashariki, Samuel Sitta, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Uhusiano na
Uratibu), Stephen Wassira, Waziri wa Katiba na Sheria, Dk Asha-Rose
Migiro, Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, George
Simbachawene na Naibu Waziri wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Dk
Abdulla Juma Saadallah.
Mawaziri hao walimsindikiza Werema hadi nje ya Ukumbi wa Bunge na kutoweka.
Ilivyokuwa
Hali ilianza kuchafuka wakati Jaji Werema alipokuwa akijibu mwongozo uliombwa na Kafulila kuhusu fedha za akaunti ya Escrow.
Katika mwongozo huo, Kafulila alisema Wizara ya
Nishati na Madini kupitia Waziri wake, Profesa Sospeter Muhongo
alizungumza uongo mara mbili bungeni kuhusiana na fedha za akaunti ya
Escrow.
“Alisema uongo mbele ya Waziri Mkuu na Mwanasheria
Mkuu wa Serikali katika maeneo mawili, kwamba uamuzi wa kutoa fedha za
Escrow kwa IPTL ulikuwa wa Mahakama na Serikali isingeweza kwenda
kinyume...” alisema.
Alisema katika hukumu hiyo ya Septemba mwaka jana,
hakuna mstari hata mmoja unaosema kuwa fedha za Escrow wapewe Kampuni
ya IPTL.
“Profesa Muhongo aliliambia Bunge kuwa Serikali
ililipa fedha hizo ili kuondokana na kesi hiyo lakini ninazo nyaraka za
Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco), kuteua kampuni mbili za uwakili
kwenda kuiwakilisha katika kesi nchini Uingereza,” alisema Kafulila.
Alisema kwamba aliomba mwongozo sababu huo umekuwa
mwendelezo wa kuzungumza uongo bungeni... “Naibu Waziri (Nishati na
Madini - Stephen Masele), alizungumza uongo bungeni tukaambiwa kuwa
wamekutana katika sherehe za kuzaliwa yakaisha, haiwezekani, Bunge ni
sehemu ya kuisimamia Serikali.
“Haiwezekani Bunge ling’olewe meno liwe ni chombo ambacho mtu
anaweza kuzungumza uongo bila kuchukuliwa hatua kwenye jambo hili ambalo
linaligharimu taifa mabilioni ya fedha.”
Baada ya madai hayo, Jaji Werema alisimama na
kusema: “Bunge hili liliamua mambo mawili, kwanza kulikuwa suala la
rushwa na CAG apewe kazi ya kuchunguza na kutoa taarifa bungeni. La pili
kuna watu walitoa vipeperushi humu bungeni, miongoni mwao ni huyu
anayetoa maneno machafu (Kafulila),” alisema Werema na kumfanya John
Mnyika (Mbunge wa Ubungo-Chadema), kuomba mwongozo uliokataliwa na
Mwenyekiti Zungu.
Hata hivyo, Mnyika na Kafulila waliendelea kuomba
mwongozo, lakini Zungu aliwataka wamsikilize Jaji Werema kwa sababu naye
alimsikiliza Kafulila. Werema aliendelea: “Suala la Escrow ni suala
linalotokana na wanahisa wawili ambao ni IPTL na Mechmar… Pesa ya
Serikali haikai kwenye Escrow.”
Hata hivyo, alikatishwa na kelele za Mnyika ambaye alitaka mwenyekiti kumpa nafasi ya kutoa taarifa.
“Sasa kama unataka kuleta mambo ya nje ndani ya
Bunge ningojee pale nje,” Jaji Werema alisema wakati wabunge hao
walipokuwa waking’ang’ania kutoa taarifa.
Alisema ugomvi huo ulitokana na wanahisa wawili
hao kila mmoja akitaka IPTL ifilisiwe ili waachane. Alisema Serikali
iliingia katika mgogoro huo kwa sababu ya mikataba ya udhamini na kwamba
wakati wanagombana iliamua kufungua akaunti ya Escrow.
Hata hivyo, kuliibuka maneno tena kutoka upande wa
Kafulila na Jaji Werema alitaka kusikilizwa hata kama yeye ni mtuhumiwa
katika suala hilo.
“… Wanyankole wanasema tumbili hawezi kuamua
masuala ya misituni… sikiliza tumbili, sikiliza ‘please’ (tafadhali),”
alisema Werema.
Sentensi hiyo iliamsha kelele kutoka upinzani na Kafulila alisikika akimwita Werema mwizi.
Hata hivyo, Zungu alizuia vurumai hizo kwa kumtaka
Jaji Werema kukaa na kisha kuwataka wabunge hao wawili kupeleka
ushahidi wao Taasisi ya Kuzuia na Kupambana Rushwa (Takukuru).
Mara tu baada ya Zungu kuahirisha Bunge, Jaji
Werema alisimama na kumfuata Kafulila lakini kabla hajamfikia, mawaziri
hao walimzuia na kumsindikiza hadi nje.
Baadaye, Kafulila na Mnyika waliitisha mkutano na
waandishi wakitaka Waziri Mkuu, Mizengo Pinda afute uongo huo bungeni
ndani ya siku mbili na akishindwa, watakusanya sahihi za wabunge
kumuondoa katika nafasi hiyo.Alipohojiwa kama ni vyema kwa Wassira alisema walimsihi Werema kuachana na Kafulila na kuendelea na shughuli zake.
No comments:
Post a Comment