Msemaji wa kambi hiyo, John Mnyika ambaye amesema katika kipindi cha miaka 39 kuanzia 1970 hadi 2008, Sh9.6 trilioni zilitoroshwa kiharamu kwenda nje |
Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, imeilipua Serikali kwa kushindwa kudhibiti utoroshwaji mkubwa wa fedha kwenda nje.
Msemaji wa kambi hiyo, John Mnyika alisema katika
kipindi cha miaka 39 kuanzia 1970 hadi 2008, Sh9.6 trilioni zilitoroshwa
kiharamu kwenda nje.
“Utoroshaji wa fedha hizi unasadikiwa kutokana na
ukwepaji wa kodi, na misamaha mikubwa ya kodi,” alisema Mnyika na
kuongeza; “Fedha nyingine zilitokana na usiri mkubwa wa mikataba baina
ya wawekezaji na Serikali, upotoshaji wa bei katika biashara na rushwa
katika mikataba na wawekezaji” alisema.
Mnyika alisema Serikali ya CCM haiwezi kukwepa
kuwajibika kwa sababu utoroshaji wa mapesa yote haya umefanyika wakati
na CCM ipo madarakani, ” alisema.
Mnyika alifafanua, utoroshaji huo wa fedha ulifanyika kwa mafungu na kutolea mfano mwaka 1980, Dola 570. 6 milioni zilitoroshwa.
Fedha hizo zilitoroshwa wakati hayati baba wa
Taifa mwalimu Jullius Nyerere akiwa madarakani na dola 1,566 milioni
zikatoroshwa 1985 wakati wa Rais Ali Hassan Mwinyi.
“Jambo la kusikitisha zaidi mwaka 2002
zilitoroshwa jumla ya Dola za Marekani 1,1010 milioni katika kipindi
ambacho Rais Benjamin Mkapa yuko madarakani,” alisema Mnyika.
Mnyika alisema kambi hiyo imesikitishwa na kitendo
cha Bunge kushindwa kuisimamia kikamilifu Serikali hususan Wizara ya
Nishati na Madini.
Alisema fedha zote zilizotoroshwa nchini tangu mwaka 1970 mpaka 2008 zinaweza kurejeshwa nchini kwa kuanzia na kuzibaini zilipo.
“Uchunguzi wa kina ufanyike kuzuia fedha hizo
katika akaunti za benki zilipotunzwa nje ya nchi na hatimaye kurejesha
fedha hizo nchini,” alisema.
Kitengo cha Financial Intelligence Unit (FIU) cha
Benki Kuu ya Tanzania (BoT) kimetakiwa kukusanya taarifa za
kiintelijensia na kuziwasilisha Takukuru ili uchunguzi ufanyike.
No comments:
Post a Comment