Tuesday 3 June 2014

Majambazi wavamia na kuiba ma milion ya fedha Mwanza

WATU wanaodhaniwa kuwa majambazi usiku wa kuamkia jana wamevamia kituo cha mafuta Smat Usagara, kilichopo wilayani Misungwi na kuiba kiasi kikubwa cha fedha.
Akizungumza na Tanzania Daima, mmoja wa watumishi wa kituo hicho, Janet Alex (36), mkazi wa Usagara, alisema kuwa akiwa kazini majira ya usiku wa saa tano, walikuja wateja wakiwa na gari wakihitaji mafuta aina ya petroli lita 200.
Alisema alianza kuwahudumia na zilipofikia lita 156 alivamiwa na kundi la majambazi wapatao 10 wakiwa na silaha na kuwaamuru wateja walale chini huku watatu wakiondoka naye kuelekea ofisini, ambako kulikuwa na sefu ya kutunzia fedha na kumwamuru awapatie fedha.
Alibainisha kuwa majambazi hao waliiona sefu hiyo na kuamua kuilipua kwa kitu kinachodhaniwa kuwa ni baruti na kuisambaratisha na kufanikiwa kuchukua fedha za mauzo ya siku tatu zilizokuwepo.
Janet alisema kuwa mauzo ya siku moja ni kati ya sh milioni 10, hivyo kiasi walichokichukua hakipungui sh milioni 30.
Alibainisha kuwa licha ya kuiba fedha zilizokuwamo kwenye sefu, pia walipora nyingine kwa wateja waliokuwamo kwenye gari lililokuwa likijaza mafuta.
Matukio ya ujambazi yameendelea kushamiri katika Jiji la Mwanza, ikiwemo Wilaya ya Misungwi eneo la Usagara ambapo hivi karibuni majambazi walipora fedha katika kituo hicho pamoja na cha jirani yake, Lake Oil.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, Valentino Mlowola, amethibitisha kutokea kwa tukio hilo na kusema kuwa Jeshi la Polisi mkoani Mwanza linawahoji watu watatu kuhusiana na tukio hilo ambapo majina yao hakuwa tayari kuyataja kwa kuwa upelelezi bado unaendelea.

No comments: