Jaji mkuu Othuman Chande akizungumza na waandishi wa habari |
Mahakama Kuu ilitoa msimamo huo jana wakati ikitoa
uamuzi wa pingamizi la awali katika kesi ya kikatiba iliyokuwa
ikimkabili Waziri Mkuu Mizengo Pinda, lililowasilishwa na Jopo la
Mawakili wa Serikali wakiongozwa na Naibu Mwanasheria Mkuu wa Serikali
(DAG, George Masaju.
Kesi hiyo namba 24 ya mwaka 2013 ilifunguliwa na
Kituo cha Msaada wa Kisheria na Haki za Binadamu (LHRC) kwa kushirikiana
na Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS), dhidi ya Pinda na Mwanasheria
Mkuu wa Serikali (AG), aliyeunganishwa kama mlalamikiwa wa pili.
LHRC na TLS walikuwa wakidai kuwa Pinda alivunja
Katiba kutokana na kauli aliyoitoa bungeni, wakidai kuwa ni amri kwa
vyombo vya utekelezaji wa sheria kuwapiga wananchi wakati wa vurugu.
Hivyo, walikuwa wakiiomba mahakama, pamoja na
mambo mengine, itamke kuwa kauli hiyo ni kinyume cha Katiba na imwamuru
Pinda aifute hadharani.
Hata hivyo, Pinda na AG waliokuwa wakitetewa na
DAG Masaju akisaidiana na Mawakili wa Serikali Wakuu (PSA, Gabriel
Malata, Alecia Mbuya na Sarah Mwipopo), waliweka pingamizi la awali
dhidi ya kesi hiyo, wakitoa hoja tano za kuomba kesi hiyo itupiliwe
mbali.
Miongoni mwa hoja hizo ni pamoja na kwamba kesi
hiyo ni batili na iko mahakamani isivyo halali kwa kuwa inakiuka Katiba
ya Jamhuri ya Muungano ya Mwaka 1977 na Sheria ya Mamlaka, Kinga na Haki
za Wabunge, ya mwaka 1988.
Mawakili hao walidai kuwa Pinda analindwa na
Katiba Ibara ya 100 (1) na (2), ambazo zinamkinga mbunge kushtakiwa au
kufunguliwa shauri la madai mahakamani kwa jambo lolote alilolisema, au
alilolitenda, au alililoliwasilisha bungeni kwa njia ya maombi, muswada
au hoja.
Mahakama Kuu katika uamuzi wake jana ilikubaliana
na baadhi ya hoja za mawakili wa utetezi (Serikali) na kuitupilia mbali
kesi hiyo, lakini ikatamka kuwa wabunge na mawaziri wanaweza kushtakiwa
kwa kauli au jambo walilolitamka bungeni, linalokiuka sheria na haki za
binadamu.
Uamuzi huo ulisomwa na Kiongozi wa Jopo la Majaji
wa Mahakama Kuu, lililokuwa likisikiliza kesi hiyo, Jaji Kiongozi Fakih
Jundu kwa niaba ya majaji wenzake, Agustine Mwarija na Dk Fauz Twaib.
Katika uamuzi huo, majaji walikubaliana na hoja
tatu za pingamizi kuwa walalamikaji katika kesi hiyo hawakuwa na haki ya
kufungua kesi hiyo na kwamba walikosea taratibu za ufunguaji wa kesi
kama hizo kwa kuwa walikiuka amri na kanuni zinazoongoza Mashauri ya
Madai (CPC).
Katika hoja ya kwanza kuwa Pinda kama mbunge
analindwa na Katiba, jopo hilo lilisema kuwa ni kweli wabunge wanalindwa
na Katiba Ibara ya 100 (1) kuhusu haki na upendeleo (Previledge), yaani
haki na uhuru wa mjadala na maoni. Hata hivyo, lilikataa hoja za
utetezi kuwa wabunge wana kinga isiyo na mipaka ya kutokushtakiwa kwa
kauli au jambo lolote walilolitamka bungeni.
Badala yake jopo hilo lilikubaliana na hoja za mawakili wa
walalamikaji, kuwa japo wabunge wana kinga, lakini kinga yao ina mipaka
na kwa kuwa inadhibitiwa na masharti ya ibara nyingine za Katiba na
Sheria za Bunge.
Walalamikaji walikuwa wakitetewa na Peter Kibatala, Fulgence Massawe, Harold Sungusia, Mpale Mpoki na Jeremiah Mtobesya.
Kuhusu hoja ya pingamizi kuwa walalamikaji
hawakuwa na haki ya kufungua kesi hiyo, mahakama ilikubali kuwa kwa
walalamikaji katika kesi hiyo hawakuwa na haki ya kufungua kesi hiyo.
Ilifafanua kuwa anayepaswa kufungua kesi ni yule
tu aliyeathirika na kauli iliyotolewa na mlalamikiwa na si mashirika,
kwa kuwa kauli ya mlalamikiwa haikuyaathiri mashirika hayo yaliyofungua
kesi.
Mahakama ilifafanua kuwa mtu aliyeathirika na
kauli iliyotolewa bungeni anaweza kuwasilisha malalamiko yake kwa Spika
kwa mujibu wa Kanuni za Bunge hasa kanuni ya 71 (1) .
Ilisema kwa kuwa kanuni hiyo haitoi nafasi kwa
mashirika, basi mashirika yanaweza kufungua kesi mahakamani kwa kufuata
taratibu za kisheria, ikiwa kauli iliyotolewa bungeni itakuwa
imeyaathiri moja kwa moja.
Akizungumzia uamuzi huo, Wakili Kibatala alisema
kuwa ingawa kesi yao imetupiliwa mbali, lakini kitendo cha mahakama
kutamka kuwa wabunge hawana kinga isiyo na mpaka na kwamba wanaweza
kushtakiwa ni ushindi mkubwa.
Kwa upande wake Wakili Sungusia alisema kuwa wiki
ijayo watakutana na jopo la mawakili ili kujadili uamuzi huo na hatua za
kuchukua kama watakata rufaa Mahakama ya Rufani au la.
Katika pingamizi lao, mawakili wa utetezi pia
walidai kuwa hati ya madai iliyowasilishwa mahakamani haijasainiwa kwa
kuwa waliosaini si walalamikaji na kwamba hawajaonyesha kama wamepewa
mamlaka ya kusaini kwa niaba ya walalamikaji.
Walidai kuwa walalamikaji ni taasisi yaani LHRC na
TLS, lakini waliosaini ni Dk Hellen Kijo Bisimba kwa niaba ya LHRC na
Wakili Francis Stolla (Rais wa TLS) kwa niaba ya TLS, lakini hawaonyeshi
kama wamepewa mamlaka ya kusaini hati hiyo.
Pia mawakili wa walalamikaji walidai kuwa hati ya
madai ina dosari za kisheria kwa kuwa kwa mujibu wa kanuni za Uendeshaji
wa Mashauri ya Madai (CPC), hati inapaswa kueleza madai tu na si
ushahidi, hoja wala maoni, walalamikaji wameelezea na maoni yao binafsi.
Upande wa walalamikaji katika majibu yao walidai
kuwa walalamikaji wana haki ya kuwashtaki walalamikiwa. Wanadai kuwa
kinga ya mbunge ina mpaka na inamlinda kwa shughuli za bunge tu na
kwamba hati hiyo haina dosari huku wakidai kuwa hata kama zipo dosari za
kisheria, basi zinaweza kurekebishwa.
Pinda alitoa kauli hiyo inayolalamikiwa, katika mkutano wa 11 wa
Bunge wakati wa kipindi cha maswali ya papo kwa papo kwa Waziri Mkuu
bungeni, Juni 20, 2013.
Alikuwa akijibu swali la nyongeza la Mbunge wa
Kilwa Kaskazini (CCM), Murtaza Mangungu kuhusu msimamo wa Serikali,
pamoja na mambo mengine, malalamiko dhidi ya vyombo vya dola katika
baadhi ya maeneo kama Mtwara, kuwapiga wananchi.
“Ukifanya fujo, umeambiwa usifanye hiki, ukaamua
kukaidi, utapigwa tu... Eeh, hamna namna nyingine, eeh maana lazima
tukubaliane kwamba nchi hii tunaiendesha kwa misingi ya kisheria.
“Sasa kama wewe umekaidi, hutaki unaona kwamba ni
imara zaidi... wewe ndiyo jeuri zaidi... watakupiga tu na mimi nasema
muwapige tu, kwa sababu hakuna namna nyingine, eeh… maana tumechoka,”
inasomeka hati ya madai ikinukuu maneno ya Pinda.
No comments:
Post a Comment