Sunday 22 June 2014

Boban kurudi simba


Haruna Moshi Bobani.
BAADA ya kumwongezea mkwanja straika, Mrundi Amissi Tambwe viongozi wa kundi la Friends of Simba wamekuwa katika majadiliano juu ya uwezekano wa kumrejesha kundini kiungo wa zamani wa timu hiyo Haruna Moshi Bobani au la endapo watafanikiwa kuchukua madaraka.
Boban kwa sasa amemaliza mkataba wake na Coastal Union ya Tanga aliyokuwa akiichezea msimu uliopita hivyo Simba inawaza namna ya kumrejesha kundini lakini inasemekana kuwa nidhamu ndogo ya mchezaji huyo imekuwa changamoto kubwa katika kufanya uamuzi.
Chanzo cha ndani kutoka kwenye kundi hilo kilieleza kuwa baadhi ya wadau walipendekeza Boban kurejeshwa kutokana na aina yake ya uchezaji kuwa angeweza kumchezesha zaidi Tambwe na kumwezesha kupachika mabao mengi zaidi yatakayoisaidia timu hiyo.
Utata zaidi kuhusu kumrejesha Boban umejitokeza pale viongozi hao walipoangalia msimamo wa kocha wa sasa wa klabu hiyo Mcroatia Zdravko Logarusic waliyepanga kuendelea kumtumia kwa msimu ujao endapo watafanikiwa katika uchaguzi wa msimu ujao.
Kocha Logarusic amekuwa na uvumilivu mdogo juu ya wachezaji wenye nidhamu haba hivyo ujio wa Boban unaweza kuongeza matatizo katika klabu hiyo iliyokuwa na mwendo wa kusuasua msimu uliopita.

No comments: