Kamishna wa Operesheni na Mafunzo wa Polisi, Paul Chagonja
Hili linawezekana kuwa ni tukio la kwanza na la aina yake. Majambazi wanaokisiwa kuwa sita, wakiwa na pikipiki tatu, juzi walivamia Kituo Kidogo cha Polisi Mkamba kilichopo Kimanzichana, Wilaya ya Mkuranga, Pwani na kuua askari mmoja na mgambo na kujeruhi mgambo mwingine na kisha kupora bunduki tano na risasi 60 usiku wa kuamkia juzi.
Polisi aliyeuawa ni Konstebo Joseph Ngonyani na
majeruhi Venance Francis na Mariamu Mkamba ambao walipelekwa katika
Hospitali ya Wilaya Mkuranga kwa matibabu.
Kwa mujibu wa wakazi wa eneo hilo, majambazi hayo
yalikuwa na taarifa kwamba kituo hicho kina silaha za moto na kuweka
mpango wa kukivamia usiku baada ya kupiga hesabu na kujiridhisha kwamba
polisi kutoka Kibiti, wilayani Rufiji au Mkuranga wasingeweza kufika
hapo kabla ya wao kutekeleza azma yao.
Mkazi wa Kimanzichana, Mohamedi Muba alisema
wananchi wenzake walimwambia kuwa majambazi hayo yalifika kituoni hapo
saa saba usiku na kuvamia kituo hicho wakitaka funguo za kufungulia stoo
zilipohifadhiwa silaha.
“Kituo cha Kimanzichana kipo mbali sana na vituo
vingine vya Kibiti na Mkuranga, ni kama kilometa 30 hadi 35, hivyo kwa
wakati huo wa usiku wa manane ingekuwa vigumu kuwahi kutoa msaada,”
alisema mkazi mwingine ambaye hakutaka kutajwa jina.
Mkazi huyo alisema baada ya kubishana na askari
huyo aliyekuwa na ufunguo, majambazi hayo yalitumia nguvu kumlazimisha
kutoa funguo.
Huku mzozo huo ukiendelea, majambazi wengine
walikuwa wakiwashambulia askari mgambo kwa mapanga na walipoona askari
amegoma kutoa funguo walimpiga risasi na kuzichukua kisha kufungua na
kuchukua silaha na kutokomea kusikojulikana.
Alisema majambazi hayo yalionekana kujipanga na kuwa na taarifa zote kuhusu hali ya ulinzi katika kituo hicho.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Pwani, Ulrich Matei
alipoulizwa kuhusiana na tukio hilo, alisema ameagizwa na Kamishna wa
Operesheni na Mafunzo wa Polisi, Paul Chagonja kwamba ndiye
atakayelizungumzia suala hilo.
“Kwa sasa nipo chumba cha kuhifadhia maiti katika
Hospitali ya Taifa Muhimbili ninashughulikia mwili wa askari aliyeuawa,
Makao Makuu watalizungumzia zaidi,” alisema Kamanda Matei.
Chagonja alonga
Akizungumzia tukio hilo jana, Chagonja alisema
majambazi hayo yalitumia bunduki na mapanga kumuua askari huyo na
kuwajeruhi mgambo hao na kutokomea na bunduki mbili aina ya Sub Mashine
Gun (SMG), mali ya Jeshi la Polisi na bunduki tatu aina ya shortgun,
mali ya raia ambazo zilikuwa kituoni hapo zikisubiri kupelekwa kwenye
ghala kuu la silaha.
“Polisi inalaani vikali kitendo hicho na imeanzisha msako mkali
na itahakikisha inayatia mbaroni majambazi hayo,” alisema Chagonja.
Aliwaomba wananchi wenye taarifa za wahalifu hao
kujitokeza au kupiga simu ili waweze kuyakamata na kuyafikisha
mahakamani na kupata silaha hizo. Alitoa namba ya Mkuu wa Jeshi la
Polisi Tanzania (IGP), Ernest Mangu na ya Kamanda wa Polisi Mkoa wa
Pwani ambazo ni 0754 785 557 na 0715 009 953 kwa ajili ya kutoa taarifa
zitakazowezesha kupatikana kwa watu wenye silaha au wanaotiliwa shaka
kuhusiana na tukio hilo.
“Kwa sasa wananchi wawe watulivu, waendelee na
shughuli zao lakini wafahamu muda wote polisi hatutalala, tutayasaka
usiku na mchana na tutahakikisha tunayatia mbaroni,” alisema.
Kimanzichana na Mkuranga
Habari za majambazi hayo kuvamia kituo hicho
zilisambaa haraka mapema asubuhi kutokana na msako mkali ulioanza
kufanywa muda mfupi baada ya tukio hilo.
Madereva wanaotumia barabara ya Dar es Salaam - Kilwa walisema magari yote yalisimamishwa katika vizuizi na kupekuliwa.
“Kila gari lililopita katika Kijiji cha
Kimanzichana lilifanyiwa upekuzi ili kutafuta silaha hizo, ukikutwa na
mkaa au mbao kazi unayo,” alisema dereva wa daladala, Hussein Ali.
Alisema kutokana na msako huo, madereva wengi
walisitisha safari na dereva mmoja alisikika akimweleza mwenzake
aliyekuwa akielekea huko... “Usiende Mkuranga leo kuna msako mkali,
usipokutwa na mkaa au mbao gari lako hata likiwa na tatizo dogo tu
utakamatwa.”
No comments:
Post a Comment