KUNDI la wanachama matajiri wa Simba, Friends of Simba limegawanyika katika makundi mawili, moja linahangaikia usajili na lingine lipo bize na uchaguzi.
Lile linalopambana na usajili lina habari njema,
muda wowote kuanzia leo Jumamosi litashusha nchini vifaa viwili kutoka
Uganda tayari kwa mazungumzo ya mwisho ya usajili.
Chini ya Mwenyekiti wa Kamati ya Usajili Zacharia
Hans Poppe na rafiki yake Geofrey Nyange ‘Kaburu’ ndiyo wanaotajwa
kusimamia kazi hiyo ambapo siku yoyote kuanzia leo wanawashusha nchini
wachezaji hao ambao wanaweza kucheza kama mido na straika.
Mmoja ni Joseph Mpande anayeichezea Vipers SC ya
Uganda ambayo zamani ilikuwa ikijulikana kwa jina la Bunamwaya iliyopo
katika nafasi ya nne katika ligi kuu ya nchi hiyo. Mchezaji huyo
alijumuishwa katika kikosi cha Uganda ‘The Cranes’ kilichoshiriki
michuano ya wachezaji wa ndani ya Afrika CHAN iliyofanyika Afrika
Kusini.
Mbali na Mpande aliyezaliwa miaka 21 iliyopita
ambaye aliwahi kukunjana uwanjani na Haruna Niyonzima wakati wakitumikia
mataifa yao, pia katika mchakato huo Simba imemnasa kiungo mchezeshaji
Allan Kyambade kutoka klabu ya Express ya Kampala, Uganda.
“Nimeongea na mmoja wao kwa kuwa ni rafiki yangu,
yeye amenithibitishia kuwa wanakuja Tanzania kumalizia mazungumzo yao.
Kama unakumbuka huyo mshambuliaji aliwahi kutaka kupigana na Niyonzima
wakati fulani akiichezea Cranes,” alisema mmoja wa nyota aliyepo katika
kikosi cha Cranes. Hans Poppe hakupatikana kwa kuwa yuko safarini
nchini Malaysia.
Dili hiyo ikikamilika Simba itaachana na Wakenya wa Gor Mahia Rama Salim na Jerim Onyango waliozungumza na Kocha Logarusic.
No comments:
Post a Comment