Waziri Kivuli wa Fedha, James Mbatia. |
Wakati Serikali ikibanwa na wabunge kwa kushindwa kutekeleza Bajeti ya mwaka 2013/14 kutokana na kutegemea fedha za wahisani, Kamati ya Bunge ya Uchumi, Viwanda na Biashara imesema deni la taifa limeongezeka kwa Sh8.2 trilioni kwa kipindi cha miezi saba tu.
Ilisema jana kuwa hadi Juni, mwaka jana deni hilo
lilikuwa Sh21.2 trilioni lakini hadi Januari mwaka huu, deni hilo
lilipaa hadi Sh29.4 trilioni na fedha hizo zimekopwa kwa ajili ya
kuendeshea warsha, semina, safari, mafunzo na matengenezo ya magari.
Akiwasilisha taarifa ya kambi ya Upinzani, Waziri
Kivuli wa Fedha, James Mbatia alisema ukiligawanya deni hilo kwa idadi
ya Watanzania milioni 45, kila mwananchi atakuwa anadaiwa Sh600,000.
Kati ya Sh5.8trilioni za bajeti ya Wizara ya Fedha mwaka 2014/15, Sh4.3trilioni zimetengwa kwa ajili ya kulipa Deni la Taifa
Akiwasilisha taarifa ya Kamati, Mwenyekiti wake,
Luhaga Mpina alisema Sh24.18trilioni ni deni la Serikali, Sh3.75trilioni
ni deni la sekta binafsi na Sh1.15trilioni ni deni la Benki Kuu
Tanzania (BoT).
“Ongezeko hili la deni haliendi sambamba na kasi
ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo na ujenzi wa miundombinu ya
uchumi. Hali hii inajenga hofu kuwa huenda deni hili limekuwa ni
uchochoro wa ubadhilifu wa fedha za umma,” alisema Mpina.
Alisema licha ya Serikali mara kadhaa kueleza kuwa
deni hilo ni himilivu, kuna viashiria vinavyoonyesha kuelemewa kwa
taifa na mzigo mkubwa wa madeni.
“Mfano ni mapato ya ndani yamezidiwa na matumizi
ya kawaida hivyo kuifanya Serikali kukopa hata kwa ajili ya warsha,
semina, safari, mafunzo na matengenezo ya magari,” alisema Mpina.
“Deni la Taifa sasa limefikia asilimia 47 ya Pato
la Taifa na kwa kipimo cha bei ya sasa deni la taifa limefikia asilimia
24, huku deni la nje pekee likiwa ni asilimia 19” alisema Mpina na
kuongeza:
“Licha ya Mdhibiti na Mkaguzi wa Hesabu za
Serikali (CAG) kuahidi kwa muda mrefu kufanya ukaguzi maalumu wa deni la
taifa, hadi sasa taarifa yake haijawasilishwa. Ni lini taarifa hiyo
itawasilishwa bungeni ili kuwawezesha wananchi kufahamu undani wa jambo
hili?” alihoji.
Kamati hiyo pia iliilipua Serikali kwa kuuza
mashine za elekroniki (EFD), kati ya Sh600,000 hadi 700,000 kwa maelezo
kuwa kiwango hicho ni kikubwa kwa mzunguko wa biashara ya mtaji wa Sh14
milioni kwa sababu mtaji wake hauzidi Sh5milioni.
Mpina alisema mashine hizo zinatakiwa kugawiwa
bure kwa wafanyabiashara wenye kipato chini ya Sh40milioni na kufafanua
kuwa chombo hicho chenye taarifa muhimu za mapato ya Serikali hakitakiwi
kuuzwa na kufanyiwa matengenezo na mtu binafsi.
Mpina alibainisha kuwa utafiti uliofanywa na Mtandao wa
Kimataifa wa Global Financial Integrity (GFI), umebaini kuwa Tanzania
inapoteza Sh3trilioni kila mwaka kutokana na mzunguko wa fedha haramu.
“Kamati inataka taarifa ya mabilioni ya fedha
zilizofichwa katika Benki za Uswisi iwasilishwe mapema kabla Bunge
halijaisha ili kuwawezesha wabunge na wananchi kujua ukweli wa jambo
hili,” alisema.
Waziri Kivuli
Akizungumzia mikopo Mbatia alisema: “Dhamira kubwa
ya kuruhusu Serikali kukopa ni kwa ajili ya miradi ya maendeleo, lakini
hakuna taarifa za kuridhisha kuhusu namna ambavyo fedha zinazokopwa
zinatumika katika uwekezaji wa maendeleo.”
Alisema Wizara ya Fedha imeshindwa kusimamia
viwango vya riba vinavyotozwa na mabenki kwa maelezo kuwa vinapanda
wakati mfumuko wa bei umeshuka kutoka asilimia 19 mwaka 2011 hadi
asilimia sita Machi, mwaka huu.
“Deni la Taifa limeongezeka kutoka Sh9.3trilioni
hadi Sh22.2 trilioni Aprili, mwaka huu. Takwimu zinaonyesha kuwa deni
lote la taifa la ndani na nje limefikia Sh28trilioni.”
Awali, Waziri wa Fedha, Saada Mkuya aliwasilisha
Bajeti ya wizara hiyo ambayo ni Sh5.8trilioni, kati ya hizo, Sh66bilioni
ni kwa ajili ya matumizi ya kawaida na Sh29.8 kwa ajili ya matumizi ya
miradi ya maendeleo.
Alisema Hazina imetengewa Sh1trilioni kwa ajili ya matumizi ya kawaida na Sh47bilioni kwa ajili ya matumizi ya miradi.
“Sh4trilioni zimetengwa kwa ajili ya kulipia deni
la taifa, Mhasibu Mkuu wa Serikali ametengewa Sh82bilioni kwa matumizi
ya kawaida Sh7.9bilioni kwa ajili ya matumizi ya miradi ya maendeleo,”
alisema.
Alisema Tume ya Pamoja ya Fedha imetengewa
Sh2.3bilioni, Kitengo cha Udhibiti wa Fedha Haramu kimetengewa
Sh2bilioni kwa matumizi ya kawaida na Sh195bilioni kwa ajili ya matumizi
ya maendeleo.
Alisema Ofisi ya Msajili Hazina imepewa Sh88bilioni kwa matumizi ya kawaida na Sh1.9bilioni kwa ajili ya miradi ya maendeleo.
Wabunge waiponda Bajeti
Wakichangia bajeti hiyo, Mbunge wa Igunga (CCM), Dk Peter Kafumu
alisema shida kubwa iliyopo ni kwamba fedha hazitoki Hazina. “Mwisho wa
mwaka tunakuwa na fedha zimetoka asilimia 20, 40, sasa tutaweza
kuendesha kweli miradi namna hii?
Mbunge wa Nkenge (CCM), Asumpta Mshama alisema
tatizo kubwa la fedha zinazoidhinishwa na Bunge kutokwenda kwa wakati
linatokana na bajeti ya Serikali kuzingatia fedha taslimu.
Mbunge wa Viti Maalumu (Chadema), Christina
Mungway alisema hali ya kutopeleka bajeti kwa wakati inasababishwa na
mambo mengi ikiwamo kutokuwapo kwa vyanzo vya mapato vya kutosha.
Mbunge wa Kasulu Mjini (NCCR-Mageuzi), David
Kafulila alisema kuna changamoto kubwa kwa Serikali kushindwa kukusanya
mapato yake... “Ifike wakati tuwe na mkakati mkubwa wa kuhakikisha kuwa
maeneo yote ambayo hayakusanywi kodi yanakusanya.”
Alitoa mfano wa Mgodi wa Mwadui ambao tangu nchi
ipate uhuru mwaka 1961 wanasema hauapati faida lakini wanaendelea kuwepo
nchini.
No comments:
Post a Comment