Hamis Tambwe |
Tambwe ameliambia Maandishi wa habari kwa njia ya simu
kutoka Bujumbura kwamba jambo la kwanza atakalomweleza rais mpya wa
Simba baada ya kumpongeza kwa ushindi ni kutaka alipwe fedha zake za
usajili zilizobaki.
Lakini hataishia hapo atataka kujua kuwa mshahara wake wa Dola 800(Sh1.3milioni) utaongezwa kwa asilimia ngapi.
Mchezaji huyo aliyeifungia Simba mabao 19 katika
msimu uliopita wa Ligi Kuu Bara na kutwaa tuzo ya Mfungaji Bora,
aliongeza kwamba atauambia uongozi huo ubadilishe baadhi ya vipengele na
kuboresha mkataba wake vinginevyo hatakuja Dar es Salaam.
Alisema mgombea yeyote atakayeshinda nafasi ya
urais kati ya wawili waliobaki awe Evans Aveva au Andrew Tupa
waliopitishwa kuwania nafasi hiyo, atapaswa kuweka mambo sawa kwa vile
ana ofa kadhaa alizopata DR Congo lakini anaisikiliza Simba kwanza.
“Simba wananijua mimi siyo msumbufu, lakini
natambua kuwa sasa wapo katika uchaguzi, kwa nafasi yangu ya mchezaji
hainihusu sana, ninachotaka kwa yeyote atakayeshinda katika urais
anihakikishie mambo yangu kwanza,” alisema Tambwe ambaye habari za ndani
zinadai kwamba ulipomalizika msimu uliopita alianza kushinikiza
aongezewe mshahara baada ya kujigundua amezidiwa na wachezaji wengine wa
kigeni.
“Sitaki maneno Simba wajue kwamba, nataka
kuboreshewa mshahara wangu kwa maana nguvu na mchango wangu kwa timu
wameviona. Jingine ni kupatiwa nusu yangu ya fedha za usajili kwa wakati
pia hata mshahara uwe unakuja kwa wakati, hayo nitazungumza na huyo
rais mpya atakayeshinda vinginevyo sitakuja kirahisi,”aliongeza mchezaji
huyo.
Utafiti wa Mwanaspoti katika klabu zote 14
zinazoshiriki Ligi Kuu Bara umeonyesha kuwa klabu tatu; Azam, Yanga na
Simba ndizo zinazolipa wachezaji wake mishahara mikubwa zaidi nchini.
No comments:
Post a Comment