Friday 20 June 2014

Vitambulisho vya kupiga kura kubadilishwa

Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), Jaji Mstaafu Damian Lubuva akizungumza na wahariri wa vyombo vya habari Dar es Salaam jana. Kulia ni Mkurugenzi wa Uchaguzi wa Tume hiyo
Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), imetangaza matumizi ya teknolojia mpya ya Biometric Voter Registration (BVR), katika maboresho ya Daftari la Kudumu la Wapigakura ambayo yatafuta matumizi ya vitambulisho vya kupigia kura vya sasa.
Kwa hatua hiyo, Mwenyekiti wa NEC, Jaji Damian Lubuva ametangaza kuwa: “Katika kura ya maoni ya Katiba Mpya na Uchaguzi Mkuu wa 2015, mpigakura atatumia kitambulisho kipya atakachopatiwa na Tume baada ya kuandikishwa upya katika mfumo huu na si vinginevyo.
Vitambulisho vilivyotolewa katika uandikishaji na uboreshaji uliopita havitatumika tena.”
Akitangaza mpango huo mpya Dar es Salaam jana, Jaji Lubuva alisema Tume hiyo itaanza maboresho ya daftari hilo kwa watu wote wenye sifa za kupiga kura Septemba mwaka huu na kukamilisha kabla ya kura ya maoni ya Katiba na Uchaguzi Mkuu 2015.
BVR ni mfumo wa kuchukua taarifa za mtu za kibaiolojia hasa alama za vidole.
Mwaka 2004, NEC ilianzisha Daftari la Kudumu la Wapigakura ikiwa ni pamoja na ukusanyaji wa taarifa za wapigakura na uhifadhi wa taarifa za kielektroniki.
Sanjari na hilo, tume hiyo ilitoa vitambulisho vya wapigakura ambavyo pia vimekuwa vikitumika kwa shughuli mbalimbali za utambulisho katika maeneo kama benki, polisi, mahakamani, uhamiaji, ukataji leseni, usajili wa simu na mengineyo.
Jaji Lubuva alisema katika kazi hiyo ya uandikishaji, NEC imekusudia kutumia Sh293 bilioni kwa ajili ya ununuzi wa vifaa, mafunzo ya watendaji na uandikishaji.
Maofisa watakaotumika katika uandikishaji ni pamoja na waratibu wa uandikishaji wa mkoa, maofisa waandikishaji ambao watakuwa ni wakurugenzi wa halmashauri, maofisa wasaidizi watakaokuwa watatu kwa kila jimbo, watendaji kata na waratibu wa elimu.
Mafunzo kwa watendaji hao yanatarajiwa kuanza Julai, 2014 na uandikishaji utaanza Septemba na katika vituo 40,015 kote nchini.
Vituo vya uandikishaji
Jaji Lubuva alisema kwa utaratibu wa sasa, vituo vya kujiandikishia vimeongezeka kutoka 24,919 hadi 40,015 ambavyo vimewekwa katika ngazi za vitongoji, vijiji na mitaa ili kuwezesha kuwa karibu zaidi na wananchi.
“Kwa kutumia mfumo huu, wananchi wote wenye sifa za kuwa wapiga kura na wale walio na kadi za mpigakura za sasa watatakiwa kuandikishwa upya… Uandikishaji utafanyika kwa siku 14,” alisema
Changamoto
Mfumo BVR uliwahi kutumika katika nchi mbalimbali na kuripotiwa kushindwa kukamilisha shughuli hiyo kutokana na sababu kadhaa za kiufundi au ukosefu wa umeme.
Akizungumzia changamoto hizo, Mkurugenzi wa NEC, Julius Malaba alisema Tanzania haitakuwa ya kwanza kuutumia kwani ulishatumiwa na nchi za Nigeria 2007, Ghana 2009, Liberia 2005, Guinea 2005, Mali 2005, Uganda 2008, Kenya 2013, Zambia 2008, Afrika Kusini na Zanzibar 2009.
“Tanzania itatumia mfumo huu katika uandikishaji wa Wapigakura tu. Matatizo yaliyojitokeza katika nchi hizo hayakusababishwa na mfumo wa uandikishaji,” alisema Malaba na kuongeza.
“Changamoto kubwa ambayo ni ya kiteknolojia na kimiundombinu ni jinsi ya kusafirisha taarifa za wapiga kutoka kituoni hadi kwenye ‘seva’ ambapo baadhi hutokea zikiwa pungufu.
“Tatizo hili liliikumba Kenya kwenye Uchaguzi Mkuu 2013 na husababishwa na kukosekana au kuwapo mtandao hafifu wa simu za mikononi…”
Alisema changamoto za mfumo uliopita ni pamoja na kuwapo kwa majina ya watu waliofariki dunia katika daftari, majina ya wapigakura kutoonekana kwenye daftari kwa watu waliojiandikisha huku wakiwa na kadi.
Nyingine ni kushindwa kurekebisha taarifa za waliotaka kurekebisha au kuhamisha endapo mpigakura amehamia sehemu nyingine na kuwapo kwa majina ya wapigakura waliojiandikisha zaidi ya mara moja na ambao taarifa zao kama vile dole gumba hazikuchukuliwa kwa usahihi.
“Changamoto hizi zilisababisha daftari kulalamikiwa na wadau mbalimbali wa uchaguzi kwa kuhoji usahihi wake na hivyo kutokuaminika. Hizo ndizo zilizoisukuma Tume kufikiria teknolojia itakayosaidia kuziondoa,” alisema Malaba.

No comments: