MBUNGE
wa Singida Mashariki, Tundu Lissu (CHADEMA), ameilaumu serikali kwa
kutoa fedha za miradi ya maji kwa kupendelea baadhi ya maeneo wanayotoka
viongozi.
Lissu, alitoa lawama hizo jana bungeni alipokuwa akichangia bajeti ya
Wizara ya Maji, kwa mwaka 2014/2015 iliyowasilishwa na Profesa Jumanne
Maghembe.
Alisema mgawo wa fedha hizo unaonyesha kuwa mikoa yenye vyanzo vya
uhakika na nafuu ya maji, imetengewa fedha nyingi kuliko mikoa yenye
hali mbaya na isiyo na vyanzo vya maji.
Akitolea mfano, Lissu alisema mikoa yenye hali mbaya kama Dodoma,
Singida, Shinyanga, Shimiyu imetengewa fedha ndogo ukilinganisha na
mikoa yenye nafuu ya maji kama Tanga, Kilimanjaro, Mtwara na Mbeya.
Alisema mgawanyo wa fedha za miradi ya maji umefanywa kwa upendeleo
kwani maeneo ya mawaziri yametengewa fedha nyingi kuliko maeneo ya
wabunge.
“Mwaka huu, Mkoa wa Dodoma, umetengewa sh bilioni 7, Singida sh
bilioni 3, Shinynga sh bilioni 3, Simiyu bilioni 5, lakini mikoa yenye
nafuu ya maji kama Tanga sh bilioni 10, Kilimanjaro bilioni sita, Mbeya
sh bilioni tisa, Mtwara bilioni saba.
“Mheshimiwa Mwenyekiti, Wilaya ya Mwanga anayotoka Waziri Maghembe
peke yake imetengewa sh bilioni 1.5, wilaya ya Makete anayotoka
aliyekuwa Naibu wako Binilith Mahenge, imetengewa bilioni moja, lakini
wilaya kama ya Mkalama imetengewa sh milioni 100 tu. Huu upendeleo huu,
ni hatari sana na waziri atupe majibu.
“Maelezo yaje kwanini mikoa yenye hali mbaya ya maji inapata fedha
kidogo kabisa, na ile yenye nafuu, inapata fedha nyingi, lakini mikoa
yenye mawaziri ina bajeti kubwa zaidi,” alisema Lissu.
Naye Mbunge wa Mbozi Magharibi, David Silinde (CHADEMA), alisema
maeneo wanayotoka mawaziri na manaibu wao wamekuwa wakijitengea fedha
nyingi za miradi ili kuyanufaisha.
Alisema wakazi wa Wilaya ya Momba ni wengi, lakini fedha zilizotengwa
kwenye miradi ya maji ni kidogo zaidi kuliko Mwanga anakotokea Waziri
Maghembe, ambako kuna watu wachache zaidi.
Naye Mbunge wa Ubungo, John Mnyika (CHADEMA), ameibana serikali itoe
kauli juu ya chanzo cha kifo cha Meneja Biashara wa Petroli wa Mamlaka
ya Udhibiti wa Nishati na Maji (EWURA), Julius Gashaza.
Mnyika alisema Gashaza, aliripotiwa kujiua akiwa hotelini jijini Dar es Salaam baada ya kutoka kuhojiwa na Kamati ya Bunge.
“Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa vile wizara hii inahusika na EWURA,
waziri atakapokuja kutoa majibu, aeleze chanzo cha kifo hicho,” alisema
Mnyika.
Akitoa maoni kuhusu Bajeti ya Wizara ya Maji, Mnyika alisema njia
bora ya kumsaidia Waziri Maghembe ni kuikataa bajeti ya mwaka huu wa
fedha ili serikali ikajipange upya.
Alisema kila mbunge aliyechangia hoja kwenye bajeti ya wizara hiyo,
anakiri imetengewa fedha kidogo, lakini mwisho wa siku anamalizia kwa
kuiunga mkono.
Mnyika alisema Waziri Maghembe anaitwa mzigo, lakini hawezi kufanya
vizuri kama fedha zinazoidhinishwa na wabunge, zitaendelea kutolewa
kidogo.
No comments:
Post a Comment