Jenerali Fransisco Soriano Kamanda wa majeshi ya
Ufaransa katika Jamhuri ya Afrika ya Kati amesisitiza kwamba majeshi ya
nchi hiyo yataanza kuondoka nchini humo tarehe 15 Septemba mwaka huu.
Majeshi ya Ufaransa yalipelekwa Jamhuri ya Afrika ya Kati mwezi Disemba
mwaka jana baada ya kushadidi mapigano Bangui, mji mkuu wa nchi hiyo ya
Kiafrika. Rais Francois Hollande wa Ufaransa alidai kuwa, operesheni
hiyo ilifanyika kwa lengo la kuisaidia serikali ya Bangui na kulinda
maisha ya raia wa nchi hiyo. Hivi sasa nchi hiyo ya Magharibi imetangaza
azma ya kuondoa majeshi yake nchini humo, baada ya kuyapeleka huko
miezi sita iliyopita. Inafaa kuashiria hapa kuwa, mwezi Aprili mwaka
huu, Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa lilipitisha azimio jipya
baada ya hali ya kibinadamu kuwa mbaya nchini humo na hasa wimbi la
mauaji yaliyofanywa na kundi la wanamgambo wa Kikristo la Anti Balaka
dhidi ya Waislamu wa nchi hiyo. Kwa mujibu wa azimio hilo, iwapo jamii
ya kimataifa haitatoa radiamali ya haraka kuhusiana na hali mbaya ya
Jamhuri ya Afrika ya Kati, kuanzia tarehe 15 Septemba mwaka huu,
kitapelekwa mjini Bangui kikosi cha wanajeshi wa kulinda amani wapatao
elfu kumi na askari polisi elfu moja mia nane. Ban Ki moon Katibu Mkuu
wa Umoja wa Mataifa na mashirika ya kutetea haki za binadamu mara kadhaa
yametahadharisha juu ya uwezekano wa kutokea janga la kibinadamu nchini
humo. Umoja wa Mataifa mapema mwaka huu uliunda kamati iliyokuwa na
jukumu la kuchunguza kwa kina chanzo cha mauaji, unyama na ukatili
uliofanyika nchini humo. Uchunguzi huo utaweza kuweka bayana iwapo kile
kilichofanywa na wanamgambo wa muungano wa Seleka na wale wa Kikristo
wa Anti Balaka, ni jinai za kivita na dhidi ya binadamu au la. Baraza la
Usalama lilitahadharisha kwamba mashambulio ya kulipiza kisasi kati ya
Waislamu na Wakristo mjini Bangui, ni mwanzo wa kuibuka vita vya pande
zote, mauaji ya kimbari na kikabila nchini humo. Naye Bwana Mull Sebujja
Katende mwakilishi wa Uganda ambapo nchi yake ni mwenyekiti wa
mzunguko wa Baraza la Amani na Usalama la Umoja wa Afrika amesisitiza
kwamba moja ya vifungu vya baraza hilo ni kutiwa mbaroni na kufunguliwa
mashtaka wale wote waliotenda jinai kwenye nchi mbalimbali za Kiafrika.
Hivi sasa kuna makubaliano kati ya Baraza la Amani na Usalama la Umoja
wa Afrika na Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa juu ya ulazima wa
kufanyiwa uchunguzi wa kina matukio yote ya mauaji yanayofanyika barani
humo. Pamoja na hayo yote, hatua ya Ufaransa ya kupeleka wanajeshi wake
wasiopungua 2,000 huko Jamhuri ya Afrika ya Kati haikuweza kusaidia
kurejesha amani na utulivu nchini humo, bali ilichangia kwa kiasi
kikubwa mwendelezo wa mauaji ya kundi la Anti Balaka dhidi ya
Waislamu.
No comments:
Post a Comment