Wakati kukiwa na juhudi za watendaji wa Bunge maalumu la Katiba
kuwashawishi viongozi wa vyama vya siasa vya upinzani wawaruhusu wabunge
wao kurejea bungeni wakati vikao vya Bunge hilo vitakavyoanza Agosti 5
mwaka huu, bado utata umegubika kuhusu uwezekano wa kupatikana katiba
hiyo kwa wakati
Hata hivyo tayari Rais Jakaya Kikwete amesema kuwa
kama katiba hiyo haitapatikana sasa, Katiba ya Muungano mwaka 1977,
itaendelea kutumika.
Kwa wakati, siku na mara kadhaa zimefanyika juhudi
hizo bila ya kuzaa matunda, huku viongozi wa vyama vya CUF, Chadema na
NCCR-Mageuzi, wakionekana kuweka ngumu na kutoa masharti kwa Serikali
kama itataka warejee bungeni.
Ni dhahiri sasa msimamo huo umeendelea kuliweka
taifa katika wakati mgumu hasa inapoonekana kuwa matumaini ya kupata
Katiba Mpya yanaendelea kufutika.
Katibu wa Bunge Maalumu la Katiba Yahya Khamis
Hamad anatoboa siri ya Bunge kuchukua juhudi hizo na kusema hata hivyo
bado hazijazaa matunda na hadi sasa bado haijafahamika kama wabunge wa
kundi a Ukawa watarajea au la.
Hamad anazitaja baadhi ya hatua zilizochukuliwa
hadi sasa kuwa ni pamoja na Mwenyekiti wa Bunge la Katiba Samuel John
Sitta kukutana na viongozi wa vyama hivyo kwa nyakati tofauti, akiwamo
Makamo wa Kwanza wa Rais Zanzibar Maalim Seif Sharif Hamad mwenye
ushawishi mkubwa kwenye kundi la Ukawa.
Aidha, chama cha CUF ndicho chama chenye
Wawakilishi wengi katika Bunge la Katiba baada ya kuwa na wabunge wa
kuchaguliwa, wajumbe wa Baraza la Wawakilishi na wa kuteuliwa.
Akiwa Zanzibar, Sitta pia amekutana na Rais wa
Zanzibar Dk Ali Mohamed Shein chini ya agenda hiyo akihimiza na kuwataka
wajumbe hao kurejea na kuhitimisha ng’we iliyobaki.
Katibu wa Bunge la Katiba Mpya anabainisha kuwa
matayarisho ya Mkutano wa Pili wa Bunge maalumu la Katiba yameanza
kufanyika na kikao cha kwanza kinatarajiwa kuanza Agosti 5 mwaka huu,
huku wakiwa na matumaini kuwa kundi la Ukawa litarejea na kushiriki
vikao vya Bunge hilo.
Hamad anasema milango iko wazi kwa wabunge hao
kurejea na kushiriki Bunge hilo ili kusaka suluhu kupitia kamati ya
uongozi pamoja na ile ya maridhiano na kufikia mwafaka wa mvutano
uliojitokeza badala ya kundi hilo kubaki nje ya Bunge.
Katibu huyo anaeleza kuwa haamini kama kuendelea
kwa Ukawa kubaki nje ya Bunge ni njia sahihi na ya uhakika, badala yake
angetamani warudi bungeni ili madai hayo yakafanyiwe kazi.
Pia amesema hatua ya wabunge wengi wa makundi
maalumu miongoni mwa 201 kuendelea kubakia kwenye Bunge, ni jambo
linalotia faraja na matumaini kama njia inayoweza kurahisisha kupata
theluthi mbili ya wabunge wa Bunge hilo.
Kwa maoni na mtazamo wake, Hamad anasema kuondoka kwa wabunge wa
kundi la Ukawa hakujaathiri kutoendelea kufanyika kwa vikao vya Bunge
hilo ila kikwazo kitabaki katika upatikanaji wa theluthi mbili za uamuzi
wa vikao vya Bunge hilo kwa mujibu wa kanuni zilizopo.
Hamad anasema ikiwa hali ya kukosekana theleluthi
mbili itajitokeza, hakuna njia nyingine mbadala zaidi ya Katiba ya Nchi
ya mwaka 1977 kuendelea kutumika ikiwamo suala la mfumo wa serikali
mbili kuendelea kutumika na kukwama kwa utatuzi wa baadhi ya kero katika
Muungano.
Lipumba atoa neno
Mwenyekiti wa CUF Profesa Ibrahim Lipumba
ameuambia Mkutano Mkuu wa CUF kwamba kundi la Ukawa litakuwa tayari
kurejea bungeni ikiwa Rais Jakaya Kikwete atawaomba radhi Watanzania kwa
kupuuza maoni yao katika mchakato wa katiba. Profesa Lipumba alisema
ili Ukawa warejee bungeni na kushiriki vikao, Rasimu ya Mwenyekiti Jaji
Joseph Warioba isipanguliwe.
CCM imeshawishi na kufanikiwa kutupa baadhi ya
vipengele kwenye rasimu hiyo ikieleza kuwa siyo msaafu, Biblia au Sheria
ya nchi, anasema Profesa Lipumba.
ZEC: Hatujafanya matayarisho kura ya maoni
Mkurugenzi wa Tume ya Uchaguzi Zanzibar(ZEC) Salum
Kassim Ali anasema ZEC haijaanza matayarisho yoyote ya kura ya maoni
kwa upande wa Zanzibar kutokana na kile alichodai kutanda kwa giza nene
usoni mwa jambo hilo.
Salum amesema huwezi kuanza kufanya matayarisho ya
jambo kubwa kama hilo, huku ikionekana hakuna jambo la msingi
linalofanyika bungeni.
“Tunaweza kufanya matayarisho ya kura kama kutakuwa na dalili njema ya kupita kwa rasimu na siyo kama ilivyo sasa,” anasema.
Amesema ZEC inahitaji muda wa matayarisho ya jambo
hilo ikiwa ni pamoja na utoaji wa elimu ya uraia kwa upana wa kutosha
kwa wananchi na kukosoa mchakato wa kuitishwa kura ya maoni mwaka 2009
ulikuwa ni wa lipualipua na kukosa maandalizi ya kutosha ya jambo hilo.
Baadhi ya wakazi wa Zanzibar wameendelea
kugawanyika, huku wengine wakieleza kuwa kutopita kwa katiba hiyo,
kunaweza kuendelea kuikwamisha zaidi Zanzibar kujitanua kiuchumi.
Wamesema katiba hiyo haitakuwa na maana kama haitaheshimu kilio cha muda mrefu Wazanzibari cha Zanzibar na mamlaka kamili.
No comments:
Post a Comment