Tuesday 24 June 2014

Barabara ya Serengeti yazuiwa kujengwa

Kufuatia Mahakama ya Afrika Mashariki kuizuia serikali ya Tanzania kujenga barabara ya lami kupitia hifadhi ya Serengeti, wakazi wa maeneo hayo wamepinga uamuzi huo na kudai kuwa mradi wa barabara hiyo ni wa lazima na manufaa kwao.
Ujenzi huo umezuiwa na mahakama kufuatia taasisi mbalimbali za nje ya Tanzania kuweka pingamizi kwa madai kuwa ujenzi huo utaathiri mazingira, maisha ya wanyamapori na bayoanuai ya hifadhi hiyo.
Wakipinga uamuzi huo wa mahakama, wakazi wa maeneo hayo ambako barabara hiyo ya lami inatarajiwa kupita wamesema mahakama hiyo ya Afrika mashariki, pengine imepelekewa mashtaka yasiyo sahihi, na kutolea maamuzi masuala yasiyo wahusu.
Onesmo Olengurumwa, Makamu mwenyekiti wa Umoja wa Watu wa Ngorongoro, anasema walichotaka wao ni kutengenezewa barabara ya lami, kwa ajili ya kuharakisha maendeleo katika maeneo yao.
Shughuli ya ujenzi wa barabara
''Hatukuwa na mpango wa kutengeneza barabara kubwa yenye kupita magari mengi kwa mwendo wa kasi, kama ilivyoelezwa kwenye maelezo yaliyotolewa mahakamani’’.
Tanzania haitaki kuingiliwa
Amesema Tanzania haiwezi kuingiliwa katika kutengeneza barabara za wananchi wake kwa ajili ya maendeleo yao.
Hukumu hiyo ilitolewa baada ya taasisi inayoshughulika na masuala ya wanyama ya (Africa Network For Animal Welfare) ya nchini Kenya kufungua kesi dhidi ya Serikali ya Tanzania.
Kesi hiyo inalenga kupinga ujenzi wa barabara hiyo yenye urefu wa Kilomita 239, ikidai itaathiri mazingira, uhai wa wanyama na baioanuai katika hifadhi hiyo, ambaoo ujenzi wake utasababisha kuongezeka kwa shughuli za kibinadamu.
Watalii Serengeti
Kufuatia uamuzi wa taasisi hiyo kuipeleka mahakamani serikali ya Tanzania mbunge wa Ngorongoro Kaika Saning'o Telele aliitupia lawama nchi jirani ya Kenya kwamba ina mbinu za kukwamisha mipango ya maendeleo ya nchi yake kwa maslahi yake.
''Ndugu zetu wa Kenya , kila wakati serikali yetu inapokuwa na jambo kubwa inataka kulifanya kwa ajili ya wananchi, wamekuwa wakija na hoja za mazingira na wanyamapori, kama vile sisi hatuelewi masuala hayo’’
Kwa mujibu wa serikali ya Tanzania, barabara hiyo ingepitia Mto wa Mbu-Engaruka-Loliondo-Kleins Gate-Serengeti-Mugumu-Nata na kuungana na ile ya Tarime-Musoma-Mwanza, hivyo kupunguza adha ya usafiri kwa wananchi wa maeneo hayo ambao baadhi hulazimika kupitia Nairobi nchini Kenya.

No comments: