Balozi wa Uingereza nchini Tanzania, Dianna Melrose. |
Serikali imetangaza rasmi mgogoro wa kidiplomasia kati yake na Balozi wa Uingereza nchini ikimtaka kujieleza kwa madai ya kuingilia mambo ya ndani ya nchi.
Mgogoro huo ulitangazwa bungeni mjini Dodoma jana
na Naibu Waziri wa Nishati na Madini, Steven Maselle aliyemtaka balozi
huyo kufika Wizara ya Mambo ya Nje kujibu tuhuma hizo.
Kiini cha Serikali kumtuhumu balozi huyo ni hatua
ya Mbunge wa Kigoma Kusini, David Kafulila (NCCR-Mageuzi) kuihusisha
Uingereza na urejeshwaji wa Sh76 bilioni za chenji ya Rada.
“Katika mchango wake (Kafulila), ameongea jambo
moja nyeti sana na hili bora niliseme ili liwe fundisho kwa wengine… Hii
ni nchi huru baada ya mwaka 1961,” alisema Naibu Waziri.
“Zimekuwapo ripoti kwamba Balozi wa Uingereza
amekuwa akijihusisha kuratibu vikao mbalimbali katika Jiji la Dar es
Salaam na Dodoma kinyume cha utaratibu na hadhi ya kidiplomasia.”
Huku akionyesha kuwa na hasira, Maselle aliongeza
kusema: “Vikao hivyo vina malengo ya kuhujumu mipango na mikakati ya
maendeleo, ushahidi huo upo na utakapohitajika utatolewa.”
“Inasikitisha na kuchukiza balozi wa taifa kama
Uingereza akifanya vitendo kinyume cha maadili… Anahusishwa kushawishi
marafiki wa maendeleo wasitishe misaada ya kibajeti kwa
Tanzania,”alisema.
Balozi wa Uingereza
Hata hivyo, Mwananchi ilimtafuta Balozi wa
Uingereza Dianna Melrose, azungumzie suala hilo, msemaji wake Tamsin
Clayton ambaye ni Mkuu wa Kitengo cha Siasa, Miradi na Mahusiano alisema
wameshtushwa na taarifa hizo, lakini kwa sasa hawawezi kusema chochote
mpaka wafahamu chanzo cha tatizo.
Aidha Naibu waziri Maselle alisema kuwa hivi
karibuni Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa
(UNDP), alikuja Tanzania na kwamba upo ushahidi kuwa Balozi huyo wa
Uingereza, alitamka kuwa anafikiria kuishawishi Serikali yake isitoe
fedha za Miradi ya Maendeleo ya Millenia (MCC2).
“Ni aibu kwa Serikali ya Waziri Mkuu, David
Cameron kwa balozi wake kufanya uwakala wa Benki ya Standard Chartered,
kuishawishi Serikali ya Tanzania ikope fedha ili kulipa kampuni
binafsi,” alisema Maselle huku akipigiwa makofi na wabunge wengi wa CCM
na kuongeza:
“Rais Kikwete amelikataa kwa nguvu zote…, Serikali haiwezi kubeba mzigo wa kampuni binafsi.”
Alisema chini ya mkataba wa Vienna, katika vifungu vya 41 na 42
Serikali wakati wowote bila kuhojiwa kuhusu uamuzi huo, inaweza
kumtangaza mfanyakazi yeyote wa ubalozi au balozi kuwa hatakiwi na nchi
yake.
Maselle alisema na ikitokea hivyo na balozi huyo asirudishwe kwao, basi atanyimwa haki zote za kibalozi na baadaye kushtakiwa.
“Kwa kuwa kinga ya kushtakiwa inawalinda
wanadiplomasia wote, lakini mkataba huo wa Vienna unawataka mabalozi
kuheshimu sheria za nchi na kanuni zake,” alisisitiza Maselle.
“Kinyume chake Serikali inaweza kumfukuza balozi
anayefanya mipango ya kijasusi au kuhujumu Serikali na ustawi wa nchi
ama uchochezi wa uvunjifu wa amani,” alisema Maselle.
Aliongeza: “Kama ilivyojitokeza hivi karibuni
mkoani Mtwara, Serikali inamtaka Balozi wa Uingereza ajipime kama anafaa
na anatosha kuiwakilisha nchi yake hapa Tanzania.”
“Tanzania ni nchi huru hatutakubali kuburuzwa wala
kuingiliwa katika mambo yetu ya ndani yanayohusu ulinzi na usalama na
maendeleo ya wananchi wake,” alisema.
Waziri Maselle ameitaka Serikali ya Uingereza
ichunguze tuhuma dhidi ya balozi wake na kuchukua hatua zaidi ili
kuepusha mgogoro wa kidiplomasia unaoweza kukuzwa na balozi huyo.
“Tunamtaka Balozi wa Uingereza afike Wizara ya
Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa kujibu tuhuma hizo… Kuna mambo
mengi yanaendelea, nashukuru Kafulila leo ametufunilia,” alisema.
“Balozi anafanya mambo ambayo hayana hadhi ya
ubalozi…. Deni la IPTL ni la kampuni binafsi, inakuwaje balozi atuambie
tukope tulipe deni la kampuni binafsi?”Alihoji Maselle.
Itakumbukwa kuwa, wiki iliyopita kulisambazwa
ujumbe mfupi wa simu (SMS) ukimhusisha balozi huyo na njama za
kukwamisha Bajeti ya Nishati na Madini.
Muhongo amjibu Mnyika
Akijibu hoja za wabunge jana jioni, Profesa
Muhongo alisema aliifananisha taarifa ya Kambi ya Upinzani Bungeni
kuhusu bajeti ya wizara hiyo mwaka 2014/15 ni kama stori tu, huku
akifafanua mipango ya wizara hiyo.
No comments:
Post a Comment