WATU
kadhaa wamejeruhiwa na baadhi ya magari yameharibiwa baada ya kuzuka
kwa mapambano makali baina ya polisi na wafanyabiashara ndogondogo,
maarufu kama machinga.
Mapambano hayo yaliyochukua zaidi ya saa sita, yalilifanya Jiji la
Mwanza kutikisika kwa mabomu ya machozi na kugeuka uwanja wa mapambano
yaliyosababisha kufungwa kwa maduka, ofisi na kusimamisha shughuli za
kibiashara katika maeneo mbalimbali ya jiji kwa siku nzima ya jana.
Mmoja wa majeruhi aliyetambulika kwa jina la Fatuma Said, mkazi wa
Nyamanoro, alikimbizwa katika Hospitali ya Mkoa ya Sekou Toure baada ya
kugongwa na gari akiwa katika harakati za kukimbia vurugu hizo.
Mapambano hayo yalitokana na kitendo cha polisi pamoja na askari
mgambo wa jiji kubomoa vibanda vya biashara vya wamachinga katika eneo
maarufu la Makoroboi, katika kile kilichoelezwa kuwa ni kusafisha jiji.
Habari ambazo gazeti hili limezipata, zilisema kuwa wamachinga
walichukizwa na kitendo cha polisi na mgambo wa jiji kubomoa vibanda
vyao usiku wakiwa wamelala, na hivyo kushindwa kuokoa mali zao zenye
thamani ya mamilioni ya fedha zilizokuwa ndani ya vibanda vyao.
Akizungumza kwa uchungu huku akilia, mmoja wa wamachinga hao
aliliambia Tanzania Daima kuwa mali zao zenye thamani kubwa
zimeteketezwa na kuharibiwa vibaya na askari hao, ambao hawakuwaruhusu
kuchukua kitu chochote kutoka katika vibanda vyao.
“Kaka, wametuua, wamevunja mabanda yetu, wameharibu kabisa mali zetu na wamekataa katakata kuturuhusu kuokoa mali zetu.
“Wamevizia tumelala ndipo wakaja kufanya uharibifu huu. Kama wana
haki kwanini wasije mchana, wakaacha tukaondoa mali zetu na wao
wakaendelea na shughuli zao?” alisema machinga huyo ambaye hakuwa tayari
kutaja jina lake.
Imedaiwa kuwa wafanyabiashara hao walizuiwa kuokoa mali zao hata
baada ya kufika mapema eneo la Makoroboi, huku askari wa Jeshi la Polisi
na wale wa mgambo wakiweka ulinzi mkali kila kona ya kuingia ndani ya
soko hilo.
Hatua hiyo iliamsha hasira za wafanyabiashara hao ambao waliungwa
mkono na wenzao kutoka sehemu nyingine pamoja na raia waliokuwa
wakilaani hatua ya serikali kutumia nguvu kubwa za dola kupambana na
raia wasiokuwa na hatia.
Inadaiwa kuwa wafanyabiashara hao waliamua kujikusanya kwa nia ya
kuandamana kuelekea katika ofisi za Mkurugenzi wa Jiji, Hassan Hida,
kitendo kilichotafsiriwa na polisi kama maandalizi ya mashambulizi,
hivyo kuanzisha mapambano.
Mali zinazodaiwa kuharibiwa za wafanyabiashara hao wanaokadiriwa
kufikia 800 waliokuwa wanamiliki mabanda yao mbele ya nyumba za Shirika
la Nyumba la Taifa (NHC), ni pamoja na nguo, viatu, radio, vifaa vya
umeme, mabegi, vifaa vya ujenzi na televisheni.
Watu 10 washikiliwa
Akizungumza na waandishi wa habari,Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa
Mwanza, Christopher Fuime, alisema polisi inawashikilia watu kumi kwa
tuhuma za kusababisha uvunjifu wa amani, licha ya kukana kuwepo kwa
majeruhi kwa raia ama askari polisi.
Alisema wafanyabiashara hao wanaendesha shughuli zao kimakosa na kwamba eneo hilo limewekwa kwa ajili ya matumizi ya ziada.
“Kufanya zoezi hilo ni kuhakikisha mji wa Mwanza unakuwa na njia za
wazi na kuweka jiji katika mazingira yaliyo salama na kuhakikisha kila
mkazi anafuata sheria.
“Zoezi hili wananchi wanalifahamu kwa kuwa sio mara ya kwanza. Kuna
makundi yanayosababisha hizi vurugu na tumeyashughulikia,” alisema.
Kauli ya wananchi
Wananchi waliokumbwa na mkasa huo, wameliambia waandishi wa habari kuwa
ubomoaji huo sio wa haki na huenda kuna shinikizo la watu fulani
wanaotaka kumiliki eneo hilo kutokana na unyeti wake.
Mbele ya waandishi wa habari, mmoja wa wananchi waliodhurika katika
vurugu hizo, Joseph Mgaya, alisema kitendo cha polisi kurusha mabomu na
kupiga watu ovyo, ni cha kinyama.
Serikali yatoa kauli bungeni
Wakati Jiji la Mwanza likiwaka moto, mjini Dodoma, serikali
imeshindwa kutoa agizo la kusitiza operesheni safisha jiji hilo
iliyosababisha machafuko hayo.
Hoja kuitaka serikali isitishe operesheni hiyo ilitolewa jana na
Mbunge wa Nyamagana, Hezekie Wenje (CHADEMA), wakati akitoa taarifa ya
vurugu hizo bungeni.
“Hoja niliyonayo ni kwamba muda huu tulivyokaa hapa bungeni, mji wa
Mwanza umechafuka, mabomu yanapigwa kila sehemu, maduka yote yamefungwa
katika operesheni ya kuondoa wamachinga.
“Mheshimiwa Spika, operesheni ya aina hii, mwaka 2011 ilipofanyika
kwa kutumia polisi, kuna maisha ya watu yalipotea Mwanza, mwaka 2012
operesheni kama hii ilitokea na kuna watu walipata ulemavu wa kudumu
mpaka leo, na tambua kwamba suala la machinga ni la kitaifa, hivyo
naiomba serikali kutoa kauli ya kusitisha operesheni hiyo,” alisema
Wenje.
Akijibu hoja hiyo, Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Uratibu
na Bunge), William Lukuvi, alisema serikali inatafuta ukweli wa hali
halisi, na hivi sasa Waziri Mkuu anaendelea na mazungumzo kushughulikia
suala hilo ili liweze kumalizika.
“Mheshimiwa Waziri Mkuu alitoka kwenda kuzungumza na wahusika,
amekuja tu kupiga kura, tutachukua hatua kwa hili la Mwanza, lakini
hatuwezi kulitolea kauli hapa ya kusitisha operesheni hiyo, ila
tunaendelea kufanyia kazi na tutalitolea taarifa mara itakapokamilika,”
alisema Lukuvi.
No comments:
Post a Comment