Huku upinzani wa wananchi dhidi ya
serikali ukizidi kushika kasi nchini Jordan, askari wa usalama wa nchi
hiyo wametumia ukandamizaji katika kujaribu kuzima wimbi la maandamano
nchini humo. Wajordan ambao wanapinga siasa za serikali ya Amman hasa
katika masuala ya kisiasa na kiuchumi, kuongezeka uhusiano kati ya nchi
hiyo na utawala haramu wa Kizayuni wa Israel na kufuata kibubusa siasa
za Marekani katika eneo, wameeendelea kusisitizia upinzani wao kwa
viongozi wa serikali. Katika fremu hiyo wakazi wa mji wa Ma'an, kusini
mwa nchi hiyo hivi karibuni walifanya maandamano makubwa kwa kumiminika
mabarabarani na katika medani kuu za mji huo ambapo sambamba na
kusisitiza juu ya matakwa yao ya kimsingi, walitaka pia kukatwa kabisa
uhusiano wa nchi hiyo na utawala haramu wa Kizayuni na kadhalika
kuondolewa balozi wa utawala huo nchini mwao. Waandamanaji sambamba na
kuichoma moto bendera ya utawala huo haramu na ya Marekani, waliitaja
serikali ya Washington kuwa chanzo cha kuongezeka mgogoro ndani ya nchi
yao. Askari wa usalama wa Jordan kwa kutumia mabomu ya kutoa machozi na
risasi hai katika kuwatawanya waandamanaji, waliwapiga na kuwajeruhi
makumi kati ya waandamanaji hao sambamba na kutia mbaroni makumi ya
wengine. Kabla ya hapo pia, jeshi la nchi hiyo lilimuua kwa kumpiga
risasi kijana mmoja baada ya kuwashambulia waandamanaji wa mji huo wa
Ma'an, waliokuwa wakiandamana pia kupinga serikali ya nchi hiyo. Kitendo
hicho kinatajwa kuwa sababu ya kuitishwa maandamano ya hapo juzi mjini
hapo. Sambamba na kuanza kwa mapinduzi ya wananchi huko Tunisia na
Misri, Wajordan nao walianzisha maandamano ya kulalamikia hali mbaya ya
kimaisha na kutaka kufanyika marekebisho ya kimsingi katika muundo wa
uongozi wa taifa hilo la Kiarabu. Upuuzaji wa serikali ya Amman kwa
matakwa ya wananchi hasa upinzani wao kwa ufisadi mkubwa uliokita mizizi
nchini humo na hatua ya serikali ya kutowachukulia hatua kali wahusika
wa vitendo hivyo, ni jambo ambalo limeongeza wimbi la upinzani wa
wananchi dhidi ya serikali. Uzembe na udhaifu wa serikali, umepelekea
bunge la nchi hiyo hadi sasa kushindwa kuchukua hatua yoyote ya
kuboresha hali ya maisha ya wananchi, na badala yake wabunge wamekuwa
wakijinufaisha wao na kujaza matumbo yao wenyewe. Aidha kwa upande
mwingine ukimya wa baadhi ya makundi ya kisiasa ya upinzani nchini humo,
unatajwa kuwa sababu ya changamoto kwa mgogoro wa uchumi wa taifa hilo
suala lililomlazimu mfalme Abdullah wa II wa Jordan kutaka kutatuliwa
mkwamo wa kiuchumi na kifedha kuinuliwa kiwango cha uwekezaji ili kwa
mara nyingine nchi hiyo iweze kushuhudia ustawi wa kiuchumi. Takwa la
mfalme huyo linatolewa katika hali ambayo wataalamu wa masuala ya
kiuchumi wanaamini kwamba, Abdullah Ensour, Waziri Mkuu wa Jordan hana
tajriba ya kutosha kwa ajili ya kutatua mgogoro wa kiuchumi unaoendelea
kulikumba taifa hilo. Wanasema waziri mkuu huyo hana uwezo wa kuikwamua
nchi hiyo kutokana na mgogoro wa kisiasa unaoendelea kushuhudiwa ndani
ya taifa hilo. Uchunguzi wa matukio ya Jordan umebaini kwamba,
mabadiliko ya kiserikali yaliyofanyika hivi karibuni nchini humo
yalikuwa ya kimaonyesho tu na yaliyofanyika kwa lengo la kuzihadaa fikra
za waliowengi na kwamba, matatizo ya nchi hiyo hayawezi kupatiwa
ufumbuzi hadi pale wananchi watakaposimama na kudai haki zao za
kimsingi.
No comments:
Post a Comment