Thursday, 26 June 2014

Ghana yawafukuza Boateng na Muntari kwenye kikosi chao

Boateng na Muntari
Wachezaji wa kikosi cha timu ya taifa ya Ghana Sulley Muntari na Kevin Prince Boateng wamefukuzwa katika timu hiyo kwa ukosefu wa nidhamu.
Taarifa kutoka mtandao wa shirikisho la soka nchini humo imesema kuwa wawili hao wametimuliwa mara moja.
Boateng anayechezea kilabu ya Schalke 04 amefukuzwa kwa kutoa matamshi machafu yaliomlenga mkufunzi wa timu hiyo Kwesi Appiah wakati timu hiyo ilipokuwa katika mazoezi katika eneo la Maceio.
Naye mchezaji wa AC Milan Sulley Muntari ameadhibiwa kwa kumshambulia afisa mmoja wa kamati kuu ya timu hiyo
Shirikisho la soka nchini Ghana limeongezea kwamba kisa kinachomuhusu Muntari kilitokea siku ya jumanne na kumtaja Moses Armah,mwanachama wa usimamizi wa timu hiyo kama mtu aliyeshambuliwa na mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 29.
Wakati huohuo Boateng amedaiwa kutojali matamshi aliyoyatoa.Habari hizo zinajiri siku moja baada ya serikali ya Ghana kutuma dola millioni 3 nchini Brazil ili kuwalipa wachezaji wa timu hiyo nchini Brazil fedha zao za kushiriki katika michuano ya kombe la dunia.
Timu hiyo inayojulikana kama Black Stars ilikuwa imetishia kususia mechi kati yake na Ureno iwapo haitapewa fedha hizo swala lililoilazimu serikali kuingilia kati.
Ghana ina nafasi ya kufuzu katika michuano ya mchujo iwapo itaishinda Ureno na iwapo mshindi wa kundi G atakuwa Ujerumani.

No comments: