Sunday 22 January 2017

MKUU WA WILAYA YA HAI AZUIA SHAMBA LA MBOWE*

mwenyekiti wa Chadema Freeman mbowe akiwa anakagua shamba lake
MKUU wa Wilaya ya Hai mkoani Kilimanjaro, Gellasius Byakanwa, amesitisha shughuli za kilimo katika shamba la Kilimanjaro Veggies linalomilikiwa na Mbunge wa Jimbo la Hai, Freeman Mbowe, kutokana na kile alichosema kuwa shamba hilo lipo ndani ya chanzo cha maji ya Mto Weruweru.
Byakanwa alitoa amri hiyo jana baada ya kutembelea shamba hilo lenye ukubwa wa zaidi ya hekari mbili lililoko Kijiji cha Nshara na kukuta shughuli za kilimo zikifanyika.
Alisema Mbunge huyo pia alifanya uharibifu wa mazingira kwa kuvuna miti ya asili bila kibali cha Mkuu wa Wilaya kulingana na maamuzi ya Kamati ya Ushauri ya Mkoa (RCC) pamoja na kuvuta maji kwa kutumia mashine kinyume na kibali na taratibu za utumiaji wa maji ya mfereji.
“Nasitisha shughuli zote za kilimo zinazofanywa katika eneo hili ambalo ni chanzo cha maji ya Mto Weruweru kuanzia leo (jana) mpaka pale mamlaka nyingine zitakapojiridhirisha na utapaswa kulipa faini zote kulingana na sheria ya mazingira.

“Pia naliagiza Baraza la Taifa la Usimamizi wa Mazingira (NEMC), kufanya tathmini ya uharibifu wa mazingira katika eneo hili na kuchukua hatua pamoja na kuniletea taarifa walizochukua. Maofisa maliasili wa wilaya wafanye tathmini ya miti iliyokatwa bila kibali na kuleta kiasi cha faini ndani ya siku 14,” alisema Byakanwa.
Byakanwa alisema Mbowe ni kiongozi na ni kioo cha jamii hivyo haipendezi kufanya vitu kama hivyo kwani ni wajibu wa wananchi kuvitunza vyanzo hivyo na hakuna mradi utakaoruhusiwa kufanywa ndani ya mita 60 kutoka chanzo cha maji.
“Sitakubali kuona mazingira yanaharibiwa katika wilaya hii na kubaki kuwa jangwa wakati ndiko kwenye misitu mingi na misitu ndiyo chanzo kikuu cha kupata mvua,” alisema Byakanwa.
Alisema Januari 10, mwaka huu, alifanya ziara katika shamba hilo baada ya kupata malalamiko kutoka kwa wananchi na mamlaka ya bonde la maji na kujionea hivyo alimwandika Mbowe barua ya wito wa kufika ofisi ya Mkuu wa Wilaya Januari 13, akiwa na vibali vinavyomruhusu kufanya shughuli za kibinadamu katika chanzo hicho.
“Pamoja na kumwandikia barua hadi leo hajajibu na wala kufika ofisini kwangu kutoa maelezo, kitu ambacho kinaweza kuleta tafsiri tofauti tofauti,” alisema Byakanwa.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Kijjiji cha Nshara, Emanueli Mbowe, alisema zoezi hilo la kilimo lilianza mwaka jana na alielezwa na Mbowe kuwa anataka kuendeleza kilimo katika sehemu hiyo na kwamba ana vibali vinavyomruhusu kufanya shughuli hiyo.
MBOWE: TUNA HOFU
 Katika hatua nyingine Mwenyekiti huyo wa Chadema Taifa, Mbowe  alieleza hofu waliyonayo ya kutotendewa haki.
Mbowe alisema chama hicho kikuu cha upinzani nchini kina hofu kubwa kuhusu kutokutendewa haki viongozi wao kuanzia wale wa kitaifa, wabunge, madiwani, wenyeviti wa vijiji, wenyeviti wa mitaa na wale wa vitongoji pamoja na wanachama.
Kiongozi huyo wa upinzani aliyasema hayo jana mjini Shinyanga katika Mkutano Mkuu Maalumu wa chama hicho, Kanda ya Serengeti inayojumuisha mikoa ya Shinyanga, Mara na Simiyu.
Mbowe pamoja na viongozi wengine walikuwa wakihitimisha ziara yao ya kikazi Kanda ya Ziwa Victoria na Serengeti kwa kuchagua viongozi wapya wa kanda hiyo watakaoongoza chama hadi Uchaguzi Mkuu wa chama hicho.
Mbowe alisema nchi inapitia changamoto nyingi kwa kipindi hiki lakini kubwa zaidi ni hofu inayotamalaki ndani ya Taifa kwamba watu wameanza kujiona kuwa hawako salama.
“Kuna ambao wana hofu ya njaa, kuna ambao wana hofu ya kuporomoka kwa uchumi, kuwa watu ambao wana hofu za kiusalama, sisi kama chama kikuu cha upinzani tuna hofu kubwa kuhusu usalama wa viongozi wetu, tuna hofu kubwa kuhusu kutokutendewa haki viongozi wetu kuanzia viongozi wa kitaifa, kwenda kwa wabunge, madiwani, wenyeviti wa vijiji, wenyeviti wa mitaa hata na vitongoji pamoja na wanachama wetu.
“Tumeona namna viongozi wanavyohukumiwa vifungo katika mazingira ambayo si ya kawaida katika historia ya vyama vingi nchini, vile vile katika maamuzi ya mahakama,” alisema Mbowe.
“Tumeendelea kumwona rais wetu katika kipindi cha mwaka mmoja na miezi miwili, mitatu aliyokaa madarakani, anavyoendelea kutoa kauli za kuliogofya taifa, rais amekuwa si mtu mpatanishi wala si wa kutia moyo tena Watanzania” alisema Mbowe.
Alisema bado hawawezi kufanya mikutano ya hadhara kwa sababu imezuiwa kinyume cha Katiba kwani sheria nchini zinaruhusu.
“Ameendelea kutoa maamuzi mengi ambayo yanatia shaka, kuvitisha vyombo vya habari, kulitisha Bunge, kuwatisha watendaji wa Serikali. Watumishi  wa umma hawawezi kufanya maamuzi katika asasi wanazoziongoza kwa sababu hawajui wakifanya maamuzi bwana mkubwa atayachukulia vipi,” aliongeza Mbowe.
Mwenyekiti huyo wa Chadema alisema Rais anastahili kushauriwa kwa namna anavyolipeleka Taifa kwani Watanzania wameanza kukata tamaa hivyo ni wakati mwafaka wa viongozi wa chama hicho kusimama imara kupata haki nchini.

No comments: