Wednesday 25 January 2017

MAHAKAMA YAFUTA MASHTAKA YA KUBENEA

Dar es Salaam. Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu imeyaondoa mashtaka ya uchochezi yaliyokuwa yakimkabili Mbunge wa Jimbo la Ubungo, Saed Kubenea (46).
Hakimu Mkazi Mkuu, Wilbroad Mashauri, leo ameyaondoa mashtaka hayo mahakamani hapo kwa sababu hati ya mashtaka ilikuwa na utata na aiendani na kifungu cha 132 cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai (CPA).
Akitoa uamuzi huo, Hakimu Mashauri alisema kifungu hicho cha sheria kinataka kosa lielezwe kwa uwazi ' kinaga ubaga'.
Alisema katika kesi ya uchochezi iliyokuwa ikimkabili Kubenea ya kusambaza habari ya uongo yenye kichwa cha habari 'yuko wapi atakayeiokoa Zanzibar' ambayo ingeweza kuleta uvunjifu wa amani, Hakimu Mashauri alisema maneno hayo pekee kisheria siyo kosa.
Akiendelea kutoa uamuzi huo, Hakimu Mashauri alisema upande wa mashtaka ulishindwa kueleza maneno yenyewe hasa ya uchochezi yenye lengo la uvunjifu wa amani.
Hivyo, Hakimu Mashauri aliiondoa kesi hiyo mahakamani hapo na mshtakiwa akaachiwa huru na kwamba upande wa mashtaka unaweza kumshtaki upya.
Hata hivyo baada ya Kubenea kuachiwa huru alikamatwa na kupelekwa polisi kati na baadaye akaachiwa kwa dhamana.

No comments: