Rais wa Marekani Donald Trump anatarajiwa kutia saini amri kuu kuweka masharti kuhusu wahamiaji wanaoingia nchini humo.
Taarifa kutoka Marekani zinasema ataanza kwa hatua ya
kuimarisha usalama katika mpaka wa nchi hiyo na Mexico atakapozuru makao
makuu ya wizara ya usalama wa ndani baadaye Jumatano.
Aidha, anatarajiwa pia kutoa tangazo la kuidhinisha sheria
kali zaidi za kupata visa kwa wageni kutoka eneo la Mashariki ya Kati na
Afrika ambayo yana Waislamu wengi
Bw Trump ameandika kwenye Twitter kwamba leo itakuwa siku muhimu sana kwa usalama wa taifa la Marekani.
Mwandishi wa BBC David Willis kutoka Washington anasema
hatua hiyo huenda ikayaudhi mashirika ya kibinadamu na yale ya kutoa
misaada ikizingatiwa mzozo unaoendelea kwa sasa kuhusu hali ya wakimbizi
wa Syria.
Wakati wa kampeni yake ya urais, Donald Trump aliahidi kufanyia mageuzi suala la uhamiaji Marekani.
Aligusia ujenzi wa ukuta kati ya Mexico na Marekani kuzuia
wahamiaji haramu na kuwapiga marufuku Waislamu kuingia katika taifa hilo
kama sehemu ya vita dhidi ya ugaidi. Baadaye alibadili msimamo kidogo
na kufafanua kwamba watakachofanyiwa Waislamu ni kufanyiwa ukaguzi mkali
kabla ya kuruhusiwa kuingia Marekani.
Anatarajiwa kufika katika wizara ya usalama wa ndani
baadaye leo na anatarajiwa kusaini maagizo hayo ya kuimarisha usalama
katika mpaka wa Mexico na taifa lake na baadaye wiki hiii taarifa
zinaashiria atawajibikia ahadi yake ya kupunguza idadi ya wakimbizi
wanaoingia Marekani.
Na hiyo ni hadi pale ukaguzi mkali utakapoanzishwa na
kuzuia raia wa mataifa saba ya Afrika na kutoka eneo la Mashariki ya
Kati yote yalio na idadi kubwa ya waumini wa Kiislamu.
Ubaguzi wa kidini unapigwa marufuku kwa mujibu wa katiba ya
Marekani lakini inadhaniwa utawala wa Trump utaidhinisha marufuku hiyo
kwa misingi kwamba ni hatua za dharura kukabiliana na tishio lililopo la
ugaidi.
Awali, Bw Trump aliandika kwenye Twitter kueleza
kusikitishwa kwake na kiwango cha juu cha ghasia na mauaji katika jiji
la Chicago.
Vyombo vya habari wiki hii viliripoti kwamba tayari watu 228 wamepigwa risasi na wengine zaidi ya 40 kuuawa mwaka huu.
Bw Trump ameandika kwamba iwapo watawala wa Chicago
hawatatua tatizo hilo la mauaji, basi atawatuma 'Feds' akimaanisha
maafisa wa FBI.
No comments:
Post a Comment