Sunday, 11 May 2014

Aliyewahi kuwa Kocha Msaidizi wa Simba, Mganda Richard Amatre ailalamikia SIMBA

Aliyewahi kuwa Kocha Msaidizi wa Simba, Mganda Richard Amatre amewasilisha rasmi barua ya malalamiko kwa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) akiidai klabu hiyo Sh17.2 Milioni.
Kwa nyakati tofauti, Amatre aliwahi kufanya kazi katika klabu ya Simba akiwa kocha msaidizi wa waliowahi kuwa makocha wakuu wa klabu hiyo Mganda Moses Basena na Mserbia Milovan Cirkovic.
Akizungumza na gazeti hili katika Makao Makuu ya muda ya TFF yaliyopo Posta jijini Dar es Salaam, Amatre alisema amefikia uamuzi wa kuwasilisha barua ya malalamiko TFF baada ya kuchoshwa na ahadi zisizotekelezeka kutoka kwa uongozi wa Simba.
Amatre alisema kiasi hicho cha fedha anachoidai Simba ni fidia inayotokana na hatua ya klabu hiyo kuvunja mkataba wake sambamba na aliyekuwa bosi wake, Milovan.
“Rage (Mwenyekiti wa Simba, Ismail Aden) amekuwa akinipa ahadi ya kunilipa, lakini hajatekeleza, ni afadhali basi wangenilipa kidogo kidogo, lakini hata hilo linaonekana kushindikana, ni jambo linalonisikitisha,” alisema Amatre.
Katibu Mkuu wa Simba, Ezekiel Kamwaga alipotafutwa kwa simu yake iliita bila kupokelewa, lakini msemaji wa klabu hiyo, Asha Muhaji alisema: “Sina taarifa kuhusiana na jambo hilo, nitawasiliana na uongozi wa juu ili kujua kama ni kweli anatudai na  anatudai kiasi gani.”
Katibu Mkuu wa TFF, Celestine Mwesigwa alipoulizwa alisema: “Hili ni suala binafsi zaidi, hivyo Amatre ndiye mwenye mamlaka ya kulizungumzia, isipokuwa tupo tayari kumsikiliza na hata huo upande wa pili kwani tunapenda kuona mambo haya yanamalizwa kiungwana.”
Wakati huo huo, Katibu Mkuu wa zamani wa Simba, Michael Wambura ametangaza nia ya kugombea nafasi ya Urais kwenye uchaguzi ujao wa Simba uliopangwa kufanyika Juni 29.
Wambura alisema Jumatatu atachukua rasmi fomu za kuwania uongozi.
Katika hatua nyingine fomu za Simba ambazo zimeanza kutoka jana, zimedoda baada ya mwanachama mmoja pekee Andrew Tupa  ndiye aliyejitosa kuchukua fomu ya kuwania nafasi ya Urais.

No comments: