Monday, 17 November 2014

Simba mpya yajengeka, yajipanga kuja kivingine

WIKIENDI iliyopita Simba ilikaa chini na kocha wake, Patrick Phiri na kujadili mambo kadhaa ya msingi ambayo yatarejesha hadhi ya Mnyama kuanzia Desemba 26 itakapoendelea na mzunguko wa kwanza wa Ligi Kuu Bara.
Tayari usajili wa dirisha dogo umeanza tangu juzi Jumamosi  na utamalizika Desemba 15. Phiri amechekecha orodha kwenye faili lake akawapa viongozi majina manne ya wachezaji wapya ambao anataka watue Msimbazi huku uongozi ukimsisitizia kwamba asiwe na wasiwasi na hilo bali  aseme jingine.
Habari za uhakika ambazo  zimepatikana ndani ya kikao cha pande hizo na kujiridhisha nazo ni kwamba kocha anawataka rasmi straika Ame Ally na beki Hamis Kessy wote wa Mtibwa Sugar pamoja na Danny Mrwanda ambaye ametangaza kuachana na timu yake ya Polisi Morogoro na kwamba kuanzia mwezi ujao atakuwa na timu mpya ingawa hajaitaja. Mbali na hao pia kocha huyo amewaambia wamnunue straika wa Uganda anayeichezea Gor Mahia ya Kenya, Dan Sserunkuma (pichani) ili kuchukua nafasi ya Mrundi, Amissi Tambwe ambaye licha ya kuwa na mkataba wa miezi sita huenda akang’oka Simba muda wowote na ameweka hilo wazi.
Tambwe hana raha na maisha ya Simba tangu kutua kwa Phiri ambaye hapendi kumuanzisha mchezaji huyo kwa maelezo kwamba hana nguvu na si msumbufu kwa mabeki tofauti na ilivyo kwa Sserunkuma.
Mbali na mapendekezo hayo ya kocha, uongozi kupitia Kamati ya Usajili ulimwambia kwamba una wachezaji wawili wa ziada. Wachezaji hao wawili ambao ni Said Morad wa Azam na Deus Kaseke wa Mbeya City watawasajili kama mapendekezo ya kocha yakiwashinda kutokana na gharama na matakwa ya wachezaji husika.
Lakini ambacho kinaweza kuwa furaha zaidi kwa mashabiki wa Simba ni kwamba wachezaji hao wote waliopendekezwa na uongozi pamoja na kocha wana uwezo wa kucheza kikosi cha kwanza.
Uongozi tayari umeanza mazungumzo na Sserenkuma ambaye msimu wa ligi ya Kenya aliokuwa akicheza umekwisha. Mmoja wa vigogo wa Simba alituammbia  kuwa viongozi pamoja na  matajiri wengine wa klabu hiyo wamechangishana kiasi cha Sh40 milioni ili kumsajili Kaseke aliyeonyesha uwezo mkubwa na Mbeya City msimu uliopita pamoja na kwenye mechi kadhaa za msimu huu.
Kocha Phiri alipoulizwa hakupenda kuzungumzia kwa undani mapendekezo aliyoyatoa, lakini aliushukuru uongozi wa klabu hiyo kwa kupitisha mapendekezo hayo hivyo anasubiri utekelezaji wake tu kwa sasa.
“Siwezi kuwataja wachezaji waliokubalika lakini nashukuru kuwa mapendekezo yangu yamepita, ni utekelezaji wa viongozi tu kwa sasa ili timu iwe ya ushindani,” alisema Phiri ambaye anakabiliwa na mechi ya Mtani Jembe dhidi Yanga Desemba 13.
Simba ambayo Rais wake, Evans Aveva ametangaza mapambano ya kurejesha heshima, tayari amembakiza Msimbazi Jonas Mkude aliyekuwa akiwindwa na Yanga na Azam na sasa anajipanga kuwapa mikataba mipya wachezaji wengine muhimu akiwemo Said Ndemla.

No comments: