Wakati Yanga wakiwapa mapumziko ya siku
10 nyota wake kabla ya kurejea kuanza maandalizi rasmi ya mechi ya ‘Nani
Mtani Jembe 2’, wapinzani wao, Simba, wamewapa mapumziko ya siku 14
huku wakitamba kikosi chao kuwa ‘fiti’ tayari kwa mchezo huo.
Timu hizo zinatarajia kushuka Uwanja wa Taifa,
Desemba 13, kuwania taji la ‘Nani Mtani Jembe 2’ linaloratibiwa na
wadhamini wakuu wa timu hizo, bia ya Kilimanjaro Premium Lager, ikiwa ni
mara ya pili tangu kuanzisha kwa kampeni hiyo.
Hadi jana, Simba ilivuna Sh17,900,000 dhidi ya Sh
62,100,000 za Yanga huku Novemba 11, Simba ikiwa nazo Sh 20,115,000
dhidi ya Sh59,885,000 za Yanga na Novemba 10, Simba Sh20,445,000, huku
Yanga wakivuna Sh 59,555,000.
Katibu mkuu wa Yanga, Beno Njovu alisema wao wameishaanza maandalizi ya mchezo huo, lakini si rasmi
Alisema wao wataanza kuyafanyia kazi baada ya
nyota wao kurejea toka mapumziko ya siku kumi baada ya ligi kusimama
kupisha michuano ya Chalenji.
“Vijana wetu tumewapa mapumziko ya siku kumi, na
wakirejea maandalizi yanaanza kwa ajili ya Mtani Jembe 2, tuna imani
tutafanya vyema katika mchezo huo,”alisema Njovu.
Ofisa habari wa Simba, Humphrey Nyasio alisema
kikosi chao mara baada ya ligi kusimama kimepewa mapumziko ya wiki
mbili, ambapo wanatarajia kurejea Novemba 21 kuanza maandalizi ya ‘Nani
Mtani Jembe2’.
Alisema baada ya kurejea vijana wao wataendelea na
maandalizi yao kama kawaida, huku akili zao zikiwa kwa ‘Nani Mtani
Jembe 2’ , mashindano ambayo wao ni mabingwa watetezi wa kampeni hiyo
baada ya mwaka jana, kuwabugiza Yanga mabao 3-1.
Aliwataka mashabiki kuiunga mkono kwa wingi klabu
yao katika kampeni hiyo, hasa katika kuvutana ili wazoe fedha zote,
yaani Sh 95milioni na kumwachia mtani (Yanga), Sh 5milioni pekee na
kwamba watarajie mabao matatu msimu huu.
Meneja wa Bia ya Kilimanjaro, George Kavishe
aliwataka mashabiki Simba wavutane zaidi ili kuipatia timu yao fedha
kwani hadi sasa wanazidiwa na Yanga.
No comments:
Post a Comment